DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amesema kuwa watu wanaolitangaza jina la Mungu katika mazingira yoyote, hueleweka.
Kardinali Pengo alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Clara wa Asizi - Chamazi, jijini Dar es Salaam.
“Watoto wa Kipaimara, jitahidini sana kulitangaza jina la Mwenyezi Mungu katika maisha yenu. Watu wanaolitangaza jina la Mungu katika mazingira yoyote yale, watu hao hueleweka,” alisema Kardinali Pengo.
Aidha, Kardinali Pengo aliwasisitiza vijana waliopokea Sakramenti hiyo kutambua kwamba, lengo kuu la kupokea Sakramenti kuja kulitangaza Neno la Mungu.
Aliongeza kuwa siku watakaposahau kwamba lengo lao kuu ni kulitangaza Neno hilo, basi watajikuta wanaingia katika vurugu.
Wakati huo huo Kardinali Pengo, aliwaasa Waimarishwa hao kuepuka kuwa waoga, badala yake watambue kwamba wanasimama kwa niaba ya kundi lililoamini kuwa Kristo alifufuka katika wafu.
Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo aliwapongeza waamini wa Parokia hiyo, kwa kuwa na kanisa kubwa na la kisasa, akiwasihi kuongeza nguvu ili kukamilisha maboresho yaliyobaki kwa sasa.