Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, akimpatia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara mmoja wa vijana waliopokea Sakramenti hiyo, katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Imakulata, Upanga, Jimboni humo, (kulia kwa Kardinali) ni Paroko wa Parokia hiyo Padri Casmir Kavishe. (Picha na Mathayo Kijazi)
Na Mathayo Kijazi
Mwadhama Polycarp Kardnali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewasihi Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kutambua kwamba kwa sakramenti hiyo wanatumwa kuitangaza habari njema kwa Mataifa.
Kardinali Pengo aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 37, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Imakulata, Upanga, Jimboni humo.
“Ndugu zangu mnaoimarishwa leo katika Sakramenti hii Takatifu, tambueni kwamba mnapopakwa mafuta, mnatumwa kwenda kuifanya kazi ya Mungu ya kuitangaza habari njema kwa Mataifa, yaani mnatumwa kuwatangazia masikini habari njema,” alisema Kardinali Pengo, na kuongeza,
“Masikini hao wanaotangaziwa habari njema, siyo umasikini wa kukosa fedha, kwa sababu kama ni umasikini wa fedha, hata Yesu Kristu mwenyewe alikuwa ni masikini.”
Aidha, Kardinali Pengo aliwasihi vijana hao kufahamu kwamba hata kama ni masikini na wenye kujiona kuwa hawana thamani maishani mwao, lakini Mungu hajawaacha, hajawatupa na wala hajawalaani.
Kardinali Pengo aliongeza pia kuwa heri watu walio masikini ambao wanamtegemea Mungu, kuliko matajiri ambao wanadhani kwamba wana kila kitu, na hivyo hawahitaji uwezo wa Mungu katika maisha yao.
Alisema pia kuwa kuitangaza habari njema ni pamoja na kuyaishi Maandiko Matakatifu, kwani mtu hawezi kuitangaza habari njema kwa kutenda kinyume na mafundisho ya Mungu.
Kardinali Pengo aliwasihi wazazi na walezi kuwasindikiza watoto wao katika kumsifu na kumtukuza Mungu, ili waendelee kudumu kuwa Askari hodari wa Kristo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Casmir Kavishe alimshukuru Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa kufika Parokiani hapo na kuwapatia Sakramenti hiyo Takatifu vijana 37 katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Padri Kavishe aliwashukuru Makatekista na waalimu wote walioshiriki katika kuwafundisha vijana hadi kuwa imara na kuweza kupokea Sakramenti Takatifu, huku akiwasihi vijana hao kuendelea kudumu katika yale yote waliyofundishwa.