DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Waamini wametakiwa kuendelea kujitolea damu bila kuogopa, ili kuokoa maisha ya wengi wenye uhitaji.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na Walezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, walipofanya matendo ya huruma katika Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Ukonga, jijini Dar es Salaam.
“Wanaotoa damu kwa kweli tunawashukuru sana, kwani wanaokoa maisha ya watu wengi. Pengine kuna wengine wanaogopa kutoa damu. Kwa hiyo, naomba msiogope, unapotoa damu ujue kwamba unaokoa maisha ya mtu.
“Siyo kwamba ni wakinamama wanaojifungua ndio tu wanaohitaji kuongezewa damu, lakini kuna wengine pia ambao pengine wamekutwa na upungufu wa damu, wapo wengine waliopata ajali ambayo imesababisha damu nyingi kumwagika, kwa hiyo unapotoa damu, unaokoa maisha ya watu hao,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu Mchamungu aliwahimiza Walezi hao kuendelea kuwalea watoto katika malezi bora, ili liweze kupatikana Taifa lenye kujaliana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Timothy Nyasulu Maganga, aliwashukuru Walezi hao kwa kufanya matendo ya upendo, huku akiwapongeza kwa majitoleo yenye thamani ya Shilingi 10,150,000/=, kwani mwaka jana ilikuwa Shilingi milioni tisa.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Dk. Jane Manyahi, aliwashukuru Walezi hao kwa kufanya matendo ya upendo hospitalini hapo, huku akiwaomba kuwa hayo waliyoyafanya yasiwe mwisho, bali yawe endelevu.
Aliwaomba wale wote wenye vigezo vya kuchangia damu kwenda kufanya hivyo, kwani wakichangia, watapewa kadi maalum za kuwatambulisha kwamba ni wachangiaji, ili na wao au ndugu zao watakapohitaji kuchagiwa damu, waweze kuchangiwa.
Akisoma historia fupi ya Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Katibu wa Hospitali hiyo, Honest Antony alisema kuwa Hospitali hiyo ilianza Mei 22 mwaka 1986 kama Zahanati, wakati huo Kanisa lilikuwa na zahanati nzuri katika maeneo ya Pugu kwenye shule ya Mtakatifu Fransisko, iliyotaifishwa mwaka 1970.
Alisema kuwa Serikali ilitaka pia kuchukua Zahanati hiyo iliyoendeshwa na Masista wa Baldeg. Kardinali Laurean Rugambwa aliyependa kuwa na hospitali ya Jimbo akishauriana na viongozi jimboni, alisisitiza wabadilishane na Zahanati ya Serikali iliyokuwa hapo Ukonga.
“Ukonga palikuwepo tayari Parokia, na Paroko wake Padri Zakeo, Mfransiskani Mkapuchini, alifanya kazi kubwa katika mchakato mzima wa makabidhiano. Bahati nzuri Waamini wa Ukonga walimpenda sana Padri Zakeo, nao wote kupitia Halmashauri ya Walei ya Parokia ya Ukonga, walikuwa nyuma yake katika shughuli nzima, hasa kazi ya kukabidhi umiliki wa viwanja,” alisema Katibu, na kuongeza,
“Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa aliwaomba Masista wa Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu wa Bukoba waje kusimamia zahanati hii ya Ukonga, na Viongozi wao wakakubaliana Septemba 17 mwaka 1984 Shirika liliwatuma Masista wawili wauguzi na wakunga, Sista Ariadina Bijuka na Sista Mechtilda Lwakalema, ambao bado wako hai mpaka leo.”
Katibu alisema kuwa wakati mchakato wa makubaliano na Serikali ukiendelea, Kardinali Laurean Rugambwa alianza kujenga Konventi ya Masista katika kiwanja cha Kanisa Parokiani Ukonga. Baadaye Jimbo Kuu lilipata kiwanja cha zahanati na kujenga nyumba nyingine ya Masista mwaka1995, na konventi ya kwanza ilibadilishwa na kuwa nyumba ya Mapandri.
