DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amekemea vitendo vya unyanyasaji wa watoto vinavyoendelea kufanyika nchini, akiwataka Waamini wenye tabia hiyo kuacha mara moja.
Aidha, Kardinali Pengo aliwasihi waamini kujitafakari na kuamua kumchagua Kristo, kwani ndiye muweza wa yote.
Kardinali Pengo alitoa rai hiyo katika homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Matawi iliyoadhimishwa hivi karibuni katika Parokia ya Mtakatifu Polycarp Askofu na Shahidi – Kilamba, jijini Dar es Salaam.
“Muwe tayari kuutangaza ukweli na kuwa katika upande wa haki siku zote. Simameni katika upande wa Yesu Kristp, kwa sababu kusimama upande wa Yesu, kunasaidia hata katika kuziimarisha Jumuiya zenu,” alisema Kardinali Pengo na kuongeza,
“…Kwa hiyo ndugu zangu msijisahau mkaamua kumtupa Kristo. Mnatakiwa kujitafakari na kuamua kumchagua Kristo katika maisha yenu yote. Kila mnachokifanya katika maisha yenu, hakikisheni kwamba mnamuweka Kristo mbele.”
Aidha, Kardinali aliwapongeza Wanakilamba kwa hatua mbalimbali walizopiga katika Parokia hiyo, huku akiwaombea kwa Mungu ili waweze kukamilisha kila mpango ulioko mbele yao parokiani hapo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo ya Kilamba, Padri Timoth Nyasulu Maganga alisema kuwa kabla ya hapo walikuwa na shauku kubwa ya kumwona Kardinali Pengo kufika parokiani hapo kwa ajili ya kuadhimisha Misa hiyo Takatifu ya Dominika ya Matawi.
Padri Nyasulu aliendelea kumwomba Kardinali Pengo watakapomwomba tena akaadhimishe Misa Takatifu katika Parokia hiyo, akubali, kwani bado wanamhitaji.
Padri Nyasulu alivishukuru vyombo vya habari ikiwemo Tumaini Media, kwa kuchukua habari juu ya Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Dominika ya Matawi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo, Herman Lyoba alimshukuru Kardinali Pengo, akisema kwamba kila anapowatembelea kwa ziara kama hiyo ya kitume, wamepiga hatua katika ujenzi wa nyumba ya Mapadri.