DAR ES SALAAM
Na Nicolaus Kilowoko
Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars Mecky Mexime amefunguka kuwa kwa sasa Watanzania wanapaswa kuganga yajayo, hasa katika kuwekeza nguvu na mapenzi juu ya timu yao ya Taifa.
Mexime ameyasema hayo mara baada ya Watanzania wengi kusikitishwa na matokeo ya Taifa kushindwa kufurukuta katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki, na kusababisha wengi kuumia.
Mexime alisema kuwa kwenye mpira hakuna kukata tamaa, na matokeo siku zote ni ya pande tatu, hivyo kwa sasa si vyema kulaumu sana, ila ni kuongeza nguvu kwa pamoja kama Watanzania.
Alisema kuwa timu ya Taifa ni ya Watanzania wote, na si ya mtu mmoja. Hivyo, kila jambo linawezekana ikiwa mataifa mengine yanafanikiwa kushiriki mashindano makubwa, hata Tanzania inaweza kushiriki katika mashindano hayo.
“Siku zote kuteleza siyo kuanguka, na hata kama ukianguka, unapaswa kusimama tena. Watanzania wazidi kupenda vya kwao na kuongeza nguvu kwa pamoja katika kuijenga timu yetu, na siyo kulaumu mtu”, alisema Mexime.
Alisema kuwa mchezo wa mpira kwa sasa ni vyema wote kwa pamoja tukatengeneza mkakati wa pamoja ili tuweze kufanya vyema katika michuano inayofuata na inayoshiriki timu hiyo.
Stars ilishindwa kufurukuta katika uwanja wa Benjamin Mkapa wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya wachezaji wanocheza ligi za ndani, CHAN, mbele ya timu ya Taifa ya Uganda kwa kufungwa bao 1-0.
Huu ni mwendelezo wa matokeo mabovu ambayo Stars wameendelea kuyapata baada ya misimu iliyopita kushindwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia, Afcon, Chan pamoja na michezo mbalimbali ya kirafiki.
Meck Maxime anachukua nafasi ya kocha msaidizi mara baada ya kuvunjwa kwa benchi la ufundi la Stars kutokana na matokeo mabovu. Hivyo anaungana kwa sasa na kocha Mkuu, Hanour Janza, akisaidiwa na kocha wa magolikipa, Juma Kaseja.
TFF ilitangaza kukubaliana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Kim Poulsen kumbadirishia majukumu, na sasa atabaki katika timu za vijana za Taifa.
Ikumbukwe kuwa Kim alitangazwa na TFF kuwa Kocha Mkuu wa Stars, Februari 15 mwaka 202, kabla yake aliwahi kuwa kocha wa Stars mwaka 2012 na 2013.
Kim mpaka anawekwa pembeni, amepoteza mechi 7, akipata ushindi kwenye mechi 6, na sare kwenye mechi 4. Alipewa mkataba wa miaka mitatu kuinoa timu ya Stars.