Dar es Salaam
Na Mathayo Kijazi
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Austin Makwaia Makani Investment (AMMI), Austin Makani amewashauri Wafanyakazi wa Tumaini Media kuhakikisha wanawafahamu vyema wateja wao, kwani hiyo itawasaidia kufahamu bidhaa gani wateja wao wanazitaka.
Makani ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tumaini Media, aliyasema hayo alipokuwa akitoa mada katika Semina Elekezi kwa Wafanyakazi wa Tumaini Media kuhusu mambo ya Masoko ilioyofanyika hivi karibuni ofisini kwake Posta, jijini Dar es Salaam.
‘Kwanza kabisa ukimfahamu vyema mteja wako, basi utauza bidhaa yako. Ni lazima pia ujue kwamba mteja anahitaji bidhaa gani, na kwa wakati gani. Muuzie mteja bidhaa ambayo anaitaka, siyo bidhaa unayotaka wewe…
“Tuchukulie mfano kwa watu ambao pengine wanapenda sana kula ‘chips’, je, ukienda kuvua samaki baharini, kwenye ile ndoano yako unayotumia kuvulia, utaweka kipande cha ‘chips?’ hapana, lazima uweke kitu ambacho samaki anakipenda, siyo kitu ambacho unapenda wewe.
Kwa hiyo, hata kwenye biashara, uza kile mteja anachotaka, siyo unachotaka wewe, kwa sababu inawezekana unachotaka wewe, mteja hakitaki,” alisema Makani.