Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Paje Kijiji Chenye Hoteli 35, Watalii kibao,Wanawake walima Mwani

UNGUJA

Na Paul Mabuga

Unaweza kusema kuwa kijiji cha Paje kule Unguja  ni mahali ambapo tamaduni zinapambana ili kuleta moja inayowakilisha mchanganyiko wa watu wanaoishi hapo wakiwa ni wageni wa muda kama watalii, wengine walioamua kuhamia,  na pia wenyeji.

Wakati maeneo mengine ya Unguja, kama Tumbatu na Makunduchi yakipambana na kuhifadhi tamaduni na hasa mila, desturi na historia, Paje inazidi kukaribisha na kukumbatia mchanganyiko wa amali hizo za maisha na kupata kile kinachoitwa ‘cultural amalgamation’.

Ni rahisi kutambua hili, kwani unapokuwa pale Unguja, utashuhudia mji ukijitambulisha kwa mavazi, ambayo kwa akina mama, kama siyo baibui, basi ni nguo ndefu inayofunika mwili na kichwa, huku wanaume wakiwa katika kanzu, ama hata kama ni shati na suruali, kibagarashia  na makubasi, basi ni katika mtindo unaoashiria ustaarabu wa Kizanzibari.

Lakini ukipanda zile daladala za mbao na kusafiri kwa saa nzima hadi  Paje, utakaribishwa mji unaonekana mkiwa umepoa kwa mchana lakini wenye mambo makubwa kinapoingia kiza. Pamoja na kuwa ni kama kijiji, lakini kuna hoteli zaidi ya 35, hizi zote pamoja na malazi na chakula, lakini pia zinatoa burudani mbali mbali kwa watalii, wahamiaji na wenyeji pia.

Paje inapendelewa na wageni wengi wakiwemo watalii, kutokana na fukwe yake kuwa mahali salama kwa kuogelea, na hata kutiara  kwenye maji [kiteboating] na kuwepo kwa maji ‘meupe’.  Wingi wa migahawa na hoteli pia unawafanya  wageni kuvutiwa ma machaguo kulingana na uwezi wao kifedha. Wapo wanaoona heri wafanye huko makazi na kwenda kutembelea vuvutio vya Unguja, na kurudi huko kwa malazi.

Kutokana na mazingira haya, kuna wahamiaji wengi wameingia Paje kwa ajili ya ajira katika sekta ya huduma na biashara, wao ukichanganya na watalii na wenyeji, unapata mchanganyiko wa tamaduni ambazo ni dhahiri kupitia mavazi, lugha na mitindo ya maisha. Mavazi unayoyaona Paje ni nadra kuyaona katika miji kama Unguja, Makunduchi ama Wete.

Katikati ya kuchangamka huko akina mama wameanzisha kikundi cha ujasiriamali ili kufaidika na fursa katika kijiji cha Paje. Walikianzisha mwaka 2011, na wanakiita ‘Furahia Mwanamke’, na wanajishughulisha na kuzalisha na kuuza zao la baharini la mwani.

“Nimefanya kazi kwa miaka 40, lakini tangu tumejiunga na kikundi, niseme tu, mazingira ya biashara ni mazuri, na karibu sisi hivi siyo tegemezi tena, maana mwani una soko kutokana na thamani yake ya virutubisho muhimu,” anasema Hifadhi Ally, mmoja wa wanachama wa kikundi.

Akina mama hawa wameweka hata duka lao hapo Paje, wakiuza bidhaa mbali mbali zinazotokana na mwani, ikiwa ni pamoja na unga, ambao thamani yake inafika hadi shilingi elfu arobaini kwa kilo moja, mafuta ya kupaka, sabuni, pamoja na dawa za mafua.

“Kuna changamoto kadhaa katika biashara zetu, ikiwa ni pamoja na magonjwa kwa mmea wenyewe, na wakati mwingine bei kupungua. Ilifika hadi shilingi 50,000 kwa kilo, lakini sasa hivi bei imeteremka. Ila tunashukuru tunasomesha watoto, na hata tuna mashine ya kusaga mwani,” anasema mwanachama mwingine wa kikundi hicho,Tano Hassan.

Artifisha Abdul Harim, yeye amepata ajira ya kuuza duka la bidhaa za mwani la umoja wa akina mama hawa ambao anasema kwa idadi wapo 34. Katika duka hilo kuna bidhaa nyingi za mwani na kinachovutia kuna mwani wenye rangi nyekundu, mwingine kijani na ipo ya rangi nyeupe pia. Na hizi rangi ni za mimea yenyewe.

Mwani wanaupanda baharini na hutegemea kupwa na kujaa kwake, na kwamba wakati mwingine katika jua kali, kilimo chao huathiriwa. Wanasema kwamba kwa sasa kilimo hicho kimekuwa na faida kidogo kutokana na gharama yake ya uzalishaji kuwa kubwa.

Licha ya malalamiko haya kutokana na akina mama hawa, lakini bado Zanzibat ni nchi ya nane duniani kwa uzalishaji wa zao hilo, na katika hali ya ubora. Na wanakikundi wana msemo wao kwamba “mwani ni pesa, mwani ni chakula, mwani ni zawadi kutoka kwa Mungu.”

“Mwani una sifa nyingi. Sabuni ya mwani ni nzuri kwa watoto na hata kupaka kabla ya kunyoa nywele ama ndevu kwa kuwa inafanya mwili kuwa laini. Pia karajina [unga wake] Unaweza kuchanganywa kwenye sharubati [juisi], tambi, chachandu, kachumbari na kuleta ladha ya kuvutia,” anasema Artifisha.

Paje inajiweka mahala pema, kwani wakati akina mama hawa wanachangamka na mwani, huku utalii nao ukichagiza biashara, lakini pia una nafasi katika maendeleo ya uchumi wa bluu, ambao serikali ya Zanzibar imeiweka kama ajenda yake ya kipaumbele.

Kilimo cha mwani ambacho kwa sehemu kubwa kinaendeshwa na akina mama,  kinatajwa katika na ripoti ya umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Biashara kuwa kimechangia pakubwa katika kuifanya Zanzibar kuelekea kuyafikia Malengo ya Milenia ambayo, pamoja na mambo mengine, yanalenga kupambana na umaskini, na hivyo kuboresha hali za wanawake na watoto.

Mafanikio haya yanapatikana ingawa ripoti hiyo inaonesha kuwa kuna kushuka katika rekodi kwa uzalishaji wa mwani kutoka tani 178,000 mwaka 2016 hadi 81,000 ilipofika mwaka 2021. Lakini hata hivyo, bado zao hilo limeendelea kuwa na mchango mkubwa, huku likitoa ajira kwa akina mama zaidi ya 400 visiwani humo.

Ukiacha Paje, kuna kijiji kinaitwa Makunduchi, huko utamkuta Bibi Nali Kombo! Yeye anakuonesha kuwa unahitaji kujifunza Kiswahili, kwani akikusemesha anakutaka uitikie ‘enhee’, na wala siyo kuitikia kwa kichwa ama kuguna, huko ni kukosa nidhamu.

“Hano pa, swalaa swalaa hiyo” anakuambia, pengine akimaanisha, ‘ameamka alfajiri’, na zaidi anakujibu kwa swali lako la kutaka kujua jinsi huduma bora za afya zilivyomsaidia kupambana na shinikizo kubwa la damu, “dawa maungoni zinaingia, upo!” Anakuona kama unazubaa kidogo, kisha anakuambia, “ useme enhee!”

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.