Dar es Salaam
Na Celina Matuja
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, amewaasa Mapadri, Watawa na waamini kwa ujumla kutambua kwamba wanapokabiliana na kifo, hawapaswi kughafilika, kukata tamaa na kuona mambo yote yameharibika, bali watambue kwamba kifo cha Mkristo ni sehemu ya safari yake ya kuungana na Kristo katika ushindi wake.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kumwombea marehemu Padri Novatus Mbuya-ALCP/OSS, aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mtume, Kijitonyama, jimboni humo, iliyofanyika parokiani hapo, ikihudhuriwa na Maaskofu Wasaidizi Mhashamu Stephano Musomba na Mhashamu Henry Mchamungu.
Alisema kuwa Mkristo wakati wote anatakiwa kuwa tayari kwa kuweka mahusiano mema na Mungu katika maisha yake yote, na asingoje kesho kwa sababu maisha ya mwanadamu hayapo katika mamlaka binafsi.
“Nikiwauliza kwa sasa wangapi wapo tayari kuungana na Kristo, wachache mtanyoosha, na baadhi mtajificha kwa sababu mnataka kuniambia kwamba ‘ndiyo’, lakini siyo sasa. Ila tutambue kwamba hakuna hata mmoja wetu anayepanga siku zake,”alisema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi aliongeza kwamba huo ni mwaliko muhimu kupitia Maandiko Matakatifu, kwa habari ya Mlima Zioni, ambao unadokeza Mji Mtakatifu wa Yerusalem kwa maana ya Maisha ya Mbinguni, ambayo yameandaliwa na Mungu Mwenyezi kwa ajili ya Mwanadamu.
Alisema pia kuwa kwa Zioni ya Mbinguni, Mwandamu atafika huko ikiwa tu amepatamani, amepatafuta, na amepashughulikia maisha yake yote kwa kuweka mahusiano yake vizuri kiroho na Mwenyezi Mungu.
Aliongeza kwa kusema kwamba Zioni ni kushirikishwa Mwanadamu na Ushindi wa Kristo aliyeteswa, aliyekufa, aliyefufuka, na ambaye kila amwaminiye ameunganishwa kwa njia ya Ubatizo na kuwekwa kuwa shahidi wake.
Aliongeza kusema kuwa kitendo cha kukusanyika waamini kumwombea na kumuaga Marehemu Padri Novatus Mbuya, ni upendo, lakini pia ni kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwani kibinadamu wanaweza kusema amefariki akingali kijana.
Padri Novatus Mbuya alifariki dunia Septemba mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Muhimbili National Hospital: MNH), kwa ugonjwa wa saratani ya tumbo.
Padri Mbuya alizaliwa Juni 25 mwaka 1978 katika Jimbo Katoliki la Moshi, na alipata Daraja Takatifu la Upadri Februari Mosi mwaka 2012. Hadi anakutwa na umauti mwaka huu, Padri Mbuya alikuwa anafanya Utume wake akiwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu Mtume, Kijitonyama, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.