Dar es Salaam
Na Pd. Richard Mjigwa- C.PP.S
Mwenyeheri Giovanni Merlini ni Mtume mwenye ari na mwamko wa Fumbo la Pasaka ya Kristo linaloleta wokovu, shuhuda, amini wa Injili na mshauri mwenye busara.
Hayo yamo katika Waraka wake wa Kitume wa Baba Mtakatifu Fransisko wa kumtangaza Mwenyeheri huyo, ambaye Sikukuu yake itaadhimishwa kila mwaka Januari 12.
Mwenyeheri Giovanni (pichani) yeye alikuwa ni mhubiri mahiri; Mshauri mwenye busara na mjumbe wa matumaini na amani katika Kristo Yesu.
Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anajifunua, kwa watu wake waliokuwa wamepokea Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi.
Hii ni siku ya Ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye” (Mt, 3:13-17, Mk, 1:9-11, Lk, 3:21-22). Ni tukio linalotakatifuza maji yote ya Ubatizo, na umuhimu wa maisha ya sala. Rej Lk, 3:21 na katika kusali, Kristo Yesu anawafundisha Wafuasi wake kusali. Rej KKK 2607.
Huu ni mwaliko kwa Waamini kutafakri ufunuo wa Sura na Sauti ya Mungu. Ubatizo wa Bwana unahitimisha maadhimisho ya Kipindi cha Noeli, Mwanzo wa: maisha na Utume wa Kristo na ni siku maalum ya Ubatizo kwa watoto wachanga, changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwarithisha watoto wao zawadi ya imani.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Fransisko, Dominika Januari 12, 2025 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini, kuwa ni Mwenyeheri na ambaye alizaliwa tarehe 28 Agosti, 1795 huko Spoleto, Perugia nchini Italia.
Akapewa daraja Takatifu la Upadri Desemba 19, 1818. Agosti 15, 1820 akajiunga na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, lililokuwa limeanzishwa na Mtakatifu Gaspari del Bufalo Agosti 15, 1815. Alijiunga na Shirika baada ya kuvutiwa sana na mahubiri yaliyotolewa na Mtakatifu Gaspari, kuhusu Fumbo la Ukombozi chemchemi ya upendo wa kimisionari.
Kumbe, Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni msaada kwa kila Mkristo kwa kuwa Damu ya Kristo ndiyo msingi wa ukombozi wa mwanadamu, na ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wote.
Tasaufi hii ina msingi wake katika, na Neno la Mungu na katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ambalo ndilo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa, na maisha ya Mkristo kwa jumla.
Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa Imani ya Kikristo, na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. Rej KKK 1324 na 1327. Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, Agano Jipya na la Milele, ikawa ni msingi wa maisha na sadaka, kwa bidii ya kutafakari na shauku ya kitume “cum ardore contemplativo et passione apostolica.”
Mwenyeheri Giovanni Merlini aliishi nyakati za Mapinduzi ya Napoleone, wakati wa mchakato wa mafundisho tanzu ya Kanisa. Papa Pio IX Desemba 8, 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili.
Mwenyeheri Giovanni Merlini akatangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika maisha ya kila siku kwa kutambua mbegu za Ufalme wa Mungu, na hivyo akajipambanua kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu na amani; na shuhuda wa matumaini yasiyotahalisha. “Spes non confundit.”
Kati ya Mwaka 1847 hadi 1873 aliteuliwa kuwa ni Mkuu wa tatu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Kama kiongozi, akaonesha utakatifu wa maisha, udugu, ari na mwamko wa kimisionari; ukaribu na majadiliano katika ukweli na uwazi; kupima mang’amuzi ya maisha na utume wa Kimisionari mbele ya Msalaba. Ni katika wakati wa uongozi wake, Shirika likapanuka na kuenea nje ya mipaka ya Italia hadi Kaskazini mwa Ulaya na nchini Marekani.
Katika maisha na utume wake alibahatika kuwa ni kiongozi wa maisha ya kiroho kwa Mtakatifu Maria De Mattias, utume alioutekeleza kwa kipindi cha miaka arobaini na miwili.
Akasaidia kujenga na kuwaimarisha Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC. Katika mashauri yake alikazia: majadiliano katika utu, heshima na ukuaji wa maisha ya kiroho, daima wakitafuta mapenzi ya Mungu.
Mwenyeheri Giovanni Merlini, alisaidiana na Mtakatifu Gaspari del Bufalo kupyaisha maisha ya Waamini na Makleri kwa namna ya pekee kama yaliyoasisiwa na Papa Pio VII (1800-1823: wa 251) na Pio 1X kwa njia ya mahubiri, mafungo, na hata wakati mwingine akahatarisha maisha yake kwa kutangaza Injili miongoni mwa majangili, kielelezo cha mtume wa msamaha unaobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Kristo.
Fumbo la Pasaka ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba Waraka wa Kitume wa “Amantissimus human” wa Mwaka 1862 ulionesha umuhimu wa Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo, na kunako mwaka 1849 katika Waraka wa Kitume wa “Redempti sumus,” Sikukuu ya Damu Azizi ya Yesu, ikatangazwa kuwa ni Sikukuu kwa Kanisa zima. Mwenyeheri Giovanni Merlini akaitupa mkono dunia tarehe 12 Januari 1873 kwa ajali.
Tarehe 10 Mei 1973, Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, likamtangaza kuwa ni Mtumishi wa Mungu. Tarehe 23 Mei 2024 Baba Mtakatifu Fransisko akaruhusu atangazwe kuwa ni Mwenyeheri. Katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Dominika tarehe 12 Januari 2025 akatangazwa kuwa ni Mwenyeheri.
Jumamosi tarehe 11 Januari 2025, kukafanyika Ibada ya mkesha wa nguvu ukiongozwa na AskofuVincenzo Viva wa Jimbo Katoliki Albano, nchini Italia. Misa ya shukrani imeadhimishwa Jumatatu, tarehe 13 Januari 2025 kwa kuongozwa na Askofu Mkuu Renato Boccardo wa Jimbo Kuu la Spoleto, Italia.
Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini kuwa ni Mwenyeheri, anasema, kwa hakika alikuwa ni Mtume mwenye ari na mwamko wa Fumbo la Pasaka ya Kristo linaloleta wokovu, shuhuda amini wa Injili na mshauri mwenye busara.
Sikukuu yake itakuwa inaadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Januari. Baba Mtakatifu Fransisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana alisema, Giovanni Merlini, Padri Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi, alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume kwa watu wa Mungu, akawa mshauri mwenye busara kwa roho nyingi, na mjumbe wa amani.