DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Dekano wa Dekania ya Mtakatifu Thomas More ambaye ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Kizito, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Romuald Mukandara amewaasa waamini kumtolea Mungu Sadaka safi.
Padri Mukandala alisema hayo hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Tokeo la Bwana, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Kizito-Kilongawima.
“Mnatakiwa kumtolea Mungu sadaka ya kupendeza na siyo kufanya maigizo, huku ukitazama zaidi kipato chako na kiasi unacho mtolea Mungu kama shukrani,”alisema Padri Mukandala.
Aidha,alisema mwaka huu ni mpya kila muamini anatakiwa kujitafakari mwenyewe wapi amejikwaa na kumkwaza Mungu, kwa mwaka uliyopita kwa matendo mbalimbali.
Padri Mukandara aliwasihi waamini kusahihisha makosa yao kwa kufuata anacho kihitaji Mungu, na kusema kama, mwizi, mchoyo, mkorofi, na kama hawajafunga ndoa Takatifu ama kutolipa Zaka wabadilike sasa.
Alisema kwamba Dekania na Parokia anayoiongonza anataka kila Mwanakwaya anayeimba mziki Mtakatifu kanisani kujitahidi kufunga ndoa hasa kwa wale wenye kuishi uchumba sugu.
Kwa mujibu wa Padri Mkandala wanakwaya wanatakiwa kuachana na maisha ya uchumba sugu, kwani wao ni vioo vya jamii.
Aidha, aliwataka waamini kutambua kwamba katika kuimba wanasali mara mbili, akiwasihi wapokee Sakramenti Takatifu.
Naye Padri Josephat Utouh, ambaye ni Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Cha Don Bosco_Jimbo Katoliki la Iringa, aliwataka waamini kuacha tabia za kukumbatia mambo yasiyofaa.
Hata alisema waamini hao wanatakiwa kuhakikisha wanaiishi Imani yao, Katoliki pasipo kutangatanga katika madhehebu mengine.
Padri Utouh aliendelea kusema waamini inawapasa kuwa na upendo kwa wanadamu akiwasihi kuachana na chuki.