Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha
Japhet

Japhet

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Vincent Mpwaji (katikati) akizindua ujenzi wa nyumba ya Mapadri katika Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga - Yombo Dovya jimboni humo, baada ya adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara. Wengine ni baadhi ya Viongozi wa Kamati ya Ujenzi.

Na Violet Tillya

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, amelitaka Kanisa Katoliki nchini kuamka kifikra na kuwazingatia zaidi watoto wa kiume katika suala la malezi na makuzi, akisema hali yao kwa sasa ni ya kutisha na inahitaji hatua za haraka.
Alisema hayo hivi karibuni wakati akitoa homilia katika adhimisho la Misa Takatifu kwenye warsha ya walei ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam, iliyofanyika katika Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata.
Alisema watoto wa kiume wameonekana kusahaulika na kutopatiwa kipaumbele katika baadhi ya maeneo ya jamii, tofauti na watoto wa kike ambao kwa mujibu wake, wamekuwa wakisaidiwa zaidi na kushika nafasi za mbele katika shughuli mbalimbali.
Askofu Mchamungu alisema hali hiyo imechangia baadhi ya watoto wa kiume kupoteza kujiamini ikilinganishwa na watoto wa zamani, jambo ambalo linaweza kuathiri maendeleo yao na nafasi yao katika jamii.
Warsha hiyo ilihudhuriwa na mamia ya walei wa Jimbo hilo, ambao pia walipatiwa mada mbalimbali zilizowasilishwa na Padri Prosper Kessy na Padri Rogatian Msafiri baada ya kumalizika kwa Misa, kwa lengo la kukuza maisha yao ya kiroho na maendeleo kwa ujumla.

Na Mathayo Kijazi

Katika kuzindua Jubilei ya Miaka 75 ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam ngazi ya Dekania ya Mtakatifu Thomas More, waamini wamekumbushwa kuitumia nafasi hiyo kuondoa changamoto za ubaridi wa kiimani na kutopokea Masakramenti, huku wakiwa wafariji kwa wenye shida na wanaopitia mazingira magumu katika maisha yao.
Hayo yalisemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Vincent Mpwaji, wakati wa homilia yake katika adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi huo, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mtakatifu Gaspar - Mbezi Beach, jimboni humo.
“Kwa hiyo ndugu zangu, kupitia nafasi hiyo ya Jubilei ya Miaka 75 ya Jimbo Kuu la Dar es Saalam, tumwombe Mungu ili atuondolee changamoto mbalimbali tulizonazo, hasa za ubaridi wa kiimani na kutopokea Masakramenti,” alisema Askofu Msaidizi Mpwaji.
Askofu huyo aliwakumbusha waamini kuitumia Jubilei hiyo kama fursa ya kuimarika kiimani, kimaadili, kiutume na hata katika Umisionari wao.
Alitumia nafasi hiyo kuwasisitiza kila mmoja ndani ya Dekania hiyo, kuimarika katika umoja na uthabiti kama familia ya Mungu katika Kanisa mahalia jimboni humo, huku wakiwa chachu ya kuleta upyaisho ndani ya Jimbo lao.

