DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Chama Cha Pool Tanzania (Tanzania Pool Association: TAPA) kimepata mwaliko kwa wachezaji binafsi kushiriki mashindano ya JOY Grand Masters Final yatakayofanyika kuanzia Machi 24 hadi 29 mwaka huu huko Qinhuangdao nchini China.
Katika mashindano hayo, Tanzania itawakilishwa na Melckzedeck Amadeus aliyemaliza kama mchezaji bora wa Bara la Afrika katika mashindano ya Afrika yaliyofanyika Afrika Kusini mwaka 2023.
Msemaji wa Chama hicho Akida Kilango alisema kuwa mchezaji atakayependa kushiriki katika mashindano hayo anaweza kupata fursa hiyo kwa kujigharamia nauli ya ndege kwenda na kurudi, malazi, pamoja na chakula.
Alisema kuwa mchezaji huyo atatakiwa kuwasiliana na TAPA ili kuweka mambo sawa juu ya ushiriki wake.
TAPA itamsaidia katika upatikanaji wa nyaraka muhimu ikiwemo mwaliko kwa ajili ya safari na itagharamia gharama ya kupata VISA.