VATICAN CITY, Vatican
Baba Mtakatifu Fransisko amesema kuwa mateso na mahangaiko ya mwanadamu, ni zawadi ya matumaini na uaminifu wa Mungu katika Fumbo la Pasaka, na kwamba upendo wa Mungu daima utawaandama waja wake hata wakati wa majaribu na vikwazo katika maisha yao.
Papa alitoa ujumbe huo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Siku ya 33 ya Wagonjwa Duniani mwaka 2025, iliyoadhimishwa mjini Vatican, siku ambayo ilianzishwa Mei 13 mwaka 1992, na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes nchini Ufaransa, mnamo Februari 11 mwaka 1993.
Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa kwa ngazi ya kijimbo yaliyoadhimishwa mwaka huu wa 2025, yananogeshwa na kauli mbiu isemayo, “Na tumaini halitahayarishi, lakini hutuimarisha wakati wa majaribu,” huku Baba Mtakatifu akiwaalika watu wote wa Mungu kuwa Mahujaji wa Matumaini.