Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Ambrosi –IPTL, Salasala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Paul Sabuni akimkabidhi Mwenyekiti mpya wa Parokia Teule ya Utatu Mtakatifu-IPTL, Restituta Mingo, bahasha  za kutegemeza Tumaini Media, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika iliyokwenda sanjali na kuapishwa Viongozi wapya wa Parokia hiyo. (Picha zote na Yohana Kasosi).

Maskofu kutoka Majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa, wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Maaskofu, uliofanyika katika Ukumbi wa AMECEA, Baraza la Maskofu Kurasini (TEC), jijini Dar es Salaam. (Picha na Yohana Kasosi)

MWANZA

Na Paul Mabuga

Upepo unavuma katika jua la saa nane, na miti iliyo karibu inatoa ukinzani,  hali hii inazalisha mvumo ulio sawa na wimbo mzuri unaopigwa kwa ala tupu! Hakika, hali hii ingeweza kuwa ya kufurahisha, lakini la hasha! Aron Malifweda [48], [siyo jina lake halisi kwa sababu za kitaaluma], zaidi ya kutafakari kila swali analoulizwa kwa ajili ya makala haya, huku akiwa ameketi kiambazani kwenye nyumba yake iliyo kwenye moja ya miji mdogo kanda ziwa, ni kama haoni wala kusikia kingine cha ziada katika mazingira yake.
Ni kwa sababu amechanganyikiwa na kuzama katika fikra zisizo na msaada wala  ufumbuzi, anaona ni kama ametengwa na jamii yake kutokana na hali aliyonayo, anachokitamani anaona kama ananyimwa, na hivyo kukata tamaa.
Alitaka awe na  watoto, ikashindikana kwa nguvu za kiume [syo rijali]. Lakini sasa anataka kuasili mtoto anakayerithi mali zake, lakini amepewa sharti, kwamba ni  lazima aoe na kuishi na mke.
“Unajua nimehangaika kwa  miaka mingi, iwe kwa madaktari hospitali, ama tiba asilia, lakini sikufanikiwa. Baadaye daktari mmoja ninayemwamini akaniambia kwamba siwezi kuondokana na hali hiyo nilipata huzuni sana siku hiyo, na nikaona dunia yote imeniangukia.
Nikifikira maisha ya kukaa bila mke wala watoto, nilikiona hata kifo kinaninyemelea! Nimehangaika hivii kwa zaidi ya miaka 15,” anasema Malifwedha, wakati akisimulia kisa chake cha sharti la kuhifadhiwa utambulisho.
Anasema kuwa kama suluhisho katika hilo, alishauriwa na daktari huyo kwamba atafute mtoto wa kuasili ndiye atakayekuwa  mrithi wa mali zake, jambo ambalo anaeleza kuwa  awali lilikuwa gumu, kwani wapo waliomkatisha tamaa kwa kumtishia kuwa anaweza kupata kijana, akamlea, lakini baadaye atakapokua, asimjali na kumkimbia akirejea katika familia yake ya uzao wa kibayolojia.
“Walikuwa wananiambia, Unaweza kupata mtoto wa kuasili na kumsomesha, lakini akifika chuo kikuu, akakukumbia na kukutelekeza,” anasimulia Malifwedha na kuongeza kuwa, “Baada ya ushauri wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika eneo langu, nilipata moyo wa kuanza mchakato wa kupata mtoto wa kuasili, ambao. Licha ya jambo kwenda vyema, lakini sasa nimefikia pahala umekwama kutokana na sharti nililopewa, kwamba ni lazima nioe!”
Kwa mujibu wa Tovuti ya Wakala wa Uzazi na Vifo, kuasili watoto ni mchakato wa kisheria ambao huhamisha uwajibikaji wa mzazi kutoka kwa wazazi wa kuzaliwa kwa watoto, kwenda kwa wazazi  wa kuwalea. Kuasili mtoto kunaongozwa na sheria  ya kuasili mtoto, Sura Namba 335 Toleo la Mwaka 2002.
Na kwa mujibu wa sheria hiyo, mara mtoto anapoasiliwa, basi unajengwa uhusiano wa kudumu na wa moja kwa maoja kati yake na wazazi waliomuasili, na kwamba haki zote kutoka kwa wazazi wake wa kibayolojia [wa damu] zinafutika na kuhamia katika familia yake mpya. Pia, Wazazi wa damu nao haki zao kwa mtoto aliyeailiwa, nazo zinakoma.
Tukirejea kwa Malifedha, anaeleza kuwa baada ya kupata mtoto wa kuasili, na wazazi wake wa damu kutoa ridhaa chini ya usimamizi wa Maafisa Ustawi wa Jamii, na uchumguzi wa kina kufanyika katika kipindi cha miezi sita, alijaza fomu mbali mbali na taarifa za ufuatiliaji zikaandikwa, tena zikionesha kwamba ana mwenendo mzuri, na ana uwezo wa kuasili.
