Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewataka Waamini kuuishi Ukristo wao, huku wakilishika Neno la Mungu.
Kardinali aliyasema hayo hivi kalibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa Vijana 112 katika Parokia Teule ya Mtakatifu Stephano wa Hungaria – Makurunge, jimboni humo.
“Sakramenti hii ya Kipaimara ni muhimu sana kwa Mkristo kuipokea, kwa sababu inakupatia uwezo mkubwa wa kumtangaza Kristo mahali,popote pale bila hofu. Pia, inakupatia nguzo kubwa ya kuwa askari hodari wa imani ya Kristo,” alisema Kardinali.
Alisema pia kuwa Waamini wengi hawasikilizi sauti ya Kristo, na hawafuati maneno yake, akiwasisitiza kuepuka kupotoshwa kwa maneno ya uongo, bali wafahamu kwamba sauti ya Mungu ndiyo inatakiwa kufuatwa.
“Sijui wamepotoshwa na kitu gani kibaya, bali utakuta wanafuata sauti za watu waongo ambao hawawezi kuwafikisha safari ya kuelekea kwa Baba Mungu. Ndugu zangu Waamini, nawaomba sana fuateni sauti ya Kristo, ambayo itawasaidia katika safari yenu ya kumtangaza Yesu Kristo ili baadaye muwe watu wema machoni mwake.
“Pia, tutambue kwamba Mungu ametuambia tusikilize sauti ya mwanaye. Huyu ndiye mwanangu niliyependezwa, naye msikieni, Mungu alikuwa na maana kubwa sana kutamka maneno haya. Tuwe watu wa kupendana, kuheshimiana, na kusaidiana kila wakati,” alisema Kardinali.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Watakatifu Wote – Kiluvya, Padri Danipaso Bitegeko, ambaye pia ni Msimamizi wa Parokia hiyo Teule, alimshukuru Kardinali Pengo kwa kufika parokiani hapo, na kuwapatia Vijana Sakramenti hiyo ya Kipaimara.
Naye, Mwenyekiti wa Parokia Teule, Gabriel Mwalo alisema kuwa kwa sasa wapo katika ujenzi wa nyumba mpya ya Mapadri, ili Padri aweze kukaa hapo hapo, kwani kwa sasa Waamini wanazidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo wanahitaji huduma ya kiroho kwa karibu.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ametoa wito kwa Vijana wanaopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, kumweka Mungu maanani siku zote za maisha yao.
Kardinali aliyasema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyoambatana na Sakramenti hiyo katika Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu Mtume – Kijitonyama, jimboni humo.
“Wanakipaimara tambueni kwamba katika maisha yenu ni lazima mumuweke Mungu Mwenyezi maanani. Na ndilo Neno lililotukusanya leo hapa, mlipotualika tuje kuadhimisha, kushuhudia adhimisho lenu la Sakramenti ya Kipaimara, ni ninyi mmetualika. Huwa hamumwoni Askofu anakuja hapa kanisani, lakini ni kwa sababu yenu ninyi mnaopokea Sakramenti ya Kipaimara, mimi niko hapa…
“… na hawa wote waliopo hadi Wanakwaya, huwa wanakuwepo sawa, lakini kwa leo ni kwa sababu yenu kuonyesha kwamba tunaweka maanani tendo mnalolifanya siku hii ya leo. Ni tendo kubwa lenye manufaa, siyo kwenu tu, ni tendo kubwa ambalo mnalifanya kwa niaba ya Kanisa zima. Kwa hiyo tunawaombea kwa Mungu Mwenyezi atekeleze maombi yanayokuwa ndani ya moyo wa kila mmoja wenu,” alisema Kardinali Pengo.
Aliongeza kwamba hakuna mwanadamu anayeweza kufanya kitu na kufanikiwa bila kumtanguliza Mungu, akisisitiza kuwa kila mmoja ahakikishe anamtanguliza Mungu katika mipango yake.
