Amani na Salama! Tumekuwa tukisoma na kutafakari Injili ya Marko, leo Liturjia inatualika kugeukia Injili ya Yohane na hasa sura ile maarufu ya sita, juu ya Yesu kama chakula cha uzima. Mwaka B wa Kiliturjia wa Kanisa kwa kawaida tunasoma Injili ya Marko, lakini Liturjia ya Mama Kanisa ameingiza pia Injili ya Yohane sura ile ya sita kwa Dominika tano mfululizo. Injili ya Marko inatupa masimulizi mawili juu ya muujiza wa Yesu kulisha makutano mikate. Na ndipo tunaona kwa jinsi anavyotoa mkazo na msisitizo huo, hapo Mama Kanisa ameona ili kupata mafundisho ya kina hatuna budi kugeukia sura ya sita ya Injili ya Yohane. Leo tunasikia juu ya muujiza ule wa kugawa mikate kwa watu wengi, na baadaye zaidi katika dominika zijazo tutasikia juu ya mafundisho ya Yesu mkate wa uzima, aliyoyatoa akiwa katika sinagogi la Kapernaumu.
Ni vema ili kupata ujumbe kusudiwa wa Mwinjili Yohane, badala ya kuwahi kuhitimisha juu ya fundisho la Yesu la Ekaristi Takatifu, ambalo kwa kweli linagusiwa sio mwanzoni mwa sura ile ya sita bali mwishoni kabisa, hivyo niwaalike kusoma na kubaki na kile ambacho kipo mbele yetu ili kukwepa kupotoka au kupata maana inayokuwa siyo ile inayokusudiwa na Mwinjili.
Kati ya miujiza iliyofanywa na Bwana wetu Yesu Kristo, ni muujiza huu wa kugawa mikate unaosimuliwa mara nyingi zaidi na Wainjili wote wanne. Wainjili wote haidhuru mara moja wanatupa masimulizi ya muujiza huu, na Wainjili Matayo na Marko wanasimulia mara mbili juu ya muujiza huu, hivyo kufanya masimulizi juu ya kugawa mikate kuwa sita.
Na ndio hapo tunaweza kujiuliza, kwa nini Kanisa lile la mwanzo linatoa msisitizo mkubwa kabisa juu ya muujiza huu? Yesu alitenda miujiza mingine mingi tena mikubwa zaidi, lakini kwa nini Wainjili wote wanne wanatoa mkazo na msisitizo mkubwa kwa muujiza huu? Na kama ndivyo, kwa nini basi miujiza mingine inasimuliwa mara moja peke yake tofauti na muujiza huu wa leo?
Muujiza wa mikate kama unavyosimuliwa na Mwinjili Yohane ni tofauti na jinsi inavyosimuliwa na Wainjili wengine. Na ndio mwaliko wangu leo kujaribu kuingia ndani ya Injili hii ili tuweze kwa pamoja kuchota ujumbe unaokusudiwa kwetu. Na ndio tunaona pia Mama Kanisa ameingiza sura ile ya sita ya Injili ya Yohane kwa Dominika tano mfululizo, ili tuweze kuchota mafundisho ya kina kabisa juu ya utambulisho wa Yesu kama mkate wa uzima.
Tafakari hizi zitusaidie na kutusindikiza tunapoelekea kwenye kilele cha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa hapo Septemba katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Yesu wa Ekaristi Takatifu ni nani haswa katika maisha yako na yangu, katika maisha ya kila mwamini na kwa Kanisa kiujumla. Mababa wa Mtaguso wa II wa Vatikano wanatualika kuona Ekaristi Takatifu kama chemuchemu na kilele cha maisha ya Kanisa. Ni Ekaristi Takatifu inayolifanya Kanisa liwepo, na Kanisa linadumu hata ukamilifu wa dahari kwa kuadhimisha Ekaristi Takatifu.
Kwanza yafaa kutambua kuwa Mwinjili Yohane hauiti kama muujiza bali kama ishara, na pia hatusikii moja kwa moja kuwa Yesu aliifanya mikate na samaki kuwa mingi na wengi ili kuwatosha watu wote, na badala yake ni mikate ile ile na samaki wale wale kidogo waliwekwa kwa ajili ya wote mpaka kila mmoja akapata kadri ya haja na mahitaji yake na hata kusaza.
Na bado wakaweza kukusanya mabaki vikapu kumi na viwili vya mikate, ndio kusema waliweza kupata kila mmoja na bado hawakuweza kumaliza chote kilichowekwa mbele yao. Hivyo tunaona mara moja msisitizo wa somo la Injili ya leo haupo katika ongezeko la mikate wala samaki, na badala yake moyo na roho ile ya kushirikiana kidogo kinachokuwepo kwa wote kadri ya uhitaji wa kila mmoja wetu.
Falsafa ya ulimwengu wa leo ni kuwa na kila kitu kwa wingi katika maisha, iwe ni pesa, afya, elimu, miaka ya kuishi, marafiki, mafanikio, na kadhalika na kadhalika. Na huu ndio ugonjwa wa wengi wetu, wa kujikusanyia, wa kujilimbikizia, wa kujijali na wenye kutaka na kusaka zaidi na zaidi. Ugonjwa huu wa kujilimbikia unaakisi hasa utamaduni wa kifo, unaotokana na maisha yenye kujaa hofu ya kifo, na ndio dalili ya wazi ya kukosa imani, kwani tunakuwa watumwa wa vitu na mali na badala ya kuwekeza katika upendo kwa Mungu na kwa jirani.
Somo la Injili ya leo, Yesu anatufundisha juu ya ugonjwa huu wa kujilimbikizia na kujikusanyia kila kitu, ugonjwa wa kutaka zaidi na zaidi katika maisha, ni njaa ya vitu na mali.Yesu leo anatupa dawa ya ugonjwa wetu huu, dawa ambayo ni kinyume kabisa na mantiki na utamaduni na falsafa ya ulimwengu wetu, Yesu leo anatuonesha njia salama na sahihi ya ugonjwa wa ubinafsi na umimi ni ile ya kushirikiana sote kwa pamoja bila ubaguzi kidogo kinachokuwepo mbele yetu.
Pasaka, ndiyo sikukuu ya Wayahudi ilikuwa karibu. Mwinjili Yohane anatuonesha ni wakati gani Yesu alitenda ishara ile. Ndio kusema mazingira yalikuwa ni pale walipokumbuka kukombolewa kwao kutoka utumwani Misri.
Ndiyo kusema Mwinjili anajaribu kuoanisha na kuhusianisha tukio la ishara ya mikate, pamoja na tukio la kihistoria la kutoka utumwani Misri. Yesu leo anavuka kama vile Musa alivyowavusha Wanawaisraeli katika bahari ile ya Shamu, na ndipo tunaona leo hakuna chombo kinachotajwa kumvusha Yesu.
Kama vile Musa alivyowaongoza watu wengi, ndivyo na Yesu leo wanamkusanyikia watu wengi na hapo anatenda ishara kama vile Musa nyakati za kuwakomboa Wanawaisraeli. Mara mbili Yesu anapanda juu mlimani, ni kama Musa alivyokuwa akipanda juu mlimani na huko kupokea maagizo ya jinsi ya kuliongoza taifa lile teule.