Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Dar es Salaam

Na Arone Mpanduka

Kuimba ni kutamka maneno katika hali ya kimuziki, au pia twaweza kusema ni kutamka maneno moja baada ya jingine kwa sauti yenye lahani (sauti ya ala ya muziki,tyuni) au ghani (melodi).
Mwimbaji ni mtu yeyote mwenye uwezo wa kuimba kwa sauti yake  bila kutumia vyombo vya muziki.
Ikumbukwe pia kuwa katika vikundi vya uimbaji, wapo wale wanaoongoza wengine katika uimbaji (lead singers), na wengine kazi yao ni kuitikia (backing singers).
Kuna mitindo mbalimbali ya uimbaji. Wengine wanaimba huku wamesimama wima, wengine wanaimba huku wamekaa, na wengine wanaimba huku wakionesha ishara mbalimbali kwa mikono, miguu yao,au vyote viwili.
Mitindo ya uimbaji ni mizuri iwapo tu inasaidia kufikisha ujumbe kwa wahusika. Huduma ya uimbaji siyo “show.”

JINSI YA KUPATA WIMBO/MADA MPYA
Watu wengi wanapenda vitu vipya,mathalan kiatu kipya, gauni jipya, nyumba mpya,vyombo vipya, n.k. Vivyo hivyo, watu wanapenda kusikia nyimbo mpya. Lakini je, ni rahisi kwaya au watunzi wa nyimbo kutunga nyimbo mpya kila mara?
Mambo yafuatayo yanaweza kukusaidia kupata nyimbo au mada mpya.Ukisikia sauti ya wimbo (melody) moyoni mwako, fanya haraka kuirekodi kwenye kanda (kama una radio cassette na microphone au simu).ili usisahau.
Njia nyingine ni kusoma sana vitabu mbalimbali vya kisiasa, kiuchumi na historia za ndani na nje ya nchi, ili vikupe uelewa mpana wa kuimba maudhui unayoyataka.
Pia, unaweza kuwa mdadisi wa mambo kwa kuuliza wajuzi mbalimbali, na kufuatilia vyombo vya habari kuhusiana na yale yanayoendelea kujitokeza kila siku.
Wimbo unaweza kuwa na mada (topic) moja au zaidi. Lakini wimbo wenye mada moja ni mzuri zaidi. Kwa nini?
Wimbo wenye mada moja mara nyingi unaanza kwa utangulizi,baadaye unaelezea mada yenyewe, na kisha unatoa hitimisho.Kwa hiyo ni rahisi kukumbuka ujumbe wa wimbo huo.
Pia, hakikisha unakuwa na ufafanuzi wa kutosha. Beti 3 au 4 zinaweza kuzungumzia mada moja tu kwa kuifafanua. Mada ya wimbo inaweza kumlenga mtu mmoja au watu kadhaa.
Nyimbo nyingi zinaangukia katika makundi mbalimbali, kama vile nyimbo za mafundisho/maonyo, Nyimbo za Faraja, Nyimbo za Mahubiri,
Nyimbo za siasa, nyimbo za uchumi na nyimbo za kuburudisha ambazo ndani yake zinaweza kukosa ujumbe sahihi, lakini zikaishia kuwa na midundo mizuri kwa lengo la kusherehesha.

VYAKULA NA VINYWAJI KWA MWIMBAJI
Vilaji na vinywaji visivyofaa kabla ya kuimba, ni muhimu ili kuepuka kuimba  tumbo likiwa tupu kabisa. Kuimba ni kama riadha, inahitajika nguvu kwa ajili ya utendaji wako. Hata hivyo, ni muhimu pia kuepuka kuimba tumbo likiwa limeshiba sana.
Kumbuka kuimba ni kazi ngumu, unahitaji mafuta (you need fuel), hivyo inashauriwa kuwa na mlo wa kawaida wa saa moja au mbili kabla ya uimbaji.
Kulingana na mazoea yetu, vipo vyakula na vinywaji ambavyo ni vigumu kuachana navyo ghafla, mengine huchukua muda.