Sambamba na hayo, Kardinali alitoa mfano wa watu waliotaka kujenga mnara mrefu ili wakamwone Mungu mbinguni, na kwamba Mungu hakuona wivu juu ya maamuzi hayo, bali lengo ni kuwaonyesha kuwa hakuna kitu kinachofanywa na mwanadamu bila kumweka Mungu maanani.
“Waliotaka kujenga mnara ili uwe kumbukumbu yao hata kama hawapo, Mungu Mwenyezi alipogundua kwamba hawa watu wanataka kujenga kitu cha namna hii, akaamua kuwachanganya kwa lugha, hawakuweza kuelewana tena; mmoja akitumwa na mwenzake lete jiwe, yeye analeta maji; naomba mchanga, yeye analeta maji, kwa hiyo hawakuweza kuendelea kwa sababu hawaelewani tena…
“Si kwamba Mungu Mwenyezi aliwaonea wivu kwamba watafanya kitu kikubwa hivyo, lakini Mwenyezi alitaka kumwonyesha mwanadamu kwamba ‘ukitaka kufanya kitu chochote bila kuniweka mimi Mungu maanani, haiwezekani, hutafanikiwa,” alisema Kardinali Pengo.
Vile vile, alitoa wito kwa Vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara katika Adhimisho hilo, pengine wana mipango mikubwa iliyopo katika maisha yao, bali watambue kwamba hawataweza kufanikiwa bila kumweka Mungu mbele.
Aliwasisitiza kufahamu kuwa hakuna anayeweza kuwazuia kupanga mipango, hasa ya kimaendeleo maishani mwao, bali wakumbuke kwamba bila kumweka Mungu maanani, hakuna kitakachofanikiwa.
Wakati huo huo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwakumbusha Vijana hao kuendelea kuishi maisha yanayompendeza Mungu, kwani hayo ndiyo yatakayowasaidia kupokea baraka katika kila wanaloliomba kwake.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba mwaka huu, na kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), Aretas Lyimo, alisema  kuwa mpaka sasa watuhumiwa 58 wamekamatwa kwenye operesheni hiyo.
“Katika dawa za kulevya tulizozikamata, ni pamoja na mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, na tumeweza kuteketeza jumla ya ekari 157.4 za mashamba ya bangi, na lita 19,804 za kemikali bashirifu,”alisema Kamishna Lyimo
Aidha alisema kuwa kati ya dawa hizo, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja (01) ya hashishi, zilikamatwa katika eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.
Alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa skanka ni wanawake, ambao hudai kutumia dawa hizo kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha.
“Skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inayosababisha madhara makubwa kiafya. Vile vile, hashishi ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka. Mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa, na magonjwa haya wamerogwa,”alisema Lyimo.
Adiha, alisema kwamba katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Mamlaka ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein, zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi, pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.
“Dawa hizi ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka, ili kuepuka kubainika. Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, Hali hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya, na kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya,”alisema Kamishna Lyimo.
Kamishna Lyimo alisema kuwa mkoani Dodoma, Mamlaka imewakamata watuhumiwa wawili Suleiman Mbaruku Suleiman (maarufu Nyanda), mwenye umri wa miaka 52, na Kimwaga Msobi Lazaro (miaka 37) wakazi wa mtaa wa Kinyali, Kata ya Viwandani.
“Watuhumiwa hao walikamatwa na jumla ya gramu 393 za heroin. Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo, na amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu,”alisema.
Kupitia operesheni za kanda, DCEA pia imekamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin, na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaomba wananchi waendelee kuunga mkono jitihada hizi kwa kufichua wafanyabiashara wa dawa za kulevya, na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini makubaliano na taasisi ya Henan Polytechnic Institute, kutoka Nanyang, China, ili kushirikiana kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika nyanja za kilimo na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, (TEHAMA).
