BAGAMOYO
Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Mhashamu Stephano Musomba, alisema kuwa siasa ni neno zuri ila watu wameliharibu, kwa kutumia uongo na kupotosha.
Askofu Musomba alisema hayo wakati akitoa homilia yake, katika Ibada ya Ijumaa Kuu, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli-Bunju, jimboni humo.
“Ukweli mara zote unauma, japo unaponya na ni mchungu, ingali huwa ni mtamu kama asali, ikiwa utatenda katika mastahili ya ukweli,” alisema Askofu Musomba.
Aidha, aliwasihi Waamini kusikiliza kila wanachoambiwa, kwa sababu kitawafanya wawe bora zaidi, japokuwa wakati mwingine huzaliwa ‘machawa’, ambao kazi yao ni kusifia bila kukosoa, wakifanya hivyo kwa ajili ya kujipatia kipato tu.