Na Angela Kibwana
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa mchango wa Sh milioni 100 kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa Kuu la Mt. Patrick jimboni Morogoro.
Mchango wa Rais Samia umewezesha kuezeka upya Kanisa hilo kongwe ambao ukarabati wa Kanisa hilo umefikia asilimia 98.
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Lazarus Msimbe (SDS) ametoa shukrani kwa Serikali na wadau mbalimbali kwa ushirikiano walioonesha tangu kuanza kwa shughuli za ukarabati wa Kanisa kuu la Mtakatifu Patris jimboni humo.
Mhashamu Askofu Msimbe ametoa pongezi hizo kwa mahojiano maalum na Tumaini Letu ofisini kwake akisema kuwa anawashukuru pia waamini wa Kanisa hilo walioshiriki kuchangia ukarabati wa Kanisa hilo huku akiwapongeza uongozi wa Halmashauri Walei kwa umoja na mshikamano wao.
Aidha Mhashamu Askofu Msimbe alisema kuwa baada ya hatua zote muhimu kukamilika kukarabati Kanisa hilo ikiwa ni pamoja hatua itakayofuata ni kutabaruku kutokana na kugusa sehemu mbalimbali za Kanisa hilo nje na ndani, maeneo matakatifu ya Kanisa hilo kuguswa wakati wa ukarabati huo.
“Napenda kutoa shukurani kwa Mwenyezi Mungu ambaye ametupa nguvu na kutuwezesha kimawazo, ni Mungu mwenyewe amefanya hii kazi kwa ajili ya nyumba yake. Nipende kutoa shukurani nyingi kwa ushirikiano tuliokuwa nao kwa Serikali katika suala zima la ukarabati wa Kanisa, niwashukuru viongozi na waamini wote walioshiriki kuchangia ukarabati huu,” alisema Askofu Msimbe.