Print this page

TGNP yaendelea kupinga ukatili

By February 09, 2024 1088 0

NA MWANDISHI WETU

Mtandao wa Jinsia Tanzania (Tanzania Gender Networking Program: TGNP) umesema kwamba utaendelea kutekeleza kwa kishindo mpango wake wa kupinga vitendo vya ukatili ili kutokomeza ukeketaji nchini.
Afisa wa Idara ya Ujenzi Nguvu za Pamoja na Harakati, Flora Ndaba, akizungumza katika Kongamano la kupinga vitendo hivyo alisema kuwa wamejadili mada mbalimbali na kuona kwamba kuna jinsi ya kuwekeza katika wanawake na kwa mabinti walionusurika kukeketwa.
Alisema kuwa wametumia Bonanza na Sinema ambayo imeandaliwa na Mtandao huo kwa lengo la kupaza sauti zao kuujulisha Umma kuhusiana na Janga hilo la ukeketaji.
“Tupo kwenye Soko la Kivule, na hapa tupo na wadau ambapo kuna sinema ambayo imeandaliwa na TGNP,” alisema Flora.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii, Magdalena Msaki alibainisha kwamba wao wamejipanga kuzuia ukeketaji, kwani kisheria hasa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, ukeketaji ni kosa la jinai.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, ukeketaji ni kosa la jinai, kwa hiyo tunataka kutoa elimu kwa jamii inayotuzunguka katika Kata hizi tatu,” alisema Magdalena.
Kwa upande wake mmoja wa Wanaharakati wa Masuala ya Jinsia, Seleman Bishangazi alisema kuwa wameamua kushirikisha Vijana kwa madhumuni ya kupaza sauti zao ili jamii itambue kuwa ni jambo baya, na hivyo kuachana na jambo hilo.
Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu “Sauti yangu, Hatma yangu” na kufanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam wilayani Ilala.

Rate this item
(0 votes)
Japhet