VYA KUZINGATIA UWAPO STUDIO YA MUZIKI
Mosi; Usikimbilie kwenye chumba cha kurekodia kabla hujawa tayari. Kusimama studio ili kurekodi inaweza kuwa ya kukatisha tamaa kwa waimbaji wapya. Hivyo, fanya mazoezi sana kabla ya kurekodi.
Pili; Jaribu kujirekodi mwenyewe kabla ya kuingia studio, na sikiliza kujua kile ulichokipenda, na kusahihisha usichokipenda. Chagua funguo sahihi ili kuweza kufikia nota za juu kwa wepesi, mbinu zako za kiuimbaji zinatakiwa kuwa nzuri kiasi cha kuzuia kupoteza muda katika studio kwa kurekodi mara nyingi, na kutumia tyuni nyingi.
Tatu; tumia vizuri microphone katika kuimba. Katika studio hakikisha kunakuwa na umbali fulani kutoka mdomoni mwako hadi kwenye microphone. Waimbaji wenye uzoefu mdogo kwenye microphones hujikuta wakiyumbisha vichwa vyao, kitu ambacho kinaweza kuharibu ubora wa sauti.Sogea karibu na microphone sauti inapokuwa ndogo, na mbali inapokuwa kubwa. Hii itakusaidia kuondoa tofauti ya kupanda na kushuka kwa sauti.
Nne; Epuka kusisitiza maneno yenye P na B ambayo mara nyingi huzalisha sauti yenye popp. Pia weka msisitizo kwenye maneno yenye F na S.
Tano; Dhibiti sauti za pumzi (kuhema kwa sauti). Kudhibiti sauti za pumzi wakati wa kurekodi itasaidia kuondoa usumbufu wakati wa kuhariri sauti.
Sita; Kabla hujaanza kurekodi, jaribisha aina tofauti za microphone kuona ni ipi inayofaa. Unaweza kurekodi ubeti mara kadhaa, na kusikiliza ipi inayofaa.

LONDON, Uingereza
Hakuna muda ulio wazi wa kurejea kwa Andy Murray, baada ya nyota huyo aliyekuwa mchezaji nambari moja wa Uingereza kupasuka mishipa ya kifundo cha mguu mapema mwezi Machi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alipata jeraha katika kushindwa kwake kwenye michuano ya Miami Open, raundi ya tatu.
Murray atakosa mashindano ya Aprili ya Monte Carlo Masters, na BMW Open huko Munich, kufuatia mashauriano na wataalam wa matibabu.
Bingwa huyo mara tatu wa Grand Slam, hapo awali alisema hana mpango wa “kucheza zaidi msimu huu wa joto”.
Murray alicheza kukamilisha mechi dhidi ya Machac, kwa kupoteza 5-7 7-5 7-6 (7-5), kabla ya kufichua ukubwa wa jeraha siku ya Jumatatu.
Raia huyo wa Scotland alisema kuwa alipata mpasuko kamili wa ligament yake ya mbele ya talofibula, na karibu  kupasuka kwa unene wa kano yake ya calcaneofibular.
Murray, ambaye anatimiza umri wa miaka 37 mwezi wa Mei mwaka huu 2024, alisema mapema mwaka huu kwamba anataka kushindana katika Michezo mingine ya Olimpiki kabla ya kustaafu.

BURNLEY, Uingereza
Meneja wa klabu ya soka ya Burnley Vincent Kompany amelalamikia kiwango cha mwamuzi katika Ligi Kuu ya England msimu huu, akidai kuwa hakijakuwa kizuri vya kutosha.
Kompany alionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Darren England wakati wa sare ya 2-2 dhidi ya Chelsea Jumamosi kwa kupinga uamuzi wa penati uliosababisha beki Lorenz Assignon kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Wachezaji sita wa Burnley wametolewa nje kwa kadi nyekundu katika mechi 30 msimu huu, idadi kubwa zaidi kuliko ya timu yoyote ya Ligi Kuu England.
