DAR ES SALAAM
Na Editha Mayemba
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, anatarajiwa kuadhimisha Misa Takatifu ya kutabaruku kanisa jipya la Parokia ya Mt. Vincent wa Paulo, Kibamba, Septemba 23 mwaka huu.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Katibu wa Parokia hiyo, Victor Rweyongeza, amesema kuwa Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 3:00 asubuhi, ikiwashirikisha Mapadri, Watawa, Waamini Walei na waalikwa kutoka Parokia jirani, na Jimbo kwa ujumla.
Amebainisha kuwa maandalizi kwa ujumla yamekamilika, ikiwemo kiroho na kimwili, yaani maungamo, semina na mafundisho kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya WAWATA, UWAKA,VIWAWA na Wanandoa, kwani siku hiyo kutakuwa na ndoa nyingi zitakazofungishwa.
Amekumbusha pia kuwa mwaka uliopita waliadhimisha Sakramenti ya Ndoa Takatifu kwa Wanandoa jozi 30, ikiwa ni maandalizi ya waamini hao kuingia katika Kanisa jipya wakiwa wametakatifuzwa.
Kuhusu ujenzi wa kanisa hilo la kisasa ulioanza mwaka 2013, Rweyongeza amesema kuwa wanafanya maandalizi ya mwisho, ikiwemo kupaka rangi ndani na nje, na kumalizia maeneo madogo madogo yaliyobaki.
Amewashukuru Waamini na watu wenye mapenzi mema kwa niaba ya Kamati Tendaji na Kamati ya Ujenzi kwa majitoleo yao na michango iliyowezesha kazi hiyo kukamilika kwa mafanikio makubwa na kwa wakati.