Makubaliano hayo yamesainiwa, ambapo katika makubaliano hayo VETA Kihonda kitanufaika katika nyanja ya kilimo na Chuo cha VETA Kipawa, kitanufaika katika sekta ya TEHAMA.
Aidha, waalimu na wanafunzi kutoka vyuo vya VETA Kihonda na Kipawa watajengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo katika maeneo ya Kilimo na TEHAMA, ili kuboresha elimu na mafunzo ya ufundi stadi na kuhakikisha wanazalisha wahitimu bora wenye kukidhi ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya Tanzania.
Katika mpango huo, waalimu na wanafunzi kutoka pande zote mbili, watapata fursa za kutembeleana na kubadilishana uzoefu baina yao, ili kuhakikisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanatolewa katika ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, ameishukukuru taasisi ya Henan Polytechnic kutoka China kwa kuona VETA ndiyo sehemu sahihi ya kuleta teknolojia mpya katika masuala ya kilimo na TEHAMA.
CPA. Kasore alisema kupitia makubaliano hayo, VETA inatarajia kunufaika kwa kiasi kikubwa, hasa katika kupata utaalam mpya ambao utawezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi bora na yenye viwango vya kimataifa ambayo yatakidhi ushindani katika soko la ajira.
“Ninaamini, kwamba kupitia ushirikiano huu, ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha vijana wa kitanzania wanapata elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujikwamua kimaisha inaenda kutimia, naomba ushirikiano huu uwe chachu katika kuzalisha vijana ambao wataweza kushindana katika soko la ajira kimataifa katika kujenga uchumi wao na taifa la Tanzania,” alisema CPA. Kasore.

MOSHI

Na Mathayo Kijazi

Wakristo wametakiwa kuwa wanyenyekevu na wenye hekima katika maisha yao, kwani hiyo itawasaidia kuishi maisha yanayompendeza Mungu.
Hayo yalisemwa na Padri Festo Tingo wakati wa homilia yake katika Misa Takatifu ya kumwombea marehemu Mzee Michael Lesio Kissoka, baba mzazi wa Padri Bonaventura Kissoka AJ, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mtakatifu Anna – Kirima, Jimbo Katoliki la Moshi.
Padri Tingo aliwasihi Waamini walioshiriki katika Adhimisho hilo, kuiga mfano wa maisha ya Mzee Kissoka, yakiwemo ya unyenyekevu na kuwajibika, kwani ni katika jitihada tu ndipo wanafanikiwa.
“Ukimya ni jambo lenye tafsiri nyingi katika maisha ya binadamu, ambapo pia ndani yake ukimya huashiria busara. Mzee Kissoka alikuwa mkimya, mnyenyekevu, mwenye busara, na mwenye kupenda kusali. Kwa hiyo ndugu zangu, ni vema kila mmoja akatumia muda wake vizuri kufanya matendo yaliyo mema, kwa sababu kwa kufanya hivyo, mtakuwa mmeitengeneza njia ya kwenda mbinguni,” alisema Padri Tingo.
Alisema pia kwamba hata kama Mzee huyo amefariki, bali watoto pamoja na ndugu kwa ujumla, wasiache kwenda kusalimia, kwani Kirima bado ina watu wanaostahili kwenda kusalimiwa.
“Usiseme kwamba siendi tena Kirima kusalimia kwa sababu mzee wangu hayupo, hapana. Endelea kuja kusalimia kwa sababu Wanakirima wapo, na Kirima ipo,” alisema Padri huyo.
Kwa upande wake Padri Bonaventura Kissoka aliwashukuru Mapadri wenzake, Waamini kutoka Majimbo mbalimbali, pamoja na watu wengine kwa kushiriki na kuwafariji katika msiba huo.
Padri Kissoka alisema kuwa wao kama familia, wanamshukuru Mungu kwa maisha ya baba yao kwa kuwalea katika misingi iliyo bora, ikiwa ni pamoja na kuwasomesha.