Bila shaka mchakato kama huu, kulingana na taratibu, baadaye ulihitaji idhinisho la mamlaka ya juu ya Ustawi wa Jamii. Kutoka hapo, hoja hupelekwa mahakamani mbele ya jaji, na  kama kutakuwa na kukidhi matakwa ya kisheria, basi, hutolewa amri ya kuasili, na mchakato huwa umekamilika. Hata hivyo, katika muda wote Maafisa Ustawi wa Jamii huendelea kufuatilia ustawi na maslahi ya mtoto.
Pengine kilichoonekana kuwa ni kikwazo kwa Malifwedha kwa mujibu wa sheria hiyo, ni kwamba mzazi wa kiume anayeishi pake yake haruhusiwi kumuasili mtoto wa kike, ama vingunevyo kuwe na mazingira mahsusi! Ingawaje hata huvyo  anaruhusiwa kuasili mtoto wake wa kiume. Na pia, kuwe na tofauti ya umri wa miaka  isiyopungua 21 kati ya mzazi anayeasili, na mtoto anayeasiliwa.
Tena basi, inaelekezwa katika kanuni za sheria hiyo kwamba katika mazingita yanayofaa, mtoto aliyeasiliwa, atakapofikisha umri wa miaka 14, ataelezwa hali ya kuasiliwa kwake na maafisa ustawi wa jamii katika eneo husika.
Kuhusu suala na kuoa Malifwedha anasema, “Nilikwenda kwa wanasheria, wakaniambia kuwa huyo mwanamke nikimuoa, atakuwa na haki zote kama mke kwenye mali zangu, hata kama itakuwa ni ndoa ya kudanganyia ili tu nipate kibali cha kuasili! Hilo nalo nkaliona gumu. Nikashauriwa niende kwa Wakurya,  eti huko ukioa mwanamke aliyezalia nyumbani, na ukishatioa mahari, watoto wanakuwa mali yako.”
Sadick Hunga ambaye ni Mwandishi wa Habari anayefanya kazi zake Mkoani Mara, na ambaye ni mmoja wa wanajumuia ya Wakurya wanaoishi Mkoani humo,  anasema katika mahojiano kwa njia ya simu kwamba, mila hiyo ipo katika jamii yake na imeendelea kuwepo, kwamba katika jamii hiyo, wakati wote watoto huwa ni mali ya mwanaume aliyelipa mahari.
“Huyu jamaa sisi tunamuambia karibu ‘tata’ [baba]! Yaani huku kwetu, kama mwanamke amezalia nyumbani, akaja mwanaume kumuoa, analipa mahali ya mke, mathalani ng’ombe sita, lakini baadaye atatakuwa kuwalipia watoto mahari nyingine inayoitwa ‘kuborora’, ambayo inaweza kufikia hadi ng’ombe wawili kwa kila mtoto, na kutokea hapo watoto hao wanakuwa mali yake daima dumu, hata wana umri mkubwa namna gani,” anasema Hunga.
Katika mtazamo mwingine Hunga anasema kuwa miongoni mwa jamii ya Wakurya, ikiwa mwanamke ameachana na mume wake, na  ikatokea akaolewa na mwanaume mwingine, basi, watoto wote watakaozaliwa katika familia mpya ni mali ya yule mume wa awali, “na hii imetokea majuzi huko Serengeti! Itaondoka tu ikiwa mume mpya atalipa mahari kurejesha iliyokwishakulipwa kabla.”
Wakati hali ikiwa hivi, Malifwedha bado yupo njia panda juu ya nini akifanye ili kukabiliana na hali hii, kwani ana malalamikio mengine. Anadai kwamba ndugu zake wanamtenga na hususan yanapokuja matukio kama harusi huwa hashirikishwi, na hilo linamuongezea mawazo! “Yaani utasikia tu kuna harusi huko, lakini hushirikishwi, huwa najiuliza, sijui wananionaje,” anasema.
Kuna changamoto nyingine pia, kwani Malifwedha akifikisha umri wa miaka 50, yaani katika kipindi cha miaka miwili ijayo, kwani suala la kuasili litakuwa na kipingamizi, kwani halitakuwa katika maslahi ya mtoto, na hususani katika maendeleo na makuzi yake. Na itakuwa ni kazi kubwa kujenga hoja dhidi ya pingamizi kama hizi kulingana na kanuni za kuasili.
Mrumbi wa masuala ya ndoa na muendeshaji wa kipindi cha ‘Ndoa Aminifu’ cha Runinga ya Tumaini, Paschal Maziku, anasema kwamba ndoa katika Kanisa Katoliki huwa ni kwa ajili ya manufaa ya wanandoa wenyewe, watoto wanaowalea na jamii kwa ujumla, na wala siyo kwa manufaa binafsi kama ilivyo katika jambo hili katika makala haya.
“Isitoshe, huyu bwana hawezi kuwa na ndoa, kwani ndoa huwa kati ya mwanamke na mwanaume rijali. Sasa jamaa na hali aliyonayo, haiwezekani, maana ndoa ili  ikamilike inahitaji kuwa ‘consummated’ [tendo la ndoa kufanyika ndani ya muda unaovumilia kwa busara ana kupatilizwa], kinyume na hapo inavunjwa”
Kuhusu, kuasili watoto, Maziku anasema, huko ni sawa na mtoto kuwa ‘displaced’ [kuwa pasipostahili],  na kwamba, “ni vema tukarejea katika mila zetu, kama ni yatima ama ana mazingira magumu, basi ndugu wa karibu, wajomba, mathalani baba wadogo na wengine, wachukue majukumu yao.”

