Padri Germine Laizer akiwavisha rozari baadhi ya wanachama wapya wa Chama cha Wajane na Wagane
Dar es Salaam
Na Benedikto Agostino
Wajane na Wagane nchini wametakiwa kuendelea kuishi fadhila za Mtakatifu Monica bila kukata tamaa, na kumshukuru Mungu kwa maisha ya wenzi wao waliotangulia mbele ya haki, bila kusahau kuwaombea hao na watoto waliochwa na wazazi wao kila mara.
Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Kamili, Yombo Kiwalani, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaaam, Padri Germine Laizer, wakati akihubiri katika Adhimisho la MIsa Takatifu ya Somo wa Wajane na Wagane, Mtakatifu Monica, iliyofanyika kwa ngazi ya Jimbo katika Parokia hiyo.
Katika homilia yake, Padri Laizer aliwakumbusha wajane na wagane kutambua maisha ya Mtakatifu Somo wao, Monica, kama mjane aliyeishi katika mateso na maisha mabaya ya mwanae Augustino, lakini licha ya kupitia changamoto hizo, hakukata tamaa hadi mtoto wake alipoongoka, na sasa ni Mtakatifu.
Alisema kwamba pamoja na ujane na ugane wao, ni muhimu kuishi fadhila ya unyenyekevu, kwani ni ishara ya itii mbele ya Mungu na watu, na hasa kila mmoja anapojishusha na kuwa kama mtoto mdogo.
“Maisha yetu yana maana kubwa kila tunapojinyenyekeza na kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani kila mmoja wetu anadaiwa kadri anavyokuwa mkuu kunyenyekea,” alisema Padri Laizer.
Aliongeza kusema kwamba watu wengi walioishii fadhila hiyo ya unyenyekevu wamepata kibali mbele za Mungu, na kujibiwa sala na maombi yao na kumbukumbu lao linaishi hata hivi leo.
“Tabia ya kiburi na majivuno ni kinyume cha unyenyekevu, na mara baada ya mtu kuwa na maisha hayo, hali ya mtu hubadilika na kuharibika kabisa,” alisema Padri Laizer.
Alisema kuwa tukiongozwa na unyenyekevu ni lazima tufike mbali, kwani fadhila hiyo inalipa, na hakuna aliyeishi hali hiyo ambaye hakufanikiwa kamwe.
“Ni wazi unyenyekevu unapokosekana popote, yanatawala mafarakano, uogomvi na majigambo, hali inayotawanya kundi na kupoteza amani na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu,” alisema padri huyo.
Aliwataka waamini kuiga mfano mzuri wa mtu pekee aliyeishi fadhila ya unyenyekevu, ambaye ni Bikira Maria ambapo pamoja na magumu aliyoyapitia, aliyaweka mengi moyoni mwake.
Naye Mwenyekiti wa Wajane na Wagane Jimbo, Sweetbeter Mzungu alimshukuru Paroko wa Parokia hiyo, kwa utayari wake wa kupokea ujio wa sherehe hizo, na kuwapongeza wanachama wote waliojitokeza kufanikisha shughuli hiyo muhimu ambayo hufanyika mara moja kila mwaka.
Sweetbeter alisema kwamba moja ya mafanikio makubwa kwa sasa ni hatua waliopiga kutoka kutambuliwa kama kikundi na kuwa chama cha kitume ingawa bado changamoto kubwa ni mwitikio, hasa wa kupokelewa katika Parokia zote.
Alibainsha kuwa mara nyingi watu wengi hawapendi kujitambulisha kama wajane au wagane, na hali hiyo hutokana na kutokujikubali au kuipokea baada ya kuondokewa na wapendwa wao, na hasa wagane.