Na Mathayo Kijazi

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Vincent Mpwaji, ametoa wito kwa waamini kutotaka kusukuma makosa yao kwa wengine, badala yake wawe na nia thabiti ya kuyakubali na kuyasahihisha makosa hayo.
Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa homilia yake katika adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 107 katika Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga - Yombo Dovya, jimboni humo.
“Hata ukiwa umefanya kitu pale nyumbani, mama akikuuliza kwa nini umefanya hivi, unakataa unasema ‘Hapana, sio mimi’. Kwa hiyo tunakuwa na hiyo hali ya kusukumia makosa kwa wengine. Kwa hiyo ndugu zangu tunaalikwa kutokusukuma makosa yetu kwa wengine. Tuwe na nia thabiti ya kuyasahihisha makosa yetu pale tunapokosea,” alisema Askofu Mpwaji.
Askofu huyo aliongeza kuwa Mungu daima hutoa nafasi kwa mtu anayetaka kubadilika na kuanza upya, akiwaalika kila mmoja kubadilika na kuanza kufanya matendo mema ya kumpendeza Mungu.
Pia, aliwasihi vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kusema ‘Ndiyo’ ya kweli pale wanapopokea Sakramenti hiyo, ili kwa kusema hivyo, wasiwe watu wa kubadilika.
Pia, aliwasisitiza kuwa na nia moja katika maisha yao, ili lengo lao liwe moja la kumtangaza Kristo popote pale wanapokuwa.
Aliwasisitiza kila mmoja baada ya kupokea Sakramenti hiyo, kuwa mstari wa mbele katika kusema ukweli popote pale walipo, huku wakiepuka hofu wala woga, akitolea mfano wa ‘Nani amfunge paka kengele’.

Katika kuadhimisha Somo wa Kanda ya Mtakatifu Raphael Malaika Mkuu, Parokia ya Mtakatifu Kamili - Yombo Kiwalani, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, waamini wamealikwa kumwomba Mungu ili wafanane na Malaika katika kumtukuza na kumtumikia Mungu.
Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Kanuth Nyoni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Somo wa Kanda hiyo, iliyoadhimishwa parokiani hapo hivi karibuni.
Aliwaasa Wanakanda hao kuendelea kuwa wamoja katika kumtukuza Mungu, huku wakiyafanya yote katika utimilifu wake.
Pia, alitoa wito kwa kila mmoja kuwa kweli watu wa Mungu, wakiwa tayari kupeleka habari njema kwa kufuata nyayo za malaika zao.
Aidha, akiwaalika kuongeza umoja na mshikamano wao katika kuhakikisha Kanda na Jumuiya zao zinazidi kuwa imara.
Padri huyo alisema kuwa Mungu anawaona katika kila wanachokiwaza, huku akiwafanyia yale aliyowaahidia katika maisha yao.
Aliwataka kutambua kwamba licha ya kutowaona Malaika hao, bali watambue kwamba wapo, huku wakiiga na kufuata nyayo za Malaika hao.

Na Mathayo Kijazi

Kufuatia Kongamano la Roho Mtakatifu lililokuwa likifanyika katika viwanja vya Parokia ya Mtakatifu Antony wa Padua – Vigoa, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwinjilishaji Beatus Kabambe amewakumbusha waamini kwamba Mungu akithibitisha juu ya jambo fulani, hakuna wa kuzuia.
Aliyasema hayo wakati wa Kongamano hilo lililofanyika kwa siku 10 kuanzia Septemba 11 hadi 20, 2026 parokiani hapo.
“Mungu akithibitisha, hakuna wa kuzuia. Mungu akithibitisha, hata wakuloge, hutalogeka. Mungu akithibitisha, hata wakizuia kulia, utatokea kushoto. Mungu akithibitisha, hata wakiziba Mashariki, utatokea Magharibi. Mungu akisema ndiyo, imepita,” alisema Mwinjilishaji Beatus.
Aidha, aliwasihi Waamini wa Vigoa pamoja na wa Parokia za jirani, kuendelea kumwomba Mungu ili athibitishe yale wanayoyaomba katika maisha yao na kwamba yale wanayoyaomba yasiishie tu kwao, bali yathibitishwe na Mungu.
Vilevile, aliwaalika waamini kuongeza nguvu katika kusali na kuombea sadaka zao, kwani kwa kufanya hivyo, itawasaidia kuthibitishwa na Mungu kupitia sadaka hizo.
“Kuthibitishwa kwangu na Mungu kupitia sadaka. Yaani kupata kibali cha Mungu, kupata kwangu ‘Passport’ ya Mungu, kupata kwangu ‘Visa’ ya Kimungu. Wale wanaokwenda nje ya nchi, ili utoke nje ya nchi, mbali na vitu vingine vyote, kitu ambacho unatakiwa uwe nacho pale mpakani ni Hati ya Kimataifa ya Kusafiria.
“Sasa leo tunaongelea kuhusu sadaka. Sadaka nayo pia itazame kwa mtazamo huo, kwamba mbele ya Mungu tunaposafiri kutoka duniani kwenda mbinguni, sanjari na maisha ya Sakramenti, unahitaji pia maisha ya sadaka. Sadaka ione kama Passport, sadaka ione pia kama Visa,” alisema Mwinjilishaji huyo.

