Print this page

Mabaharia na harakati zao katika ustawi na maendeleo

Na Pd. Richard Mjigwa, C.PP.S

Jalai 12, kila mwaka, Mama Kanisa huadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, ikiwa ni Siku ya kumwomba, kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mungu kwa huduma yao.
Hakika ni mchango mkubwa, unaotolewa na mabaharia hao, pamoja na wavuvi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Kwa kawaida, hiyo ni siku maalumu ya kutambua mchango na sadaka ya watu hao, ambao wakati mwingine, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali, wanazokumbana nazo kila siku.
Utume wa Bahari, “Opus Apostolatus Maris”, unaojulikana na wengi kama “Stella Maris”, ulianzishwa tarehe 4 Oktoba 1920, na Waamini Walei wanaoshiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu, unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo.
Ni jukumu na wito wa Waamini Walei, kuutafuta Ufalme wa Mungu, unaosimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani; huku wakiyashughulikia mambo ya dunia, na kuyaelekeza kadiri ya mpango wa Mungu. 
Waamini Walei wanaitwa kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya Kiinjili, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo thabiti! 
Ili kuonesha na kushuhudia ukaribu wa Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, Papa Pio XI, tarehe 17 Aprili 1922, aliridhia kuanzishwa kwa Utume wa Bahari “Opus Apostolatus Maris.” Leo hii kuna jeshi kubwa la watu, wanaojisadaka zaidi kuwadumia mabaharia na wavuvi, katika bandari 300 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka. 
Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa, wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. 
Wadau wa Utume wa Bahari, wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji wa kina, kwa kuwafunulia watu wa Mungu, ile sura pendelevu ya Mama Kanisa, kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu watakatifu wa Mungu, na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa, ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. 
Takribani miaka 100 iliyopita, Dominika ya Utume wa Bahari, imekuwa ni kipindi muafaka cha ujenzi wa misingi ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na Mataifa mbalimbali duniani.
Papa Pio XI alitamani sana kuona kwamba, Utume wa Bahari unaendelezwa kwenye Bahari na fukwe mbalimbali za dunia. Roho Mtakatifu, kwa maombezi ya Bikira Maria, aendelee kupyaisha utume na huduma hii, mintarafu mahitaji ya ulimwengu mamboleo! 
Kuna mabaharia ambao dhamiri zao zinahangaika sana, na mara nyingi Mapadri wa maisha ya kiroho, kwa mabaharia na wavuvi, wamekuwa ni msaada mkubwa. 
Mabaharia ni watu wanaofanya kazi zao, katika mazingira magumu na hatarishi, mara nyingi nje ya nchi, makazi na familia zao! 
Mapadri washauri wa kiroho katika muktadha kama huu, wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini, kwa mabaharia na wavuvi waliopondeka na kuvunjika moyo! Mapadri wanapaswa kuwa ni watu wenye huruma, wapole na wanyenyekevu wanapowahudumia mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao.

Rate this item
(0 votes)
Japhet

Latest from Japhet