Akisoma wasifu wa marehemu, Michael Kissoka ambaye ni mjukuu wa Mzee Michael Lesio Kissoka, alisema Mzee huyo alizaliwa Septemba 26 mwaka 1926, Kibosho - Kirima Kati, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Alipata elimu ya watu wazima mwaka 1954, pamoja na elimu ya ufundi seremala na udereva.
Aliongeza kuwa Mzee huyo aliwafundisha kusali, kwani alipenda kusali kabla ya kufanya chochote, desturi ambayo aliipata kwa Masista, ambapo kwa kuishi hivyo, alijenga familia ya maisha ya sala, jambo lililomfanya kuwahimiza watoto wake kuwa na desturi ya kusali kila mara.
Kuhusu ugonjwa, mjukuu huyo alisema kwamba babu yake hakuwahi kusumbuliwa na ugonjwa wowote katika utu uzima wake hadi mwaka 2015, ambapo alikabiliwa na tatizo la koo na kuanza matibabu katika hospitali ya KCMC iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, na baadaye kupata matibabu zaidi katika hospitali ya OCEAN ROAD, Dar es Salaam baada ya kugundulika kuwa na saratani ya koo.
Aliendelea kusema kuwa mwezi Juni mwaka 2015, alipatiwa matibabu katika mji wa Ahmedabad nchini India, na baadaye aliendelea na matibabu katika klinik ya BESTA iliyopo Kinondoni Dar es Salaam, ambapo baada ya vipimo, alionekana kupona ugonjwa huo, na hivyo kuendelea na maisha yake kama kawaida.
Marehemu Mzee Michael Lesio Kissoka aliyefariki dunia Jumamosi Novemba 2 mwaka 2024 siku ya kuwakumbuka na kuwaombea Waamini Marehemu Wote; ameacha watoto.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, amewaasa vijana watambue kuwa wao ni Taifa la leo na si taifa la kesho, akiwasihi kuwa na uchungu na taifa lao.
Padri Kitima alisema hayo hivi karibuni katika Kongamano la Vijana lililofanyika katika Chuo cha ufundi Don Bosco, Oysterbay, Jijini Dar es salaam.
“Unatakiwa kuwa na uchungu na taifa lako kwa kuitambua vyema nchi yako ya Tanzania pamoja na ‘focus’ yaani nchi inapolenga kwa ajili ya maendeleo ya uchumi huku ukifahamu malengo ya viongozi”. Alisema
Alikumbusha kipindi cha nyuma ambapo kulikuwa na sera kama Tanzania ya viwanda au Kilimo kwanza lakini cha ajabu kwa sasa hakuna focus yeyote ya nchi ambayo itasaidia katika maendeleo.
Hata hivyo Padri Kitima alisema kuwa unapojengewa ‘physical skills’ unapewa mbinu ya kujitambua kama Mtanzania ni vyema kutumia maarifa ili uweze kufikia malengo ya nchi.
Mbali na hayo alizungumzia‘Development plan’ ya Hayati Rais Benjamin Mkapa iliyolenga kwa kila mtu kujitegemea, Mkapa aliwekeza katika kuanzisha taasisi zilizoweza kumuongoza katika sheria kama Tanroads, Takukuru, Tanzania Revenue Authority na zingine nyingi ambazo aliweza kusaidiana nazo katika kuingoza nchi”.
Vilevile Padri Kitima alisema nchi yetu imelenga kwa vijana ili kutoa taarifa zilizo sahihi kwa kuwasimulia matukio ya nyuma kwani 1884-1885 kulitokea na tukio kubwa ambalo lilibadili siasa zote za Tanzania ambalo ni Mkutano wa Berlin ambao uliligawa bara la Afrika na kuunganishwa na makoloni mengine ya ujerumani na kuanza kutumia siasa ya pamoja.
