Baba Mtakatifu Fransisko (kushoto) akisalimiana na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI wakati Papa alipomtembelea Mstaafu huyo katika makazi yake, akiambatana na Makardinali wapya.
Vatican City
Makardinali Wapya wamemtembelea na kumsalimia Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, katika makazi yake.
Makardinali hao 20 walifanya ziara hiyo ya Kitume, baada ya Ibada ya kutangazwa na kusimikwa, ambapo walikwenda kumsalimia na kumtakia heri Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI.
Mababa Watakatifu hao wawili kwa pamoja baada ya kusalimiana na kuteta na Makardinali hao wapya, waliwabariki ili wakawashe moto wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Baba Mtakatifu Fransisko aliwatangaza na kuwasimika Makardinali wapya na kuwapigia kura Wenyeheri wapya wanaotarajiwa kuingizwa kwenye orodha ya Watakatifu wa Kanisa.
Wenyeheri hao ni Mwenyeheri Padri Giovanni Battista Scalabrini aliyetangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, kuwa Mwenyeheri, Novemba 9, mwaka 1997.
Padre Giovanni Battista alizaliwa Julai 8, mwaka 1839 na kufariki dunia Juni Mosi mwaka 1905.
Alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Piacenza-Bobbio, Italia na Mwanzilishi wa Mashirika ya Wamisionari wa Mtakatifu Carlo Borromeo, maarufu kama Wascalabrini, na pia ni Muasisi wa Taasisi ya Waamini Walei Wascalabrini, iliyoanzishwa kunako mwaka 1961.
Wa pili ni Mwenyeheri Artemide Zatti, Bruda wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco, aliyezaliwa tarehe 12 Oktoba 1880, nchini Italia.
Akafariki dunia Machi 15, mwaka 1951 huko Viedma nchini Argentina.
Utakatifu wake unapata chimbuko lake katika huduma kwa maskini kwa kuongoza hospitali na duka la dawa kwa ajili ya maskini, kwa muda wa miaka 40.
Aprili 14 mwaka 2002, alitangzwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, sasa ni Mtakatifu, kuwa ni Mwenyeheri.