ARUSHA
Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Padri Dennis Ombeni amewataka Raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki popote walipo, kuwa mstari wa mbele kulinda uhai wa mtoto angali bado tumboni.
Mambo yanayojumuisha katika kumlinda na kumtetea mtoto, yakiwemo ya ukuaji, kumlinda katika nyanja zote kiuchumi, kiafya na kiakili, na ustawi wa Mtoto.
Padri Ombeni aliyasema hayo katika warsha kwa Vijana na wazazi iliyofanyika jijini Arusha iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu athari zilizopo kwenye muswada wa ujinsi na afya ya kizazi wa Jumuiya ya Afika Mashariki wa mwaka 2021.
Kupitia mkutano huo, Padri Ombeni alieleza kusikitishwa juu ya mauaji katika jamii kati ya wanandoa yanayotokea kwa kisingizio cha wivu wa mapenzi jambo alilosema ni ouvu na linapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwani linaingilia Uhai ambao asili yake ni Mungu.
“Maandiko Matakatifu kupitia Bibilia yanaeleza kwa namna kuu mbili, juu ya thamani ya uhai katika Bibilia, Maandiko Matakatifu yanatetea uhai, hasa pale kwenye Agano la Kale, ambapo baada ya Mungu kumuumba Adamu na kumpatia msaidizi wake Eva, aliwabariki na kusema, enendeni mkazae na kuijaza dunia,”alisema Padri Ombeni.
Alisema pia kuwa uhai wa mwanadamu ni kitu kitakatifu, hivyo unapaswa kulindwa na kutunzwa tangu kutungwa mimba hadi kifo chake cha kawaida. Hivyo muswada huo wa Ujinsi na Afya ya kizazi haupaswi katika Mataifa ya Jumuiya Afrika Mashariki kwani unakwenda kinyume na Utu, Dini na tamaduni za watu hao.
Kwa mujibu wa Padri Ombeni Mswaada huo unatishia uwepo wa Dini na Imani za Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia unadhalilisha Mila na Desturi za watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani hautoi nafasi kwa wahudumu wa afya kutumia dhamiri zao katika kutoe elimu ya afya ya uzazi kwa wanaowahudumia.
Kutokana na hayo na mengine maovu yaliyoko katika Mswaada huo ambao umeakisiwa na kupigiwa debe na baadhi ya vikundi vyenye nia ovu na watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Padri Ombeni amewataka watanzania wote kuungana na wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuupinga Muswaada huo.
Mmoja wa Washiriki wa Mkutano huo, aliyejitambulisha kwa jina la Anna Anatoli alisema ulimwengu umekosa hofu ya Mungu na ndiyo maana imefika hatua wanadamu wanaweka mikakati ya kutowesha Uhai bila kuwa na hofu ya kwamba kazi hiyo ni ya kwake Mungu Muumba ambaye yeye ni asili ya Uhai wenyewe.
“Hatuna sababu ya kushabikia mambo kutoka mataifa ya mbali ambayo kwao wamefika mahali wameona Uhai si zawadi kutoka kwa Mungu kwenda kwa mwanadamu, natamani kuona tunabaki na vyakwetu huku tukiendelea kuwajengea hofu ya Kimungu watoto wetu,”alisema Anna.
Kwa upande wake Betty Sammaye aliwataka wazazi kusimama na kuwapeleka watoto wao Kanisani kwani Mtoto akikuwa kwenye uwepo wa kumcha Mungu ataweza kusimama na kujitetea na Neema ya Mungu itakuwa ndani katika kumwongoza.
Betty amewataka wazazi kuchukua muda kuzungumza na watoto wao, kwani vitu vinabadilika mno kila siku, na kamwe wasikubali watoto wao kutoka nje ya himaya yao bila kufahamu kwa kina ni wapi hasa wanakwenda na wanakwenda kufanya nini.
Muswada huo wa Afya ya Kizazi na Ujinsi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Mwaka 2021 unaelezwa kukiuka maadili, Utu na Dini za watu wa Jumuiya ambao una vipengele vinavyochochoa ngono kwa watoto na Vijana, na pia utoaji mimba.
Na ikiwa muswada huo utaachwa upite, basi itazilazimu nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutunga Sheria kulingana na matakwa ya muswada huo.