Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliendelea kuwaletea historia ya Kanisa kuibuka kuwa Mlezi wa Elimu, Leo tunaendelea kuwaletea historia ya kuibuka kwa mashirika yalianzishwa kwa ajili ya kuimarisha moyo huo Mtakatifu wa kidini. Sasa endelea…
Wakartusiani:
Wakartusiani walikuwa aina ya wakaa pweke, kwa mfano wa Mtakatifu Antoni wa Jangwani, ila waliishi pamoja bila mawasiliano. Wamonaki hawa walisali pamoja na kufunga, bila kuongea au kuwa na mawasiliano na watu wengine wa nje.
Hawa walianzishwa na Mtakatifu Bruno mwaka 1084. Shirika hili lilikuwa thabiti kiasi kwamba mashirika mengine yalipolegea, lenyewe lilibaki imara bila kupakwa uchafu wa dunia. Palikuwa na msemo kwamba, hapajakuwa na ulazima wa kurekebisha shirika hili, kwa sababu halijateteleka kwa uozo (never reformed because never deformed).
Wengi wao walikufa mashahidi, wakati wa Waprotestanti kwa kukataa kuacha Utawa. Kwa kufuata mfano huo, yalianzishwa mashirika mengine kama Wasistesiani, walioimarishwa na Mtakatifu Bernardo wa Clairvaux mwaka 1090.