Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Serikali yamuamini Askofu Kyando

Mhashamu Eusebius Kyando. Mhashamu Eusebius Kyando.

NJOMBE

Na Mathayo Kijazi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amesema kuwa Serikali ina Imani kwamba kupitia Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Njombe Mhashamu Eusebius Kyando, mkoa huo utaendelea kuwa na amani na upendo.
Waziri Jenista aliyasema hayo wakati akitoa salamu za Serikali akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyealikwa kuwa mgeni rasmi katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kumsimika na Kumuweka Wakfu, Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Njombe, Mhashamu Kyando, iliyoadhimishwa hivi karibuni jimboni humo.
“Lakini hatuna shaka sisi kama Serikali, na Mheshimiwa Rais Samia ameniambia kwamba tunaamini katika wewe, kutakuwa na amani kwenye Jimbo la Njombe, kutakuwa na upendo uliopitiliza nafsi kwa Viongozi wa Dini, Viongozi wa Serikali, Viongozi wa Taasisi zingine, na Waamini wote wa Kanisa Katoliki hapa kwenye Jimbo la Njombe. Na kwa kuwa Jimbo hili linakwenda pia katika mikoa mingine, tutaambukiza haya na hata katika mikoa mingine,” alisema Waziri Jenista.
Waziri huyo alisema kuwa Mkoa wa Njombe wenye idadi ya watu zaidi ya 885,946 kwa takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, ni miongoni mwa Mikoa yenye fursa kubwa kiuchumi katika Sekta ya Kilimo, Madini, Uvuvi na Biashara.
Wakati huo huo Jenista, alimpongeza Mkuu wa Mkoa pamoja na Viongozi wengine mkoani humo, kwa kutangaza kilimo kama jambo la msingi na la kuleta maendeleo katika Mkoa huo.
Aidha, aliwapongeza kwa kujikita katika mazao yenye tija kwenye uchumi, ikiwemo mbao, viazi mviringo, parachichi, chai, na mahindi, kwani Rais ameweka mazingira wezeshi kuhakikisha mazao hayo yanakuwa ya kibiashara na yanawanufaisha wakulima wa Mkoa huo, na wa Tanzania kwa ujumla.
Waziri Mhagama alibainisha kuwa ndani ya Serikali, Bajeti ya Kilimo imeendelea kuongezeka, ili kuhakikisha kilimo kinasonga mbele.
Alibainisha kuwa kwa upande wa Sekta ya Madini, Mkoa huo umebahatika kuwa na hifadhi kubwa ya madini ya chuma, makaa ya mawe, katika Wilaya ya Ludewa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka akitoa salamu za mkoa huo katika misa hiyo, alisema kuwa Mkoa huo unaongoza kwa watoto wenye udumavu kutokana na utapiamlo, na kuwataka Viongozi wa Dini na Taasisi mbalimbali kuwasaidia wazazi kuwaandaa watoto katika lishe bora.
“Mkoa wa Njombe tuna changamoto kubwa sana ya tatizo la lishe, na kwenye taarifa za Kiserikali, mkoa wetu unaongoza kwa kuwa na watoto wengi wenye udumavu, na sisi kama Mkoa tuna kampeni ya Kitaifa ambayo pia tungeomba Viongozi wa Kanisa na Madhehebu yote watusaidie, kwa sababu watoto wana ukondefu, watoto wana utapiamlo, watoto wana udumavu…
“Lakini Mkoa wetu, Mungu ametuneemesha kwa vyakula vingi, lakini bado hali ya afya ya watoto wetu siyo nzuri. Ningeomba kupitia hadhara hii, Kanisa na Viongozi wote waliopo hapa, Viongozi wote wa Dini, Viongozi wa Serikali, na Viongozi wa makundi yote, tuweze kushirikiana na kushikamana, kuona namna ambavyo tutasaidia wazazi kuwalisha na kuwandaa watoto katika lishe bora ili waweze kufanya vizuri katika maisha yao,” alisema Mtaka.
Aidha, Mtaka aliongeza kuwa endapo wadau hao wakiwemo Viongozi wa Taasisi za Dini wakiongeza nguvu kuunga mkono jambo hilo, na wazazi wakaelimishwa kuwapa watoto wao lishe bora, utapiamlo kwa watoto Njombe utakwisha.
Mtaka alitumia nafasi hiyo kuwaomba wazazi na walezi mkoani Njombe kuwapeleka watoto wao shuleni, kwani siyo busara watoto kubaki nyumbani katika kipindi hiki ambacho hakuna malipo yoyote.
“Tuwaombe wazazi kupitia hadhara hii watusaidie ili watoto waende shule. Si busara watoto wabaki nyumbani katika wakati huu ambao mahitaji yote ya shule yapo. Kwa mtoto ambaye hana ‘uniform’, isiwe sababu ya kutokwenda shule, aende tu, na akifika huko tutaona ni namna gani ya kumsaidia,” alisema Anthony Mtaka.
Aliwasisitiza wazazi kuzingatia na kusimamia suala la elimu, ili jamii iweze kushindana kwenye Taifa ambalo linakwenda kwenye ushindani mkubwa wa kiuchumi.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.