DAR ES SALAAM
LAURA CRISPIN
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam limeanzisha Klabu ya michezo itwayo St. Joseph Sport Club’ ili kuimarisha shughuli za uinjilishaji kupitia michezo, kuboresha afya na kutoa ajira kwa vijana.
Akizungumza na Tumaini Letu katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni, Padri Vitalis Kassembo, Mkurugenzi wa Walei Jimbo Kuu la Dar es Salaam alisema kwamba kitu kilichowasukuma kuanzisha timu ya mpira wa miguu ya St. Joseph Sport Club ni kwa ajili ya muendelezo wa Warsha ya Walei.
“Tumeanzisha klabu ya St. Joseph Sports kwa lengo la kuinjilisha kupitia michezo, kuwafanya vijana wawe na afya nzuri pamoja na kuwapatia vijana ajira kupitia michezo, japokuwa siyo wote ni kwa wale wenye vipaji vya michezo,”alisema Padri Kassembo.
Alisema kuwa mara zote wamekuwa wakipoteza timu baada ya Warsha kuisha na kuwafanya kila mwaka kutafuta timu mpya.
Padri Kassembo aliendelea kusema kuwa wameanzisha timu hiyo kwa lengo la kuacha alama ya Jubilee ya Miaka 75 ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kujenga mwili wenye afya pamoja na Roho yenye afya.
Alibainisha kwamba klabu hiyo ya St. Joseph Sport inabebwa na kauli mbiu ambayo wataishi siku zote katika michezo, ambayo ni ‘Imani, Michezo na Ushindi’.
Padri Kassembo aliendelea kusema kwamba, ikiwa wataishi katika kauli mbiu yao ya imani, michezo na ushindi basi mapato yatakayopatikana kupitia timu hiyo, yataenda kusaidia ujenzi wa Kanisa mbadala Pugu.