Hata hivyo alieleza kuwa hapo ndipo ushirikiano wa makabila ulianza kwani waliwekwa pamoja na kuanza kazi kwa umoja japo wajerumani walikuwa na lengo la kuwanyonya waafrika.
Padri Kitima alisema Tanzania ina wawekezaji wengi wa nje kuliko wa ndani lakini India wawekezaji wao wengi ni wahindi ambao wanasaidia mapato yao yasiende mbali bali yazunguke ndani ya taifa lao kutokana na wawekezaji wao.
Pia aliwataka vijana watambue kuwa Marekani matajiri wazawa ndiyo wanao ikopesha serikali na kusema inasikitisha kwa Tanzania hakuna hata Mzawa mmoja anayeimiliki hoteli kubwa kwani waliokuwa wakimiliki kipindi cha nyuma wamezibinafsisha kwa sera ya kusema hawawezi kuziendesha.
Padri Kitima aliwataka vijana kuwa na malengo na jambo Fulani kwa kuiga mfano wa Rais Obama wa kutamani kuongoza Marekani na lengo lake kutimia hivyo basi aliwaasa vijana kuwa na ndoto ya siku moja kuja kuondoa mfumo wa chama kimoja bungeni na kuruhusu vyama vingi.
Aliendelea kusema aliyepita kwa wizi wa kura hawezi kuwatetea wananchi wake, na kuwataka vijana kukataa dhambi ya kuchukua pesa kwa ajili ya kutangaza majibu ya uwongo wakati wa uchaguzi.
Aliwataka vijana kutoruhusu nchi ya vyama vingi kutawaliwa na chama kimoja kwa kusema kitashika serikali na bunge hata mahakama itashindwa kufanya kazi yake kwa haki.
Padri Kitima alisema vijana wanawajibika kuamka sasa kabla hawajaingia maofisini na baadaye kuanza kulia machozi wakati watu hao wameanza majukumu.
Alitoa wito kwa vijana kuchagua kiongozi muwazi na muwajibikaji ili aweze kutekeleza wajibu kwa haki.

ADDIS ABABA, Ethiopia

Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padri Tesfaye Tadesse Gebresilasie, ambaye alikuwa Mkuu wa Wamisionari wa Comboni wa Moyo wa Yesu (MCCJ), kuwa Askofu Msaidizi wa Archeparchy ya Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Monsinyo Tesfaye (pichani) ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Wamisionari wa Comboni nchini Ethiopia, kuanzia 2005 hadi 2009, alikuwa Rais wa Muungano wa Wakuu katika nchi hiyo kwa mihula miwili.
Mwaka 2015 alichaguliwa kuwa Mkuu wa kwanza wa Afrika na kuchaguliwa tena katika nafasi hiyo hiyo wakati wa Sura ya Jumla ya 19 ya Taasisi mwaka 2022.
Baba Mtakatifu Fransisko pia alimteua Askofu Mteule wa Jimbo Kuu Katoliki la Cleopatris, Alexandria, Misri, na atafanya kazi na Mwadhama Berhaneyesus Demerew Kardinali Souraphiel, mjumbe wa Usharika wa Umisionari (CM) na Shirika la Kawaida la Mitaa huko Metropolitan See.
Wakati wa Mkutano wa Sinodi uliomalizika hivi karibuni huko Roma kiongozi huyo mzaliwa wa Ethiopia, Tesfaye alikuwa mjumbe kutoka Chama cha Mabaraza ya Maaskofu Wanachama katika eneo la Afrika Mashariki (AMECEA), ambaye aliwakilisha Daraja za Kidini.
Tesfaye alizaliwa katika Jiji la Harar, nchini Ethiopia Septemba 22 mwaka 1969, alijiunga na Wamisionari wa Comboni mwaka 1986, na kutawazwa kuwa Padri Agosti 26 mwaka 1995, mjini Addis Ababa.