Assignon alionyeshwa kadi ya pili ya njano muda mfupi kabla ya kipindi cha mapumziko kwa kumchezea vibaya Mykhailo Mudryk, na Kompany alitolewa uwanjani kwa majibu yake.
Burnley walitoka nyuma mara mbili dhidi ya Chelsea, huku Dara O’Shea akifunga bao la kusawazisha dakika ya 81 na kupata pointi moja.
“Nimewaambia waamuzi nimesema kwa njia ya kujenga, kuelewa na ukweli sio rahisi kwao”, alisema Kompany.

Dar es Salaam

Na Nicolaus Kilowoko

Kocha Mkuu wa klabu ya soka ya Singida Fountain Gate FC, Jamhuri Kihwelo maarufu kama ‘Julio,’ amepinga madai ya wachezaji wake kushuka viwango, na kueleza kuwa wanaoendelea kuisema timu hiyo, hawako sahihi.
Julio aliyaeleza hayo wakati akifafanua hali ya kambi na maandalizi ya timu yao kwa ajili ya mechi zijazo ambazo zipo mbele yao, ikiwemo mechi muhimu ya Ligi dhidi ya timu ya soka ya Yanga.
Alisema kuwa watu hawaijui klabu hiyo hiyo kuwa kwa sasa imebadilika, tofauti na huko nyuma kabla ya yeye hajaichukua, na kudai kuwa timu ina wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kukupa matokeo chanya.
Julio alisema kuwa watu wamekuwa wakiisema vibaya klabu hiyo kuwa imelegalega, kitu ambacho siyo kweli kutokana na kuwa amekuwa na wachezaji wenye kujua nini wanafanya, tofauti na mitazamo ya watu wengine.
“Vijana wangu kwa sasa wanafanya mazoezi makubwa sana, hata ukiwaangalia, wanacheza kwa maelewano makubwa, na kwa asilimia 80 timu imebadilika sana kutokana na kuwa na wachezaji ambao wanajua nini wanachokifanya”, alisema Julio.
Alisema pia kuwa mbali na kuendelea kupambana nao katika mazoezi na kuwapa mbinu nyingi za kiufundi, lakini kitu kingine ambacho anendelea nacho kwa sasa ni kurekebisha ufahamu wao ili kuwajenga na kuwa bora kwa michezo yao ijayo.
Timu hiyo iliweka kambi Bamba Beach jijini Dar es salaam baada ya Ligi kusimama kwa muda, na hivyo kupelekea uongozi wa klabu hiyo wa kushirikiana na benchi la ufundi kwa ajili ya kuongeza kitu kwenye uchezaji wao.
Singida Foutain Gate wanatarajia kuwa na kibarua kizito Aprili 14 watakapokutana dhidi ya klabu ya soka ya Yanga katika mchezo wao wa Ligi mara baada ya kukutana na dhahama ya kipigi katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza wa Ligi.
Ikumbukwe hivi karibuni kwamba uongozi wa klabu hiyo ulifanya mabadiliko makubwa mara baada ya kuvunja benchi lote la ufundi la awali, na kumuajiri Kocha Jamhuri Kihwelo (Julio) ambapo lengo kuu ni kuinusuru timu hiyo isishuke daraja, bali kuleta sura mpya na mbinu mpya za kiufundi ili kufikia malengo yao ya msimu wa mwaka 2023/24.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Parokia Teule tatu za Mbweni Teta, Mbopo, na Nyakasangwe Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam zimepandishwa hadhi kuwa Parokia Kamili na kulifanya jimbo kufikisha Parokia162, kutoka 159.
Aidha, Vigango vitatu vya Nyantila, Yongwe, na Minazini, navyo vimepandishwa hadhi kuwa Parokia Teule.
Mabadiliko hayo yalitangazwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika Adhimisho la Misa takatifu ya kupadiri Mafuta Matakatifu iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, jijini Dar es Salaam.
