Dar es Salaam
Na Mathayo Kijazi
Mkurugenzi wa Utume wa Walei Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Vitalis James Kassembo amezindua kitenge cha Chama cha Kitume cha Wajane na Wagane, akiwataka kuutumia vema mradi huo katika kuendeleza utume kupitia chama chao.
Uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni katika ofisi ya Halmashauri ya Walei iliyopo katika viunga vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, jimboni humo.
Padri Kassembo aliwaasa wote watakaonunua kitenge hicho kuwa waaminifu, akisema kwamba anayechukua vitenge vya idadi fulani, arudishe fedha inayolingana na idadi ya vitenge hivyo.
“Mradi huu utusaidie pia kuendeleza utume. Lakini pia kama wanautume kuweza kujitawala vizuri sisi kama wanachama wa chama hiki. Maana yake tunaongea kuhusu uaminifu katika yale ambayo tutakuwa tumekabidhiwa, kama umekabidhiwa vitenge kumi, basi urudishe fedha ya vitenge kumi, usilete kona kona, kwa sababu ukileta kona kona, tunakwama wote,” alisema Padri Kassembo.
Aliwasisitiza kuutumia mradi huo kuwaunganisha na kuwafanya wawe wamoja zaidi, akiwaasa kutotengana kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kutokuwa waaminifu.