Alitunukiwa leseni ya Masomo ya Kiarabu na Kiislamu kutoka Taasisi ya Kipapa ya Masomo ya Kiarabu na Kiislamu huko Roma na Shahada ya Kwanza ya Sanaa ya Theolojia Takatifu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, Roma, na Stashahada ya masomo ya Kiislamu kutoka Taasisi ya Kipapa ya Kiarabu na Masomo ya Kiislamu mjini Roma.
Aliendelea na masomo yake ya Kiislamu katika Dar Comboni kwa Masomo ya Kiarabu huko Cairo na alihudhuria kozi ya malezi katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesian cha Roma.
Askofu Mteule huyo alihudumu katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Naibu Paroko na Mkurugenzi wa Shule ya Comboni huko Haro Wato mwaka 2001, Mshauri wa Jimbo la Wamisionari wa Combini nchini Ethiopia (2002-2004), Mkoa wa Wamisionari wa Comboni nchini Ethiopia, na Rais wa Mkutano wa Wasimamizi Wakuu wa Kidini wa Ethiopia (2005), na Jenerali Mkuu wa Wamisionari wa Comboni (2015 na 2022).

NAIROBI, Kenya

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanachama wa Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki (AMECEA), Padri Anthony Makunde amesisitiza kuwepo kwa mambo muhimu ikiwemo uongofu wa Sinodi yatakayowezesha Kanisa kuwa jumuishi.
Padri Makunde alisema hayo katika Mkutano wa Baada ya Sinodi, ikiwa ni njia ya kusonga mbele kwa Kanisa Katoliki baada ya miaka mitatu ya harambee iliyoangazia kukumbatia sauti za makundi mbalimbali ndani ya Kanisa hilo.
Padri Makunde aliyekuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa XVI wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu, alieleza mambo muhimu kutoka kwenye Hati ya Mwisho ya kuimarisha Sinodi ndani ya ukanda wa AMECEA na Kanisa zima.
Katika hotuba yake kwa wajumbe wa Sekretarieti ya AMECEA, Padri Makunde, alisisitizia umuhimu wa malezi ya sinodi katika ngazi zote kuanzia familia.
Alisema kuwa familia ndio mazingira ya kimsingi ambapo watu hukutana kwanza na maadili kama vile heshima, huruma, na kusikiliza, na kanuni kuu za sinodi.
Aidha Padri Makunde alisema familia zinapokumbatia roho ya kutembea pamoja, zinaimarisha Kanisa na jamii na kuunda jumuiya iliyojumuisha zaidi na inayoendeshwa na misheni.
Wakati huohuo Padri Makunde alisema japokuwa suala la nafasi ya wanawake katika Kanisa limekuwa likisumbua katika safari yote ya Sinodi, na pia ni mojawapo ya maeneo ya utafiti wa kina, akisema, “Sinodi imepanua fursa ya wanawake katika nafasi za uongozi.”
Zaidi ya hayo, mkutano huo ambao ulijumuisha zaidi ya wajumbe 360 kutoka kote ulimwenguni, ulikubali kwamba Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo (SCCs), ni mifumo bora ya maisha ya Sinodi.
Maeneo mengine yaliyosisitizwa na Padri Makunde ni kuongezeka kwa ushirikiano wa waamini katika uongozi wa Kanisa, kuchunguza huduma mpya ya kusikiliza na kuambatana na Waamini walei, na mkazo wa Sakramenti ya Ubatizo kama mzizi wa aina mbalimbali za karama, wito, na huduma.
Kuhusu Kanisa la Sinodi katika Misheni, Padri Makunde alipendekeza kuwa Sekretarieti ya AMECEA kwa kushirikiana na Sekretarieti za Kitaifa, wasambaze hati ya mwisho ya Sinodi kwa Familia ya Mungu na kutafuta njia zinazowezekana za kuanzisha mafunzo hayo.