Katika mabadiliko hayo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alimteua Padri Cosmas Kangwele kuwa Paroko wa Parokia mpya ya Mbweni Teta, Padri Joseph Luena kuwa Paroko wa Parokia mpya ya Mbopo, na Padri Joseph Nkusi kuwa Paroko wa Parokia mpya ya Nyakasangwe.
Aidha, Askofu Mkuu alimhamisha kituo cha kazi Padri John Bosco Mligo aliyekwua akihudumu Parokia ya Mbagala Zakhem, kwenda kufanya Utume Parokia ya Pande Msakuzi, kama Paroko Msaidizi.
Wengine ni Padri Thomas Njuwe aliyeteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mikoroshoni, na kumhamisha Padri Canisius Hall aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Mikoroshoni, kwenda kuwa Paroko Msaidizi Parokia ya Makongo Juu.
Askofu Ruwa’ichi pia alimteua Padri Israel Slaa anakwenda kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Don Bosco, Kibaha, mkoani Pwani.
Aenzi mpango wa Papa kutunza mazingira:
Katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya kubariki Mafuta Matakatifu, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitumia nafasi hiyo kuenzi mpango wa Baba Mtakatifu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti wa ‘Laudato Si’.
Akizungumzia mpango huo wa utunzaji wa mazingira kwa kuwakabidhi Madekano miche ya miti ili wakaioteshe kwenye Dekania zao, kwani kwa kufanya hivyo, mazingira yatakuwa bora.
‘Mapadri teteeni waamini ‘wasitekwe’
Awali katika homilia yake, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwasihi Mapadri kuwapatia Waamini mafundisho sahihi, ili wasirubuniwe na wababaishaji, hasa wanaojiita wapakwa mafuta.
“Naomba hapo mnivumilie kidogo niweke msisitizo, hizi ni zama zenye utata, hizi ni zama za wababaishaji. Wapo watu mbalimbali, wanajitokeza na kujitangaza kwamba wao ni wapakwa mafuta, kwa hiyo wanajipanga kugawia na kupaka watu mafuta. Naomba niseme kwa Wakristo wote, muwe macho na watu wa namna hiyo, maana wanawarubuni tu, hawana mafuta ya kuwapaka,”
Alibainisha kuwa licha ya kutoa mafundisho sahihi, pia Mapadri hao wanatakiwa kuhakikisha maisha yao inakuwa vielelezo bayana kwa Wakristo ili wafuate nyayo zao, wamjue, wamfuate na kumshuhudia kwa dhati Kristo.
Ataka Mapadri kuepa kuburuzwa:
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mapadri nao wanatakiwa kuepa kishawishi cha kuburuzwa na wababaishaji, akiwasihi kutambua kwamba wanapotoa kitu chochote cha baraka, kitolewe kwa msingi na uwelewa wa mafundisho sahihi.
Kwa mujibu wa Askofu Ruwa’ichi kitendo cha baadhi ya watu wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu, kuunga mstari kwenda kukomunika wakati wao si Wakristo, ni cha kusikitisha.
Akumbusha matumizi ya Mafuta:
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mafuta ya Krisma kwa uelewa sahihi wa Kikatoliki, yanatumika katika Sakramenti ya Kipaimara na katika Sakramenti ya Daraja Takatifu, akionya kwamba hayo si mafuta yanayowekwa kiholela, bali hutumika kwa malengo sahihi na kwa uelewa sahihi.
Aliwashukuru Mapadri wote wa Jimbo hilo walioshiriki katika Adhimisho la Misa Takatifu, akisema kwamba kuwepo kwao kunadhihirisha ushirikiano wao na Askofu katika kulihudumia, kuliongoza na kulitakatifuza Kanisa la Mungu.
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Stephano Musomba, alisema kuwa Mei 16 mwaka huu, ni Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, hivyo akizitaka Parokia zote kuwasilisha michango yao ifikapo Aprili 30 mwaka huu, ili mipango ifanyike mapema.
