VATICAN CITY
Wakristo wameitwa kuleta chachu ya ukarimu kwa ulimwengu, hasa katika ulimwengu unaoathiriwa kila mara na mantiki ya ubinafsi, huku wakifikiria na kuishi kulingana na mantiki ya kweli zaidi, ile ya ukuaji fungamani wa mwanadamu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Leo XIV, huku akiwaelekea Waamini katika kituo cha IFEMA, Madrid, ikiwa ni hotuba yake ya mwisho, kabla ya kuanza sehemu ya Pili ya ziara yake ya kitume nchini Hispania.
Hitaji la kufikiria na kuishi, kulingana na mantiki ya maendeleo fungamani ya binadamu, limesikika katika hotuba ya Baba Mtakatifu Leo XIV, akihitimisha hija yake mjini Madrid, kwa kukutana na watu wa kujitolea 17,000, katika Ukumbi wa 3 wa IFEMA, kabla ya kupanda Ndege kuelekea kwenye Mji wa Barcelona, ikiwa ni sehemu yake ya Pili ya ziara ya 4 ya Kitume nchini Hispania, iliyoanza tangu Juni 6 na kuhitimishwa Juni 12, kwa kutembelea pia Visiwa vya Kanari na Tenerife.
Banda hilo la 3 ni moja ya taasisi tano muhimu zaidi, za maonyesho ya biashara barani Ulaya, moja kuu nchini Hispania, ambapo alifika kwa gari katikati ya watu wa kujitolea, waliotambulika kwa rangi ya machungwa.
Katika hotuba yake Askofu huyo wa Roma, alianza na shukrani kwa Mwadhama José Kardinali Cobo Cano, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Madrid, kwa kaka na dada wapendwa katika Jimbo hilo.
Hapa wote walisikika wakitoa ukelele wa kusikitika, na Papa akaendelea. “Kila mmoja wenu na wengine wengi, ambao hawakuweza kuwa hapa asubuhi ya leo, wanastahili “shukrani” maalumu sana, kwa sababu mmetoa uwepo wenu na huduma yenu, na mmefanya hivyo kwa upendo kwa Bwana, Kanisa na Papa.”