DAR ES SALAAM
Na John Kimweri
Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar Mhashamu Augustine Shao, amesema kuwa mafuta Matakatifu ya Krisma yanamsaidia mtu kuwa shuhuda na mfano mwema wa imani, ndani na nje ya Kanisa.
Askofu Shao aliyasema hayo hivi karibuni wakati akitoa homilia yake kwenye Adhimisho la Misa ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Paulo Mtume, Ubungo Msewe, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Alisema kwamba miongoni mwa alama za nje za Roho Mtakatifu ni mpako wa Krisma Takatifu, ambayo humsaidia mtu aliyeimarishwa kuwa kuhani na shuhuda mwaminifu wa imani ya Kristo.
“Miongoni mwa alama za nje za Roho Mtakatifu ni Krisma Takatifu. Haya mafuta ya Krisma yanakufanya wewe uwe shuhuda na mfano mwema wa Neno, na pia uwe Kuhani wa imani yake Kristo,”alisema Askofu Shao.
Alitaja alama nyingine kuwa ni kofi la upendo, ambalo si kwa ajili ya kumuumiza mtu anayeimarishwa, bali ni kumkomaza kiimani.
Aidha, Askofu Shao alisema kuwa Roho Mtakatifu pia anaweza kuwashukia waimarishwa kwa njia ya kuwekewa mikono.
Kwa mujibu wa Askofu Shao, Roho Mtakatifu anaweza kumshukia mtu yeyote na kumpa maelekezo ya kufanya jambo fulani, kwa manufaa ya watu wengine.
Askofu Shao aliwahimiza vijana walioimarishwa kuisimamia, kuitetea na kuishuhudia imani yao kwa matendo mema, huku akiwasihi wazazi na walezi kuwaombea watoto wao ili wazidi kuimarika.
“Mafundisho ya Kanisa ni kila wakati haya huwa ni endelevu, bado mna safari ya mafundisho zaidi, hasa ya kuilinda na kuitetea imani yenu. Hivyo basi, vijana mnaombwa kuwa mashuhuda wa Injili na matendo mema,”alisema Askofu Shao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Mtakatifu Paulo Mtume, Ubungo Msewe, Bosco Bugali, alisema kuwa Parokia hiyo ilianzishwa mwaka 1973, na imetoa zaidi ya Parokia sita, ila kwa sasa ina Kigango kimoja.
Parokia hiyo ina waamini 2488, Jumuita 39, Kanda Tano na Vyama vya Kitume, vikiwemo Chama cha Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA); Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu;Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA); na Lejio Maria.