Hata hivyo, alisema kwamba kutakuwa na Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa ambalo litafanyika katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ambalo safari hii ni mwenyeji.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Waoblate watawa wa tatu wa Shirika la Mtakatifu Benedikto, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wametakiwa kuendelea kushiriki Sala, mambo ya kiroho na kijamii katika maisha yao ya kila siku ya Utume wao.
Wito huo ulitolewa na Padri Baltazar Minde, Dekano wa Dekania ya Pugu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kuwapokea Waoblate wapya wanane na wengine wanane kuweka Ahadi zao za Daima katika Utume huo wa Tatu, ilioadhimishwa katika Parokia ya Pugu, jijini Dar es Salaam.
“Naombeni sana katika maisha yenu haya ambayo mmeamua kujitoa wenyewe ninyi kama watu wa katika familia, basi mhakikishe mnaishi zile nia za Sala,”alisema Padri Minde.
Padri Minde alisema kuwa Waoblate waamini walio kwenye familia na kwenye ndoa ambao wameamua kujitoa maisha yao kwa ajili ya kufanya majitoleo ya sala, kazi na kujifunza zaidi mambo ya kiroho.
Alisema kuwa kila Mkristo anaweza kuomba kujiunga na Utawa huo wa Tatu katika maisha yake ili aweze kupokelewa katika Utawa huo wa Mtakatifu Benedikto.
Kwa mujibu wa Padri Minde, maana ya Waoblate ni kujitolea kwani kwa namna ya pekee ni kama sadaka ya pekee, hasa kwa wanafamilia hao katika maisha yao ya kawaida kuamua kujitoa kuingia utume huo.
Alibainisha kwamba kwa njia hiyo Waoblate wanajiimarisha zaidi katika imani na maisha yao ya kiroho kwa njia ya Sala na mafunzo mbalimbali ya kiroho kupitia maisha yao ya Oblate.
Naye Mwenyekiti wa Watawa wa Tatu wa Shirika la Mtakatifu Benedikto Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,Teodas Mbiro, amewataka waamini wenye nia ya kujiunga katika utume huo, wafuate utaratibu kwa kupatiwa kwa mafundisho ya mwaka mmoja na watapokelewa rasmi.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Tumaini Televisheni nchini Tanzania kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Italia (Conference Episcopal of Italia: CEI), imezindua rasmi mpango maalumu wa Utunzaji Mazingira kwa kupanda miti katika Dekania, Parokia, na sehemu mbalimbali kote nchini ikiwa ni kuunga mkono Utekelezaji wa Tamko la Baba Mtakatifu Fransisko kuhusu Mazingira, ‘Laudato Si’.
Uzinduzi huo ulifanywa Machi 26 mwaka huu na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kubariki Mafuta Matakatifu, iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, jimboni humo.
Baada ya uzinduzi huo, Askofu Ruwa’ichi alikabidhi miche ya miti kwa Madekano wa Dekania zote 15 za Jimbo hilo, ili kwenda kuipanda miti hiyo katika Dekania zao na Parokia, akiwataka Madekano hao kwenda kuhamasisha utekelezaji wa mpango huo wa kutunza mazingira kwa Waamini wao.
Akizungumzia mpango huo wa kutunza mazingira, Mkurugenzi wa Tumaini Media yenye vyombo vyake Tumaini Televisheni, gazeti Tumaini Letu, na Redio Tumaini, Padri Joseph Massenge alisema kwamba zoezi la kupanda miti ni endelevu linalotekelezwa Nchi nzima.
“Yaani kazi hii haina mwisho, ni mpaka mwisho wa dunia kwa lengo la kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa kupanda miti katika Majimbo Katoliki yote nchini Tanzania,” alisema Padri Massenge.
Mkurugenzi huyo wa Tumaini Media alisema kuwa mpango huo unaendana na utoaji wa elimu kwa vijana na Waamini kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira Nchi nzima.
Padri Massenge aliyataja Majimbo Katoliki Makuu ambapo mradi wa kutunza mazingira kwa kupanda miti, unaendelea kutekelezwa, kuwa ni Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, Mbeya, Tabora, na Jimbo Kuu Katoliki la Songea.