Na Mathayo Kijazi

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi OFMCap, amesema kuwa wito wa kujiibua mwenyewe si wito wa kweli bali ni wito bandia.
Aliyasema hayo katika homilia yake wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Daraja Takatifu ya Upadri kwa Shemasi Richard Mlay, CP, katika Parokia ya Mtakatifu Fransisko Ksaveri - Chang’ombe, jimboni humo.
“Ndugu zangu, wito wa kujiibua mwenyewe siyo wito wa kweli, huo ni wito ‘fake’. Huyu Shemasi anayepokea Daraja ya Upadri leo hakujiibua mwenyewe, bali ameitwa na Mungu,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Sambamba na hayo, Askofu Mkuu aliongeza kuwa wito una madai, sadaka na majitoleo yake na kwamba wito wa kweli ni ufuasi.
Alisema kuwa yeyote anayetaka kumfuata Kristo, anapaswa kutambua kwamba Kristo ni nani na anataka nini.
Aliongeza kuwa kila wito chimbuko lake ni Ubatizo na kwamba kila mmoja katika maisha yake ana wito wake.
Vilevile, alisema kuwa hakuna mtu mwenye mastahili ya kuwa Padri na kwamba kila Padri ameshirikishwa, kwani mwenye kustahili wito huo ni Kristo mwenyewe.

Na Celina Matuja

Waimarishwa wanatakiwa kuwa askari hodari wa Yesu Kristo kwa kujazwa nguvu na mapaji ya Roho Mtakatifu na kutumwa kuwa mashahidi wa Kristo, kama walivyoahidi walipopokea Sakramenti ya Kipaimara.
Hayo yamesemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Vincent Mpwaji, katika homilia yake wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya utolewaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa waimarishwa 42 iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Tomas Mtume Vigozi, iliyopo Mbagala, Dar es Salaam.
Alisema ili wafanikiwe kuwa mashahidi wa Kristo Yesu, kila mara wanapaswa kujitahidi kuungama dhambi zao ili wanapokwenda kushiriki Ekaristi Takatifu wawe katika hali ya neema, wampokee Yesu Kristo na kumruhusu akae ndani yao siku zote za maisha yao.
Alisema lengo la kusanyiko hilo ni kumshukuru Mungu kwa waimarishwa hao 42 waliompokea Roho Mtakatifu, kama Mitume walivyompokea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste.
Aidha, aliongeza kuwa kila mtu aliyebatizwa na kupokea Sakramenti ya Kipaimara ametumwa kuwa shahidi wa Kristo. Hivyo, jeshi la mashahidi wa imani linaendelea kuongezeka katika Taifa la Mungu.
Askofu Mpwaji alisema Yesu Kristo baada ya kufufuka, alikutana na Mitume wake na kuwapa maelekezo ya kubaki Yerusalemu mpaka watakapopokea nguvu ya Roho Mtakatifu kutoka juu.

Kufuatia ziara ya kitume ya kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni, Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Ufaransa, Kanisa limekusudia kuchochea nguvu mpya ya utendaji kwa kuanzisha jukwaa pana na la wazi la mawazo na matendo, ambapo waamini na wasioamini wanaweza kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Aidha, kati ya mambo muhimu ambayo Baba Mtakatifu Leo XIV anagusia wakati wa hija yake ya kitume nchini humo, ni pamoja na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ujenzi wa haki na amani; changamoto ya teknolojia ya akili unde sanjari na utambulisho wa Bara la Ulaya.

