DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddeus Ruwa’ichi, amewataka Waamini kujitathmini kikamilifu maisha yao, kama ni kweli ya Ukristo au ya ubabaishaji.
Wito huo aliutoa hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi, iliyofanyika parokiani hapo.
Askofu Ruwa’ichi alisema kuwa Mungu anampenda kila mmoja, na wala hana ubaguzi, chuki, lakini Waamini ndio wenye kumchukiza Mwenyezi kwa mambo mabaya wanayofanya.
Askofu Ruwa’ichi aliwasihi Waamini hao kuhakikisha wanabadilika na kuwa Wakrito wema, na wenye kupenda maendeleo ya Kanisa lao.
“Mimi na ninyi Wanaparokia hii ya Mtakatifu Nicholaus ni mapacha, pia ni ndugu, Mimi nilipata Daraja Takatifu la Uaskofu siku moja, na ninyi mnatangazwa kuwa Parokia, hongereni sana,”alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo,Padri Faustino Maganga, alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kukubali mwaliko wao, na kufungisha ndoa hizo.
Padri Maganga alisema kwamba amepokea maagizo yote ya Askofu Mkuu, na atajitahidi kuleta maendeleo katika Parokia hiyo.
Katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Parokia hiyo, Askofu Ruwa’ichi alifungisha Ndoa jozi 10.