Kwa mujibu wa Padri Massenge, kazi ya upandaji miti ltasaidia kwa kiasi kikubwa kunusuru uharibifu wa mazingira nchini, unaotokana na ukataji miti ovyo.
Julai 13 mwaka 2022, Baba Mtakatifu Fransisko alitoa Waraka wake wa Kichungaji wa ‘Laudato Si,’ yaani ‘Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote’ unagusia kuhusu mazingira; Injili ya Kazi ya Uumbaji na Amani; Vyanzo vya mgogoro wa Ikolojia na watu; Ikolojia ya mazingira, uchumi na jamii.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa Parokia ya Mtakatifu Thomas wa Akwino – Kipunguni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yusuph Mkindi ameuomba Uongozi wa Serikali ya Mtaa kuwatengenezea barabara inayotoka Moshi Bar, kuelekea parokiani hapo, kutokana na kuwa kero, hasa kipindi cha mvua.
Mkindi alitoa ombi hilo wakati akizungumza na Tumaini Letu, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Matawi iliyoadhimishwa hivi karibuni parokiani hapo.
“Sisi katika Mitaa yetu tuna Viongozi ambao wanaliona hili, na tumeshawaambia, lakini siyo kuwaambia tu, hata wao wenyewe wanaona pia…
“Kwa hiyo, tunaiomba Serikali ya Mkoa, na hata kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, tumwombe pamoja na uongozi wote watuangalie katika barabara hii, kwa sababu Waamini wanashindwa kufika kanisani, hasa mvua kubwa kama hizi za masika zinapoanza,” alisema Mwenyekiti huyo.
Mkindi aliwapongeza Waamini wenzake kwa upendo, umoja na ushirikiano wanaoendelea nao parokiani hapo, hasa katika shughuli mbalimbali za Kanisa.
Aidha, aliwasihi kuendelea kujitolea kwa moyo katika kulijenga Kanisa, huku akiwaasa pia kujitolea kwa moyo kuwasaidia wahiji, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresma.
“Tuwaone wahitaji kwamba ni sehemu yetu sisi, kwa hiyo tuwatumikie, tuwape kile ambacho kinawafaa, kwani tukifanya hivyo, Mungu wetu anazidi kutubariki,” alisema Mkindi.
Awali katika homilia yake wakati wa Adhimisho hilo la Misa Takatifu, Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, Padri Nestory Damas, alisema kuwa mtu anayemshikilia Kristo, maisha yake yanakuwa ya thamani, bali anayejitenga na kuamua kumuacha Kristo, thamani yake inashuka na kupotea.
“Kumbe wapendwa, tunapomtafakari mwanapunda, na sisi twaweza kujifananisha kama mwanapunda. Unapokuwa na Yesu, unapokuwa na Kristo katika maisha yako, unakuwa ni mtu wa thamani, unakuwa ni mtu wa kipekee….
“Lakini pale ambapo unamuacha Kristo, basi thamani yako inashuka, thamani yako inapotea, na hasa pale ambapo tunamuacha tunafuata njia ambazo zinaelekeza kwenye giza, njia ambazo zinaelekeza kwenye upotovu. Kumbe leo tunatafakari kadri ambavyo tumesikiliza historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, tujiulize swali moja ambalo litakuwa ni la tafakari yetu ya siku ya leo, ni nani alimuua Yesu?” alisema Padri huyo.
Aliwataka Waamini kuendelea kuyakabidhi maisha yao mikononi mwa Mungu, kwani ni yeye pekee ndiye mwenye maamuzi juu ya maisha yao.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa Kanisa halijiingizi katika siasa, bali lina wajibu wa kushauri inapohitajika, ili siasa hiyo iwasaidie watu katika maisha yao.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mlezi na Mshauri wa Wanataaluma Wakristo Tanzania (Christian Professionals of Tanzania: CPT), Padri Vic Missiaen, wakati akizungumza katika Mafungo ya wanachama wa CPT yaliyofanyika Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili - Mavurunza, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Kwa hiyo sisi kama Kanisa, hatuna kazi ya kuingia katika siasa, bali tu tuna wajibu wa kushauri ili siasa hiyo iweze kufanya kazi ya kuwasaidia watu,” alisema Padri Vic Missiaen.
