Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Ujenzi Barabara Sabasaba-Sepuka kwa lami waanza

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kwanza ya kikazi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kwanza ya kikazi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo.

SINGIDA

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka wananchi watakaopitiwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Sepuka-Ndago-Kizaga mkoani Singida yenye urefu wa Kilometa 77.6, kutohujumu mradi huo kwa kutokuiba vifaa ili kufanikisha ujenzi huo kukamilika kwa wakati.
Bashungwa aliyasema hayo katika hafla ya kukabidhi mradi huo kwa Mkandarasi Henan Highway Engineering Group Ltd ya nchini China, kuanza kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
“Serikali imetoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali kote nchini ikiwemo ya Mkoa wa Singida, hivyo niwapongeze wananchi kwa ushirikiano mnaowapa wakandarasi. Hata hivyo, nitoe tahadhari ya wizi wa mali na vifaa vitakavyotumika katika ujenzi, naomba viongozi muwasisitize wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi kuepukana na uhalifu wa aina yoyote kwa vifaa hivyo, badala yake wavilinde,” alisema Bashungwa.
Katika hatua nyingine, Bashungwa aliwataka Wakala wa Barabara nchini (Tanzania National Roads Agency: TANROADS), kuhakikisha wanamsimamia kikamilifu mkandarasi huyo ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa na ubora.
“TANROADS nyie ndio wenye dhamana ya kusimamia ujenzi wa barabara hapa nchini, jipangeni vizuri ili ujenzi ukamilike ndani ya muda uliokusudiwa na kwa ubora, na si vinginevyo,” alisema Bashungwa.
Bashungwa alisema kwamba ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Sh.Bilioni 88.583 bila kujumlisha kodi ya ongezeko la thamani VAT Sh. Bilioni 15.944, chini ya kampuni hiyo.
Bashungwa alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta na watendaji wenzake, pamoja na viongozi wote wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa vizuri hafla hiyo, na kueleza kuwa Singida imefungua njia, na sasa ataanza ziara ya kwenda kuwakabidhi wakandarasi miradi iliyopo katika wilaya mbalimbali, akiambatana na Wabunge wa maeneo ilipo, ambayo imekwishatengewa fedha na Serikali.
Naye Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, naye alikuwa mwenyeji wa makabidhiano hayo ya barabara hiyo, pamoja na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, aliwataka Watanzania kuwa wamoja, hasa katika suala la kuinua uchumi wa nchi, kazi ambayo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeianza kwa kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa uchumi.
“Mimi kitaaluma ni mchumi, hakuna nchi yoyote duniani ambayo inaweza kukuza uchumi wake pasipo kuwekeza kwenye sekta binafsi, na katika jambo hili hatutarudi nyuma, kwani litaongeza mapato ya nchi na kutuwezesha kutoa ajira nyingi, ikiwa ni pamoja na za wauguzi ambao watakuwa wakifanya kazi kwenye vituo vya afya tulivyovijenga nchi nzima,” alisema Mwigulu.
Alisema kwamba kumekuwa na tofauti katika jambo hilo la uwekezaji hadi kufikia hatua ya kutaka kufarakana kati yao, ambao wapo wanaoamini kwamba kupitia uwekezaji, watapiga hatua, na wenzao ambao hawautaki, wakidai Serikali inaweza kufanya kazi hiyo peke yake.
Mwigulu alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambayo alikuwa ameanza kuiomba tangu alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza, barabara ambayo inakwenda kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya za Ikungi, Iramba, Mkoa wa Singida na nchi kwa ujumla, kutokana na kupata masoko ya mazao yao.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, licha ya kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo, alitoa onyo kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe aache kumsakama Rais Samia kwa kumteua Mohamed Mchengerwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) si kwa sababu ni mkwe wake, bali inatokana na uchapa kazi wake uliotukuka kabla hajawa waziri, na baada ya kuwa Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Akitoa taarifa fupi ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta, alisema kwamba barabara hiyo inapita katika maeneo yenye uchumi wa kilimo, misitu, madini na rasilimali nyingi ambazo hazichangii kikamilifu kwenye Pato la Taifa, kutokana na kutopitika kiurahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya mkoa huo, alisema una vijiji 441, kati ya vijiji hivyo, vijiji 341 tayari vina umeme, na vijiji 100 ambavyo havina, wakandarasi wapo kazini.
Alisema pia kwamba mambo hayo yote yanafanyika kwa ufundi na ustadi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya mambo mengi katika miradi ya maji, sekta ya elimu na mingine mingi, ikiwemo minara ya simu na kilimo cha mazao yote ya alizeti, mpunga, mahindi, dengu, vitunguu, pamba, na kueleza kuwa anaamini sasa kwamba Mkoa wa Singida unakwenda kuwa kinara wa uzalishaji wa mafuta ya kula, na mazao yote ya chakula na biashara yanayolimwa mkoani humo.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo iliyopewa kazi ya kujenga barabara hiyo, Huang Lele, alisema kwamba wamejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa, na akaomba kupewa ushirikiano kwa kuzingatia kuwa China na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.