LUSAKA, Zambia
Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Zambia (Zambia Conference of Catholic Bishops: ZCCB) limezindua Kampeni ya kufuta madeni ya Mwaka wa Jubilei 2025, ikitoa wito wa msamaha wa haraka wa deni, haki ya kiuchumi, na uwazi katika usimamizi wa madeni ya Zambia.
Uzinduzi huo ulifanyika katika Kapingila House mjini Lusaka nchini humo mwishoni mwa Mkutano wa Kwanza wa Baraza Kuu wa ZCCB kwa 2025, iliyokwenda na wito wa Baba Mtakatifu Fransisko wa haki ya kiuchumi na msamaha wa madeni duniani kote kama sehemu ya Mwaka wa Jubilei 2025.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais wa ZCCB, Askofu Mkuu Ignatius Chama wa Jimbo Kuu Katoliki la Kasama, alisisitiza tena msingi wa Kibiblia wa mapokeo ya Jubilei, akinukuu kitabu cha Mambo ya Walawi, 25:1-8 kinachosisitiza huruma, haki na ufufuaji wa jamii zilizoelemewa na madeni yasiyo ya haki.