Alipendekeza pia tafsiri ya maandishi katika lugha za kienyeji na za kitaifa ili ujumbe uweze kueleweka kwa watu wote katika kanda, na wakati huo huo mikutano ya wanachama kuchukua sinodi kama jambo mtambuka katika programu zote za kichungaji.
Kwa mujibu wa Padri Makunde, somo la Sinodi linahitaji kuanzishwa katika nyumba za malezi kwa Wakleri, Watawa, na Makatekista na Kanda, linapaswa kuona njia za kukuza mazungumzo ya Sinodi katika roho kwa mtindo wa kikanisa wa SCCs.
Aliongeza kuwa Kanda ya AMECEA inapaswa kuimarisha jukumu la walei katika kujenga Kanisa la Sinodi katika utume, na pia kuchunguza njia za kuwashirikisha Mapadri katika safari ya Sinodi kupitia chama cha kitaifa na kijimbo cha Mapadri.
Alihitimisha kwa kusema na kuongeza kwamba kuanzisha shule za Sinodi kwa namna mbalimbali, ni uwezekano mwingine kama njia ya kusonga mbele, na pia kuimarisha ushirikiano uliopo wa Maaskofu na wakuu wa Dini.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amewataka Washairi kutafakari jinsi imani inavyohoji maisha, kwani haiwezi kupunguzwa kwa dhana.
Baba Mtakatifu alisema hayo katika barua yake aliyoiandika, baada ya kitabu cha “Antolojia ya shairi la kidini”, ambapo katika barua hiyo, alibainisha kuwa ushairi hauzungumzii ukweli kuanzia kanuni za kufikirika, bali kusikiliza ukweli wenyewe, kazi upendo, kifo na mambo ya maisha.
Baba Mtakatifu aliongeza kwa kusema, “Washairi wapendwa, ninajua mna njaa ya maana, na kwa sababu hiyo, pia mnatafakari jinsi imani inavyohoji maisha. Maana hii haiwezi kupunguzwa kwa dhana, hapana. Ni maana ya jumla ambayo inachukua mashairi, ishara na hisia.”
Alisema kwa kuzingatia uzoefu huo wa kibinafsi, alipenda kushiriki nao baadhi ya mambo ya kuzingatia kuhusu umuhimu wa huduma yao. “Ningependa kueleza ya kwanza kama hii, nyinyi ni macho yanayotazama na kuota. Ninyi sio tu kuangalia, lakini pia ndoto. Mtu ambaye amepoteza uwezo wa kuota hukosa mashairi, na maisha bila mashairi hayafanyi kazi. Sisi wanadamu tunatamani ulimwengu mpya ambao pengine hatutauona kikamilifu kwa macho yetu, hata hivyo tunautamani, tunautafuta, tunauota. Mwandishi wa Amerika ya Kusini alisema kwamba tuna macho mawili: moja la mwili na lingine la kioo. La mwili, tunatazama kile tunachokiona, na la kioo tunatazama kile tunachoota. Masikini tukiacha kuota, masikini sisi! Msanii ni mtu anayetazama kwa macho yake na wakati huo huo huota, anaona kwa undani zaidi, anatabiri, anatangaza njia tofauti ya kuona na kuelewa mambo yaliyo mbele ya macho yetu.”
Baba Mtakatifu aliongeza kwambaushairi hauzungumzii ukweli kuanzia kanuni za kufikirika, bali kwa kusikiliza ukweli wenyewe, kazi, upendo, kifo, na mambo yote madogo madogo yanayojaza maisha.
Aliongeza pia kwamba Sanaa ni dawa dhidi ya mawazo ya kuhesabu na usawa, na kubainisha kuwa hiyo ni changamoto kwa mawazo yao, kwa njia yao ya kuona na kuelewa mambo.
