Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, amewataka Viongozi wa Halmashauri ya Walei, wanaochaguliwa ngazi mbalimbali za Kanisa Katoliki, kufanya kazi za kitume na sio kuleta majungu, umbea na kuchonganisha Mapadri.
Wito huo aliutoa wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Rita wa Kashia - Goba Mwisho, iliyokwenda sambamba na kumsimika Paroko mpya wa Parokia hiyo Padri Festo Liheta.
Askofu Mchamungu alisema kuwa viongozi wengi wa Halmashauri ya Walei, huwa wanasahau majukumu yao waliyochaguliwa katika kazi ya Kanisa, bali utakuta wanafanya kazi za Paroko au Paroko msaidizi na kuwamiliki Makasisi hao, “Msifanye hivyo viongozi, bali fanyeni kazi mlizochaguliwa na Waamini, acheni malumbano kila wakati na Mapadri.”