Alibainisha kuwa mazungumzo juu ya makabidhiano yalikuwa magumu kwa sababu ya uwepo wa wengine ambao walitaka kuchukua zahanti hiyo. Mwadhama Kardinali Laurean Rugambwa ilibidi atie nguvu na ushawishi sana, akisaidiwa na Padre Zakeo na waamini, hasa wa Parokia ya Ukonga.
Alisema kuwa Mei 22 mwaka 1986, Sista Ariadina Bijuka alikabidhiwa uongozi wa zahanati ya Ukonga, akiwa bado mwajiriwa wa Serikali, na wafanyakazi wote wakiwa wa Serikali na Zahanati ikiwa bado serikalini. Wakati huo Zahanati haikuwa na madawa zaidi ya makopo kidogo ya Panadol. Hivyo, Masitsa waliamua kuwalipisha kidogo wateja na kununua dawa pole pole, watu wakaipenda zahanati, na wakaja wingi kutibiwa.
Aliongeza kuwa Machi 14 mwaka 1989, Serikali ilikabidhi jengo la zahanati, vifaa vyote na wafanyakazi kwa Kanisa. Mwadhama Kardinali Rugambwa alimtuma Monsinyori Deogratius Mbiku (hayati), kupokea makabidhiano kwa niaba ya Jimbo.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, mwaka 1997 ilitambuliwa rasmi kama Zahanati ya Huduma ya Uzazi ya Ukonga. Kwa upendo na heshima kwa Mwadhama Kardinali Rugambwa, mashirika ya Ulaya kwa namna ya pekee Misereor, waliendelea kusaidia zahanati hata baada ya Kardinali kuustaafu, kwa mfano mwaka 1996 Padri Stanislaus Kutajwaha alimsindikiza Kardinali Rugambwa kwenda Roma na Aachen Ujerumani, kule alishuhudia jitihada zake katika uzee wake alivyoendelea kupigania Hospitali ya Rugambwa, pale Ukonga.
Anasema, “Shughuli zake huko Aachen zilionyesha wazi kwamba hata katika uzee, tamaa yake Mwadhama ilikuwa bado ni kujaribu kwa uwezo wake wote, kuinua hali ya watu wake kiroho na kimwili.
Wakati huo pia ndoto yake ilikuwa kuboresha makao ya masista wa Shirika Jipya la Masista wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na kupanua Hospitali ya Ukonga kwa ajili ya hudma za afya kwa wananchi.
Alisema pia kuwa mwaka 2001 kituo cha Ukonga kiliweza kutoa huduma za upasuaji, hasa kwa akinamama wajawazito na watoto. Kutoka mwaka 1999 hadi 2008, Shirika la Kiitaliani ola CUAMM likiongozwa na Dkt. Flavio Bobbio lilileta misaada mingi katika Mradi wa Uzazi Salama wakitoa vifaa, dawa, mafunzo, hata na usafiri wa gari ya wagonjwa.
Katibu huyo alisema kuwa kwa sasa wanamshukuru Mungu kwa kuweza kupata cheti rasmi cha kupandishwa ngazi ya Hospitali hiyo hadi kuwa Hospitali ya Mkoa kuanzia Januari 27 mwaka 2022.
“Tunaendelea taratibu katika maboresho mbalimbali ya kukidhi huduma zinazopaswa kutolewa katika Hospitali ya Mkoa. Basi ninyi kama wadau wakubwa wa Kanisa letu Jimboni Dar es Salaam, tunaendelea kuwaomba mtushike mkono ili tuweze kuikamilisha hii kazi iliyopo mbele yetu ya upanuzi wa Hospitali, ili wananchi wote waweze kupata huduma bora kutoka katika hospitali yetu hii,” alisema Katibu.
Aliwashukuru Walezi hao kwa kufika katika hospitali hiyo, huku akiendelea kuwaomba zaidi ufadhili wao ili waendelee kusonga mbele.