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliawaletea mada ya historia ya jinsi Uinjilishaji ulivyoingia nchi za Ethiopia, Eritrea na Somalia. Leo tunaendelea na historia ya Uinjilishaji katika nchi za Maghreb.. Sasa endelea…

Katika Kiarabu, nchi za Magharibi mwa Misri huitwa ‘Maghreb’. Nchi hizi ni pamoja na Libya, Tunisia, Algeria na Morroco. Zamani nchi hizi, hasa kwenye mwambao, zilikuwa za Kikristu hadi zilipotekwa na Waislamu katika karne ya saba. Pole pole Ukristo uligandamizwa na kupotea.
Ufaransa iliteka Algiers mwaka 1830 na kufanya Algeria nzima koloni lake, baadaye waliteka Tunisia mwaka 1881 na Morocco mwaka 1912. Libya ilitekwa na Waitaliani mwaka 1912 na kuipoteza kwa Waigereza wakati wa Vita Vikuu vya Pili, mwaka 1942.
Wakati wa ukoloni, Wakristo walikuwa na uhuru wa kuinjilisha, na waliongezeka hadi kufikia milioni moja na nusu. Hata hivyo, hawakuwa na mafanikio makubwa kati ya Waarabu Waislamu. Wengi wa waumini wao walikuwa Wazungu waliohamia kule.
Waarabu walioongoka hawakuzidi 10,000. Utume katika nchi hizo ulifanywa hasa na Wamisionari wa Afrika (Mapadre Weupe) waliokuwa na Makao Makuu yao kule Algiers, Algeria.
Utume wao mkubwa ulikuwa utume wa kuwepo kwa kuonyesha mfano na kufanya matendo mema. Walianzisha vyuo vya kujifunza lugha ya Kiarabu na Uislamu kwa wageni.
Mmisionari mwingine alikuwa Charles de Foucard aliyeanzisha Mabruda na Masista Wadogo wa Yesu. Wao wanajaribu kuishi katikati ya watu na kufanya kazi pamoja nao katika viwanda na sehemu nyingine.
Nchi za Maghreb zilipopata uhuru wake, Wazungu karibu wote bila kungoja kufukuzwa, walirudi Ulaya. Kadri siku zilivyopita, nchi hizi ziliweka sheria ngumu ya kuwabana Wakristo, na hivyo hata Wakristo Waarabu walikimbilia Ulaya na kufanya kazi huko. Hivyo katika nchi za Maghreb hadi leo, Ukristo ni kama haupo.
MOROCCO
Morocco ilipata uhuru wake bila matatizo mwaka 1956. Ingawa iliwekwa sheria ya kukataza Waislamu kuongoka kuwa Wakristo, uhusiano na Kanisa ulibaki mzuri. Tangu mwaka 1952 kuna monasteri ya Wabenediktini inayoendesha semina hasa juu ya Mahusiano ya Dini mbalimbali. Kati ya wakazi milioni 31, Wakristo ni asilimia 0.5, na Wakatoliki ni asilimia 0.2 tu.
ALGERIA
Algeria ilipata uhuru wake mwaka 1962 baada ya vita vikali vilivyodumu miaka 8. Kwa sababu wakati wa vita, Askofu Mkatoliki Etienne Duval alitetea haki za wazawa, baada ya uhuru Kanisa liliheshimiwa.
Hata hivyo, Wakatoliki 800,000 waliondoka wakabaki 80,000 tu. Ila, Mapadre na Watawa walibaki kuwahudumia watu bila ubaguzi. Kati ya wakazi milioni 34, Wakristo ni asilimia 0.9 na Wakatoliki ni asilimia 0.6 tu. Kuna majimbo manne, Mapadre 62 na Watawa wanawake 116.
TUNISIA
Tunisia ilipopata uhuru mwaka 1956, kwa makubaliano kati ya serikali ya Kiislamu na Wamisionari wa Afrika, alama na mambo mengi ya Kikristo katika mji wa Tunis yaliondolewa.
