DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewataka Waamini kuuishi Ukristo wao, huku wakilishika Neno la Mungu.
Kardinali aliyasema hayo hivi kalibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa Vijana 112 katika Parokia Teule ya Mtakatifu Stephano wa Hungaria – Makurunge, jimboni humo.
“Sakramenti hii ya Kipaimara ni muhimu sana kwa Mkristo kuipokea, kwa sababu inakupatia uwezo mkubwa wa kumtangaza Kristo mahali,popote pale bila hofu. Pia, inakupatia nguzo kubwa ya kuwa askari hodari wa imani ya Kristo,” alisema Kardinali.
Alisema pia kuwa Waamini wengi hawasikilizi sauti ya Kristo, na hawafuati maneno yake, akiwasisitiza kuepuka kupotoshwa kwa maneno ya uongo, bali wafahamu kwamba sauti ya Mungu ndiyo inatakiwa kufuatwa.
“Sijui wamepotoshwa na kitu gani kibaya, bali utakuta wanafuata sauti za watu waongo ambao hawawezi kuwafikisha safari ya kuelekea kwa Baba Mungu. Ndugu zangu Waamini, nawaomba sana fuateni sauti ya Kristo, ambayo itawasaidia katika safari yenu ya kumtangaza Yesu Kristo ili baadaye muwe watu wema machoni mwake.
“Pia, tutambue kwamba Mungu ametuambia tusikilize sauti ya mwanaye. Huyu ndiye mwanangu niliyependezwa, naye msikieni, Mungu alikuwa na maana kubwa sana kutamka maneno haya. Tuwe watu wa kupendana, kuheshimiana, na kusaidiana kila wakati,” alisema Kardinali.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Watakatifu Wote – Kiluvya, Padri Danipaso Bitegeko, ambaye pia ni Msimamizi wa Parokia hiyo Teule, alimshukuru Kardinali Pengo kwa kufika parokiani hapo, na kuwapatia Vijana Sakramenti hiyo ya Kipaimara.
Naye, Mwenyekiti wa Parokia Teule, Gabriel Mwalo alisema kuwa kwa sasa wapo katika ujenzi wa nyumba mpya ya Mapadri, ili Padri aweze kukaa hapo hapo, kwani kwa sasa Waamini wanazidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo wanahitaji huduma ya kiroho kwa karibu.