Papa alisema kuwa Ufaransa ni nchi ambayo inatakiwa kutumia tunu zake za kitamaduni, kibinadamu na kidiplomasia ili kugundua upya na kuimarisha mwelekeo wake unaozingatia utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na kukuza uhusiano na Mwenyezi Mungu, kwa kuzamisha mizizi ya Kikristo barani Ulaya na hatimaye kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha, ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na kusaidiana; majadiliano katika ukweli na uwazi; bila kusahau ushirikiano wa Kimataifa ambao kwa sasa unaonekana kudhohofu sana.
Katika muktadha huo, Papa aliadhimisha ibada ya Misa Takatifu katika ‘Uwanja wa maridhiano; yaani “Place de la Concorde”, akisema kuwa hilo ni jambo jema na la kupendeza ndugu wanapoishi pamoja kwa umoja, ili kutangaza ukuu wa Mungu; kwa kuwaimarisha waamini katika imani, kuwahimiza kung’aa zaidi, kushirikishana maisha ya uzima wa milele, amani na upendo
unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kumgeukia Kristo Yesu, chemchemi ya maji ya uzima, maji yanayozima kiu na kustawisha maisha na upendo wa Mungu.
Alisema kuwa hayo ni maji yaliyomiminwa mioyoni mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu waliyopewa, huku kiu ya kumtafuta Mungu ikiwa ndani kabisa ya mioyo ya waamini, kilio cha moyo mnyenyekevu na wenye shauku kubwa ambao kiu yake ya ndani kabisa na ya msingi wa kuwepo kwake inaendelea kukua na kupanuka.

Mwadhama Pietro Kardinali Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican na Waziri wa Mambo ya Nje, ameonya kuhusu hatari za maendeleo ya teknolojia kutokana na utu wa binadamu kuwa hatarini na AI, akisisitiza kwamba ushirikiano wa Kimataifa unahitajika ili kuzuia madhara makubwa kutokea.
Papa alisema hayo wakati akizungumza katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huko New York, Marekani, akitoa wito kwa Mataifa kupata rasilimali za kifedha, kiteknolojia na kibinadamu.
Papa alisema hayo wakati akizungumza katika Mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huko New York, akionya kuhusu hatari za maendeleo ya kiteknolojia.
“Wale walio na rasilimali za kiufundi na kiuchumi wanaweza kuweka maono yao wenyewe ya ukweli,” alisema Papa katika Mkutano huo unaoadhimisha Miaka 40 ya Azimio la Haki ya Maendeleo.
Kutoka Cairo hadi Jiji la Mexico, kutoka Xi’an hadi Roma, katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian na sasa huko New York, mjadala kuhusu Akili Unde unahusisha muktadha na mabara, ambapo kila moja likiwa na historia yake ya kiutamaduni au kidini na ndiyo kiini cha tafakari za Vatican, pia zilizochochewa na Papa Leo XIV mwenyewe katika Waraka wa Kitume wa Magnifica Humanitas.
Katika suala hilo, Kardinali huyo alinukuu onyo la Papa: “Ikiwa maendeleo ya kiteknolojia yatasonga mbele bila maendeleo yanayolingana ya kimaadili na kijamii, matokeo yake yanaweza kuwa ongezeko la rasilimali bila ukuaji wa ubinadamu.”
Kardinali Parolin, pia akikumbuka kuanzishwa kwa Mazungumzo ya Kimataifa kuhusu Utawala wa Akili Unde, alihitimisha kwa matumaini kwamba Jumuiya ya Kimataifa itatenda kwa uwajibikaji kwa kujadili kila mwaka, athari za kijamii, kiuchumi, kimaadili, kitamaduni, lugha na kiufundi za AI, kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kimataifa na mbinu bora.
Mada za maendeleo na uwajibikaji wa kimataifa pia zilijirudia katika hotuba ya Katibu Mkuu wa Vatican katika mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, kuadhimisha miaka 40 ya Azimio la Haki ya Maendeleo (Desemba 4, 1986).