DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Imeelezwa kwamba endapo ikatokea Askari ama Mwanajeshi akafanya mauaji ya mtu ama watu katika vita vya haki, siyo dhambi.
Aidha, mauaji hayo yanapaswa kuwa katika zile jitihada zilizotumika kusuluhisha, lakini imeshindikana, kwani lengo la kufanya hivyo, ni kuimarisha amani katika maisha ya wanadamu.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Padri Paul Sabuni, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Ambrose – IPTL, Salasala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakati akitoa ufafanuzi wa swali alilodai kuulizwa na baadhi ya Waamini wanaofanya kazi ya Uaskari, wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa Wafanyakazi wa Sekta ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu – Makongo Juu, jijini Dar es Salaam.