Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Tumaini yakumbuka mchango wa Pd. Haule, Fredy Mosha, John Liveti

Baadhi ya Wafanyakazi wa Tumaini Media, wakiwasili katika Makaburi ya Mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, yaliyoko Pugu, wakati wa ziara ya Kiroho ya kumkumbuka aliyekuwa Mkurugenzi wa Tumaini Media, Padri Paul Haule (Hayati), aliyezikwa hapo. (Picha na Yohana Kasosi) Baadhi ya Wafanyakazi wa Tumaini Media, wakiwasili katika Makaburi ya Mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, yaliyoko Pugu, wakati wa ziara ya Kiroho ya kumkumbuka aliyekuwa Mkurugenzi wa Tumaini Media, Padri Paul Haule (Hayati), aliyezikwa hapo. (Picha na Yohana Kasosi)

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Wafanyakazi wa Tumaini Media wamewakumbuka wenzao waliofariki dunia kwa kufanya ziara maalumu ya kiroho walikozikwa kwenye makaburi ya Kinondoni na Pugu, jijini Dar es Salaam.
Katika Hija hiyo ya kiroho ya kuwakumbuka wenzao waliokuwa wakifanya kazi katika Vyombo vya Habari vya Tumaini Media, pamoja na mambo mengine katika Kuhitimisha Kampeni ya Mwezi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ni kuwaombea marehemu hao.
Akizungumza katika ziara hiyo ya kiroho, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tumaini Media, Arnold Kimanganu alisema kuwa yeye pamoja na wafanyakazi wote walioshiriki, wameguswa sana, kwani sala zao zina faida kubwa kwa wapendwa wao waliotangulia mbele za haki.
“Mimi kama mfanyakazi wa Tumaini Media nikiwakilisha wenzangu, nimeguswa kwa jambo hili jema la kiroho, na natamani sana lisiwe mwisho, bali tuendeleze utaratibu huu wa kuwakumbuka wale ndugu zetu waliokwisha kupumzika, kwa sababu tunafahamu kwamba wote hapa duniani tuko safarini, na mwisho wa safari yetu ni mauti,” alisema Kimanganu.
Aliwasihi kila mmoja katika ziara hiyo ya kiroho, kuiga yale mazuri yaliyowahi kutendwa na wapendwa wao enzi za uhai wao, na kuongeza kuwa watumie nafasi hiyo pia kuwaombea kwa yale mapungufu waliyokuwa nayo wapendwa wao hao, kama yanafahamika.
Naye Sista Leonora John, Mfanyakazi wa Tumaini Media alisema kuwa kila mmoja katika Dunia hii anatakiwa kuutambua mpango wa Mwenyezi Mungu, kwamba amepewa muda maalum wa kuishi hapa duniani, na akaongeza kuwa kifo kinawatenganisha kimwili tu, bali kiroho, wako pamoja.
“….Na kwa namna ya pekee kabisa, tunahitimisha ziara hii katika makaburi ya Pugu ambapo amelala Padri Paul Haule, pamoja na Mapadri wengine ambao wamelitumikia Kanisa Takatifu. Bila shaka tunajifunza kwamba sisi pia tuna safari ambayo tunatakiwa kuimaliza. Hivyo, tukiishi vizuri katika ulimwengu huu, tutayatimiza mapenzi ya Mungu Baba kama Yesu Kristo alivyosema, “Anayeishi vyema, atakuja kwangu, kwa sababu mimi ni njia, ukweli na uzima,” alisema Sista.
Kwa upande wake Mhariri Mkuu wa Gazeti Tumaini Letu, Alex Kachelewa alisema kuwa ipo haja ya kuendelea kuwaombea wapendwa wao waliolala katika Kristo, kwani kila mmoja anatakiwa kuiga uwajibikaji waliokuwa nao wapendwa wao enzi za uhai wao.
“Mama Esther Chilambo namkumbuka kama Mkurugenzi wa Pili wa Radio Tumaini, kabla haijaundwa Tumaini Media. Yeye alikuwa akiamini sana katika kazi, na hasa kuamini yale ambayo anaamini kwamba yanaweza kufanyika. Kwa hiyo, alikuwa ni mwenye misingi ya kusimamia kazi. Nakumbuka alikuwa na ‘column’ yake moja kwenye gazeti Tumaini Letu iliyoitwa ‘Dunia na Maumbile’. Lakini pia nakumbuka maneno machache aliyowahi kusema, “Ukiamua kufanya kazi, basi ifanye kwa moyo wa dhati,” alisema Kachelewa.
Kachelewa aliongeza kuwa Mama Esther Chilambo alikuwa ni mtu mwenye kujiamini katika utendaji kazi, kwani kwa mipango yake, alisaidia pia kuanzishwa kwa gazeti Tumaini Letu mwaka 2004, huku akisimamia mpango wa vyombo vya habari vya Kanisa, hasa Televisheni, iunde king’amuzi chake, ila baada ya kifo chake, mipango hiyo haikuendelea tena.
Naye Gaudence Hyera, Mratibu wa Matukio ya Kanisa wa Tumaini Media, alisema kuwa kufuatia Hija hiyo, wana imani kwamba sala zao zitafika pia Mjini Marseille, Ufaransa, alikozikwa mwanzilishi wa Tumaini Media, Padri Francois Galtier {aliyependa yeye kujiita ‘msela wa kijiweni’}, aliyefariki dunia Mei 17 mwaka 2021.
Gaudence aliongeza kwa kusema, “Kama ambavyo Kanisa linatufundisha kila siku juu ya kuwakumbuka marehemu, na tunatambua kwamba Kanisa lina makundi matatu, lina wale ambao bado wanaishi, ambalo linaitwa Kanisa linalosafiri; kuna wale waliotangulia, linaitwa Kanisa la wafu; lakini pia kuna wale washindi, linaitwa Kanisa la washindi, yaani wale Watakatifu wa Mbinguni;
“Kwa hiyo, ni jambo la muhimu sana ambalo tunalifanya kiimani na kijamii, lakini pia katika masuala mazima ya mahusiano ya kibinadamu, kwamba huyu aliishi katikati yetu. Kwa hiyo kwa namna moja ama nyingine, tunatakiwa kumkumbuka siku kwa siku,” alisema Hyera.
Kwa upande wake Editha Mayemba, Mtangazaji wa Redio Tumaini, alisema kuwa bado wanatambua mchango mkubwa uliofanywa na wapendwa wao, licha ya kwamba kwa sasa wametangulia mbele za haki, ila watayaendeleza mazuri yote yaliyoanzishwa na wapendwa hao.
Makaburi waliyoyatembelea wafanyakazi hao ni Kinondoni kwenye kaburi la aliyekuwa Mkurugenzi wa Pili wa Tumaini Media, Mama Esther Chilambo; kaburi la mtangazaji nguli wa Redio Tumaini Frederick Mosha, ali maafarufu ‘Defao’; na Pugu kwenye kaburi la aliyekuwa Mkurugenzi wa chombo hicho, Padri Paul Haule.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.