Padri Missiaen alisema kwamba kujenga Kanisa, kulikuja kwa lengo la kuwasaidia na kuwainua watu katika maisha yao ya kiroho.
“Lengo la kujenga Kanisa Mahalia au Local Church, kulikuja kwa lengo la kusaidia na kuwainua watu katika maisha yao ya kiroho,” alisema Padri Missiaen.
Padri Missiaen alibainisha kuwa licha ya watu wengi wanalipenda Kanisa, lakini ni wachache ndio wenye  msimamo wa kiroho tu katika maisha yao.
Aliwasihi wanachama wa CPT kutambua kwamba wao kama wasomi, ipo haja ya kutumia usomi wao kupeleka mbele mawazo yao ili kusambaza mafundisho ya kiroho kwa jamii.
“Naamini wanaCPT tuna uwezo wa kufanya hivyo, na tuna wajibu. Tukijijengea uwezo imara, tutaweza kusambaza vyema mafundisho hayo,” alisema Padri huyo.
Vile vile, aliwasisitiza kujitafakari na kuamua kusema ukweli mbele za Mungu pale wanapokosea, kwani wengi wao hawako tayari kueleza ukweli.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Mavurunza, ambaye pia ni mwanachama wa CPT, Casmir Nkumba aliwashukuru wote walioweza kushiriki katika mafungo hayo yaliyofanyika katika Parokia yao, akisema kwamba Parokia hiyo imejifunza mengi juu ya mafunzo yaliyotolewa.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amekemea vitendo vya unyanyasaji wa watoto vinavyoendelea kufanyika nchini, akiwataka Waamini wenye tabia hiyo kuacha mara moja.
Aidha, Kardinali Pengo aliwasihi waamini kujitafakari na kuamua kumchagua Kristo, kwani ndiye muweza wa yote.
Kardinali Pengo alitoa rai hiyo katika homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya Matawi iliyoadhimishwa hivi karibuni katika Parokia ya Mtakatifu Polycarp Askofu na Shahidi – Kilamba, jijini Dar es Salaam.
“Muwe tayari kuutangaza ukweli na kuwa katika upande wa haki siku zote. Simameni katika upande wa Yesu Kristp, kwa sababu kusimama upande wa Yesu, kunasaidia hata katika kuziimarisha Jumuiya zenu,” alisema Kardinali Pengo na kuongeza,
“…Kwa hiyo ndugu zangu msijisahau mkaamua kumtupa Kristo. Mnatakiwa kujitafakari na kuamua kumchagua Kristo katika maisha yenu yote. Kila mnachokifanya katika maisha yenu, hakikisheni kwamba mnamuweka Kristo mbele.”
Aidha, Kardinali aliwapongeza Wanakilamba kwa hatua mbalimbali walizopiga katika Parokia hiyo, huku akiwaombea kwa Mungu ili waweze kukamilisha kila mpango ulioko mbele yao parokiani hapo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo ya Kilamba, Padri Timoth Nyasulu Maganga alisema kuwa kabla ya hapo walikuwa na shauku kubwa ya kumwona Kardinali Pengo kufika parokiani hapo kwa ajili ya kuadhimisha Misa hiyo Takatifu ya Dominika ya Matawi.
Padri Nyasulu aliendelea kumwomba Kardinali Pengo watakapomwomba tena akaadhimishe Misa Takatifu katika Parokia hiyo, akubali, kwani bado wanamhitaji.
Padri Nyasulu alivishukuru vyombo vya habari ikiwemo Tumaini Media, kwa kuchukua habari juu ya Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Dominika ya Matawi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo, Herman Lyoba alimshukuru Kardinali Pengo, akisema kwamba kila anapowatembelea kwa ziara kama hiyo ya kitume, wamepiga hatua katika ujenzi wa nyumba ya Mapadri.