DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba-OSA, amesema kuwa vijana wanapopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, wanapokea ili watambue wajibu wao.
Askofu Musomba alisema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 60 katika Parokia ya Mtakatifu Paulo VI-Mikwambe, jijini Dar es Salaam.
Alitoa wito kwa Waamini wa Mikwembe kuepuka kiburi na majivuno, kwani tabia hizo zimetajwa kuwa ni vyanzo vinavyosababisha watu washindwe kumwelekea Mungu katika maisha yao.
Vile vile, alitoa msisitizo kwa Waamini kuepuka kuusaliti Ukatoliki wao kutokana na kudanganywa na waganga wa kienyeji wanaodai kwamba wanasafisha nyota.
Aliwasihi Wakristu kutenga muda maalum wa kuombea familia zao, kwani familia nyingi hukosa utulivu kutokana na kutokuwa karibu na Mungu katika maisha yao.
Askofu Musomba aliwakumbusha Waamini kutokufanya shughuli binafsi siku ya Jumapili zitakazowafanya washindwe kwenda kanisani, akiwataka kutambua kwamba Mungu ndiye anayewapa nguvu kila wakati.
Vile vile, aliwataka kuondoa vikwazo vinavyowafanya wawe mbali na Mungu, bali wajitahidi kuwa karibu naye ili waweze kuishi maisha yaliyo mema.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Gregory Kijanga alisema kuwa ni furaha kwao kutembelewa na Askofu Musomba, ambaye ni mara yake ya kwanza kufika parokiani hapo.
Padri huyo aliwasihi vijana walioimarishwa katika Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, kuyaishi yale waliyofundishwa, kwani hiyo itawasaidia kuiishi vyema imani yao.
Naye Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Stefano Shirima alimshukuru Askofu Msaidizi Musomba, akiwasisitiza wazazi na walezi kuwa karibu na vijana hao katika ukuaji wao, kwani wasipowasimamia vyema, wataharibika.