Print this page

Kardinali Gugerotti awasili Ethiopia kwa ziara ya kichungaji

Kardinali Gugerotti akikaribishwa na mwenyeji wake Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Addis Ababa nchini Ethiopia. Kardinali Gugerotti akikaribishwa na mwenyeji wake Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Addis Ababa nchini Ethiopia.

VATICAN CITY

Mkuu wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki ya Vatican, Mwadhama Claudio Kardinali Gugerotti, amewasili nchini Ethiopia kwa ziara ya kichungaji na kitume, akiambatana na Padri Dmytro Sabadokh, Katibu Maalumu wa Rais, na Padri Jarozlav Lajciak, anayehusika na Makanisa ya Mashariki ya Ethiopia na Eritrea.
Baada ya kuwasili hivi karibuni, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole wa Addis Ababa, Kardinali Gugerotti alipokelewa na wawakilishi wa Maaskofu, Mapadri, Watawa, na Waamini Walei, wafanyakazi wa uwanja wa ndege, na baadaye katika Ubalozi wa Vatican.
Kardinali huyo baadaye alikaribishwa na Askofu Mkuu wa Metropolitan ya Addis Ababa, Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Ethiopia (CBCE), pamoja na Mapadri wa Jimbo katika Kanisa Kuu la Kikatoliki la Kuzaliwa kwa Bikira Maria, huku ikifanyika sherehe rasmi ya ufunguzi, kuashiria mwanzo wa ziara hiyo.
Kama sehemu ya mpango wake, Kardinali Gugerotti alitembelea Sekretarieti Kuu ya Mkutano wa Maaskofu Wakatoliki wa Ethiopia, ambapo alikutana na maafisa wakuu na wafanyakazi. Wakati wa ziara hiyo, alielezwa kuhusu huduma za Sekretarieti, na jukumu lake katika kusaidia shughuli za dayosisi kote nchini.
Katika ushirikiano muhimu wa kiekumene, Kardinali Gugerotti alikutana na Mtakatifu Abune Mathias I, Patriaki wa Kanisa la Orthodox la Ethiopia la Tewahdo, ambapo aliwasilisha ujumbe kutoka kwa Papa Leo XIV, na kuelezea furaha yake ya kuwa Ethiopia.
Naye Patriaki aliwakaribisha ujumbe huo, akawatakia kila la kheri kwa kukaa kwao, na kuwapa baraka zake, ambapo wakati wa majadiliano yao, viongozi wote wawili walitafakari kuhusu masuala ya amani duniani, na changamoto zinazowakabili Wakristo leo.
Walisisitiza umuhimu wa umoja katika sala, na hatua za ushirikiano, ili kushughulikia changamoto na mateso, yanayowapata Wakristo nchini Ethiopia na duniani kote.
Ziara ya Kardinali Gugerotti itaendelea nchini humo, na kwamba amepangwa kutembelea makanisa yote ya Eastern Rite nchini Ethiopia, ikiwa ni pamoja na Utawa wa Adigrat, Utawa wa Bahir Dar-Dessie, Utawa wa Emdeber, na Utawa wa Metropolitan wa Addis Ababa.

Rate this item
(0 votes)
Japhet