DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Wadau na Watetezi wa Uhai kutoka Shirika la Kutetea Uhai, Pro-Life Tanzaania, wamesema kwamba mengi yaliyoandikwa katika Barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II (Familiaris Consortio 1981) kuhusu Nafasi ya Familia katika Ulimwengu wa leo, hayaonekani katika maisha halisi, kwani dunia ya sasa ni ya kizazi kipya.
Hayo yamejiri katika Kongamano la Shirika hilo liliofanyika Jijini Dar es Salaam, na ambalo lilijadili barua hiyo ya Kichungaji.
Katibu wa Pro-life Tanzania, Godfrey Rahabu Mkaikuta amesema kuwa maisha yamebadilika, hivyo wamefikiri ni vema kupeleka ujumbe wa barua hiyo ya Kichungaji kwa vijana, na hivyo wamelenga kuanza na Vijana katika Vyuo Vikuu.
Alisema pia kuwa mpango huo unakusudiwa kuanza kutekelezwa mapema Januari mwakani katika Vyuo vya Kati, Vidogo na Vyuo Vikuu vya Kanisa Katoliki, na tayari wameshajipanga katika makundi namna ya kufikia Vijana hao katika Vyuo.
Mkutano huo uliokuwa ukijadili Insikliko ya Baba Mtakatifu, ulishirikisha watetezi wa uhai kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda Zambia, Zimbabwe na Rwanda, uliotanguliwa na Misa Takatifu wakati wa ufunguzi iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu.
Askofu Mchamungu aliwapongeza watetezi hao wa uhai kwa juhudi na hamasa kubwa wanayofanya katika kutetea uhai bila kuchoka wala kukatishwa tamaa, na hivyo kuwataka kuendelea na moyo huo bila kuchoka.
Katika mahubiri yake, Askofu Mchamungu alieleza umuhimu wa ndoa na familia katika maisha ya binadamu, kwani familia lazima imsaidie mwanadamu kutambua wito wake mwenyewe, na kuishi kadri ya maongozi ya Mungu.
Kanisa lazima litambue muhimu wa kuweka programu zinazolinda uhai, na kustawisha ndoa na familia kwa ajili ya ustawi wake, na pia ustawi wa taifa kwa ujumla wake.