Na Mathayo Kijazi
Wanaojigamba kutokana na afya, elimu, mali walizonazo, wametakiwa kuacha kufanya hivyo na kujiweka karibu zaidi na Mungu, kwani ndiye aliyewawezesha.
Wito huo ulitolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Teule la Bagamoyo, Mhashamu Stephano Lameck Musomba -OSA, wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya 5 ya Kwaresma, katika Parokia Teule ya Mtakatifu Anthony wa Padua – Nyeburu, iliyopo chini ya Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II - Buyuni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Afya, elimu, utajiri pamoja na mazuri yote uliyonayo, ni Mungu ndiye aliyekuwezesha kuvipata, ni Mungu ndiye aliyekufanya kuwa hivyo ulivyo. Na kwa sababu hiyo, kiri udhaifu wako mbele yake,” alisema Askofu Musomba.
Askofu Musomba aliwataka Waamini kuacha dhambi ya uzinzi pamoja na yale yote yasiyompendeza Mwenyezi Mungu, kwani hayo hayatoi utambulisho ulio bora mbele za Mungu.