Aliwasihi kufahamu kuwa Kanisa pia linahitaji fikra zao, kwa sababu linahitaji kupinga, kuita na kupiga kelele, akisema, “Hata hivyo, ningependa kusema jambo la pili: ninyi pia ni sauti ya wasiwasi wa kibinadamu. Mara nyingi wasiwasi huzikwa ndani ya moyo mnajua vizuri kwamba msukumo wa kisanii haufariji tu, bali pia unasumbua, kwa sababu unaonesha ukweli mzuri wa maisha na wale wa kutisha.”
Pia, alisema Sanaa ni uwanja wenye rutuba ambamo upinzani maarufu  wa ukweli kama Romano Guardini alivyowaita, huoneshwa, ambao kila wakati unahitaji lugha ya ubunifu na isiyo ngumu, yenye uwezo wa kuwasilisha ujumbe na maono yenye nguvu.
Alibainisha kwamba anazungumza juu ya mvutano wa roho, ugumu wa maamuzi, na hali inayopingana na uwepo, kwani kuna mambo katika maisha ambayo, wakati mwingine, hawawezi hata kuelewa, ambayo pia hawawezi kupata maneno sahihi.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amewataka watu wote waliopewa jukumu la kuwatumikia watu, watekeleze jukumu hilo wakiwajibika kwa unyenyekevu na huruma, badala ya kutumia nafasi zao kuwafanya kuwa chombo cha unafiki, kiburi na wizi.
Aliyasema hayo akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume mjini Vatican kwa kuwageukia waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro wakati wa Dominika ya Novemba 10, 2024, ambapo alianza kwa kusema, “Leo Injili ya liturujia (Mk 12,38-44) inatuambia kuhusu Yesu ambaye, katika hekalu la Yerusalemu, anashutumu mtazamo wa unafiki wa baadhi ya waandishi mbele ya watu (rej Lk 12, 38-40).
“Wale wa mwisho walikuwa wamekabidhiwa jukumu muhimu katika jumuiya ya Israel: walikuwa wanasoma, waliandika na kutafsiri Maandiko. Kwa hiyo waliheshimiwa sana na watu wakawaheshimu. Zaidi ya kuonekana kijujuu, hata hivyo, tabia yao mara nyingi haikupatana na yale waliyofundisha. Hawakuwa thabiti. Wengine, kiukweli, wenye nguvu katika ufahari na mamlaka waliyofurahia, waliwadharau wengine kwa kuwatazama kuanzia juu hadi chini,” Papa aliongeza kusema, “Ni jambo baya sana kutazama mtu kunzia juu hadi chini,” alisema Baba Mtakatifu.
Baba Mtakatifu alikazia kusema kuwa “Tukumbuke kile ambacho Yesu alisema katika sala ya mtoza ushuru na mfarisayo (Lk 18,9-14). Wao lakini sio wote walitenda kama watu mafisadi, wakichochea mfumo wa kijamii na kidini ambao ulikuwa kawaida kuchukua faida ya wengine, hasa wasio na ulinzi, kwa kutenda dhuluma na kutokujali kabisa.”
Papa amesisitiza kwamba “Kiukweli, kwa neno lake na kielelezo chake, kama tujuavyo, anafundisha mambo tofauti sana kuhusu mamlaka. Anazungumza juu ya hilo kwa njia ya kujitolea na huduma ya unyenyekevu (rej. Mk 10:42-45), juu ya huruma ya umama na ubaba kwa watu (rej. Lk 11:11-13), hasa wale wanaohitaji sana (Lk 10, 25-37).” Kwa njia hiyo Yesu “ Anawaalika wale walio na majukumu kuwatazama wengine, kutoka katika nafasi zao za madaraka, si kuwadhalilisha, bali kuwainua, kuwapa matumaini na msaada.”
Baba Mtakatifu Fransisko aliwataka kujitafakari na kuzitafakari tabia zao katika maeneo yao ya uwajibikaji, akiwasisitiza kuwa wanyenyekevu, na si wenye kujivunia juu ya vyeo walivyo navyo.

Page 1 of 39