Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Waziri Mkuu asisitizia maboresho Daftari la Kudumu la Wapigakura

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

”Zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni muhimu sana katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia”.
Kauli hii ilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika hotuba yake ya  uzinduzi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura  Mkoani Kigoma uliofanyika kwenye uwanja wa Kawawa katikaka Manispaa ya Kigoma  - Ujiji, Julai 20, 2024.
Uboreshaji huo utafanyika katika mizunguko 13, na mzunguko wa kwanza unahusisha Mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi, kisha Geita na Kagera, ikifuatiwa na Mwanza, Shinyanga na baadae Mara, Simiyu na sehemu ya Mkoa wa Manyara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa zoezi hilo lina lengo la kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapata na kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
”Vile vile, umuhimu wa zoezi hili unatokana na ukweli kwamba hii ni hatua muhimu ya maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwaka 2025 hapa nchini. Pia kutokana na uwepo wa kundi kubwa la wananchi waliopata sifa ya kiumri tangu uchaguzi uliopita, zoezi hili ni muhimu kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura wapya”.
Akieleza kuhusu umuhimu zoezi hilo Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa maboresho ya daftari la mpiga kura, mbali ya kuandikisha wapiga kura wapya, pia yanalenga kutoa fursa muhimu kwa wapiga kura ambao kwa sababu moja au nyingine, kadi zao za mpiga kura zimepotea au kuharibika, au wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda jingine waboreshewe taarifa zao ili wawe na sifa za kuwawezesha kupiga kura katika uchagu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Aliwataka wote waliohama kutoka kwenye vituo vyao vya kupigia kura au kupoteza  kadi zao, kufika kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura ili kuboresha taarifa zao na kupatiwa kadi mpya zitakazowawezesha kupiga kura.
Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022; inakadiriwa kuwa jumla ya wapiga kura wapya 5,586,433 wataandikishwa, wakiwemo waliotimiza umri wa miaka 18 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu uliopita, na ambao watatimiza umri huo ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. ”Kwa mujibu wa taarifa za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inakadiriwa kuwa wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao”.
Idadi hii siyo ndogo kwenye zoezi la kupiga kura. Hivyo, nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa, iwe kwa kurekebisha taarifa au kuhama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda lingine, asisite kufika katika kituo cha kuandikisha, kwani Tume imeshajipanga ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa.
Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa ili kufanikisha zoezi hili, kila Mtanzania, Asasi za Kiraia, Vyama vya Siasa, Jeshi la Magereza na Vyuo vya Mafunzo, Vyombo vya Habari, Mawakala Vyama vya Siasa na Watendaji wa walioteuliwa na Tume, wanapswa kutimiza wajibu wao ili zoezi hili liweze kufanikiwa.
Wajibu wa kila Mtanzania:
Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa kila Mtanzania ashiriki katika usimamizi wa suala hilo, kwani wanaotakiwa kuandikishwa ni raia wa Tanzania tu wenye sifa zilizobainishwa kwa mujibu wa sheria. ”Wananchi ni watambuzi wa kwanza, niwasihi sana tuwe wazalendo, huu ni wajibu wa raia wa Tanzania kuhakikisha wanaoandikishwa ni Watanzania tu”.
Jeshi la Magereza, vyuo vya Mafunzo na Uhamiaji:
Hapa Waziiri Mkuu anasema kuwa, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu, umeongeza kundi jingine ambalo ni wafungwa wanaotumikia vifungo vya chini ya miezi sita gerezani, au kwenye vyuo vya Mafunzo na mahabusu hawa wote watapata nafasi ya kupiga kura. Hivyo Jeshi la Magereza na upande wa Zanzibar Vyuo vya Mafunzo wanawajibika kuweka miundombinu wezeshi ili Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iweze kutekeleza wajibu huo kwa ufanisi.
Aidha, Jeshi la Uhamiaji liwajibike kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuwatambua na kutoa taarifa za uwepo wa mtu au watu ambao sio raia wa Tanzania, walioandikishwa tayari, au wanaopanga kwenda kuandikishwa, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema dhidi yao.
Wajibu wa Vyama vya Siasa  Majaliwa anatoa rai kwa viongozi wa Vyama vya Siasa kuhakikisha mawakala wao wanatoka kwenye mitaa, Kijiji na shehia husika ili waweze kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kuwatambua watu wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura.
Mawakala wa Vyama vya Siasa:
Anasema kuwa kwa upande wa mawakala watakaoteuliwa na Vyama vya Siasa, wanao wajibu wa kutambua watu wenye sifa za kuandikishwa wanaofika kwenye vituo kwa ajili ya kuandikishwa kuwa wapigakura.
Watendaji walioteuliwa na Tume:
”Ninawasihi sana watendaji walioteuliwa na kuanzia ngazi ya Mkoa, Jimbo, Kata na Kituo cha kuandikisha wapiga kura kuwa waadilifu, na watangulize uzalendo kwa kutotoa fursa kwa watu ambao hawana sifa za kushiriki katika uboreshaji. Kila mmoja ajitume, afanye kazi kwa weledi na kutumia lugha nzuri kwa wananchi wanaokuja kujiandikisha”.
Taasisi na Asasi za Kiraia
Anasema kuwa eneo jingine muhimu ni suala la utoaji wa elimu ya mpiga kura, ambapo alizitaka taasisi na asasi zote zilizopewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura kutekeleza zoezi kwa weledi, na wasiingize vitu ambavyo havitakiwi, na ambavyo havipo kwenye makubaliano.
”Wakati wa zoezi hili la uboreshaji daftari la mpiga kura, , hakikisheni mnatekeleza kazi zenu kwa kuzingatia masharti ya vibali na miongozo iliyotolewa na itakayotolewa na Tume. Ni vema wakati wote taasisi ziepuke kufanya masuala ambayo hayamo kwenye miongozo waliyopewa kwa mujibu wa vibali vyao”.
Vyombo vya Habari:  Alisema kuwa Vyombo vya Habari vinao wajibu wa kutumia kalamu zao, kuwakumbusha wadau wa uboreshaji kutumia taratibu zilizoainishwa kwenye sheria, kanuni na miongozo, kutatua au kuwasilisha malalamiko iwapo kutajitokeza changamoto ya aina yoyote wakati wa uendeshaji wa zoezi hili.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa aliwahakikishia Watanzania kuwa  Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amedhamiria kuhakikisha kuwa Uchaguzi unakuwa wa huru na haki.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiandanga, alisema kuwa uzinduzi wa uandikishaji na uboreshaji, mchakato huo umeshirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi, ikiwa ni utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tume imekutana na wadau wa makundi mbalimbali kama vile Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia,Viongozi wa Dini, Makundi Maalum kama vile Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu. Lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato huu unakuwa shirikishi kwa Watanzania wote bila kujali itikadi za Vyama vya Siasa au Dini”
Naye Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele alisema kuwa jumla ya vituo 40,126 vitatumika katika Zoezi la Uboreshaji wa Daftari, ambapo kati ya hivyo, vituo 39,709 vipo Tanzania Bara, na vituo 417 vipo Tanzania Zanzibar.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.