Kwa mfano, sanamu ya mwanzilishi wa shirika iliyokuwa katikati ya mji, ilipelekwa makaburini, Cathedral nzuri ilifanywa makumbusho, kati ya makanisa sabini, sitini na tano yalipewa kwa serikali kwa matumizi ya umma, hata na cheo cha Askofu Mkuu cha Kartago kilishushwa na kuwa Usimamizi wa Kitume.
Hata hivyo, waliimarisha urafiki na Rais wa Tunisia, Bourguiba, ambaye alianzisha uhusiano wa kibalozi na Vatikano. Wamisionari walibaki na chuo chao cha kufundisha Kiarabu kilicholeta mahusiano mazuri. Kati ya wakazi milioni 10, Wakristo ni asilimia 0.3 na Wakatoliki ni asilimia 0.2 tu. Mwaka 1996 Papa Yohane Paulo II (1978-2005), alitembelea Tunisia kuwatia moyo.
LIBYA
Libya ilipata uhuru wake mwaka 1951 kutoka kwa Waitaliani. Baada ya uhuru, idadi ya Wakatoliki ilishuka hadi kubakia 5,000 tu, na baadaye Wamisionari walifukuzwa, Wakopti nao walibakia wachache.
Baada ya mapinduzi ya Kanali Ghadafi, katika makubaliano na Vatikano, Kanisa lilibakiza kanisa moja tu kule Tripoli. Ila baadaye Gadafi aliwaalika Masista manesi kwenda kusaidia watu wake. Hata Masista Watanzania wa Shirika la Konsolata walikwenda huko. Kati ya wakazi milioni 5.4, Wakristo ni asilimia 2.1,   na Wakatoliki ni asilimia 0.3 tu.
Ingawa katika nchi nyingi za Maghreb kuna uhusiano wa kidiplomasia na Vatikano, hakuna uhuru wa kuabudu. Haiwezekani kujenga kanisa au kuhubiri dini kwa Waarabu Waislamu. Kwa Mwarabu kuongoka na kuwa Mkristo, ni kosa linaloadhibiwa kisheria, mahali pengine hata kuuawa.

Vijana waimarishwa wa Parokia ya Mtakatifu Clara –Magole, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakitoka kanisani baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya kupokea Kipaimara.

Kwaya ya Parokia Teule ya Utatu Mtakatifu, Skanska -IPTL, Salasala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakiimba wakati wa Adhimisho ya Misa Takatifu ya Dominika.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Ambosi –IPTL, Salasala, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Paul Sabuni akiwaapisha Viongozi wapya wa Parokia Teule ya Utatu Mtakatifu, Skanska -IPTL, baada ya kupandishwa hadhi Parokia hiyo.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akipokea akipokea sadaka kutoka kwa Waamini na Viongozi wa  Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Clara –Magole Jimboni humo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi na Mapadri wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kamati Tendaji ya Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza, jimboni humo. (Picha zote na Yohana Kasosi).

DAR ES SALAAM

Na Pd. Dkt. Clement Kihiyo (TEC)

Mwaka wa Liturujia Leo ya Wokovu
1. Utangulizi:
Ishara na matendo yanayofanywa kwa wakati huwa njia ya wokovu kwetu. Mwaka wa Liturujia ambao pia huitwa mwaka wa Kanisa ni fumbo la Kristo. Ni kwa njia ya maadhimisho ya kumbukumbu takatifu ndani ya Mwaka wa Liturujia, ndipo tunapata wokovu. Katika Mwaka wa Liturujia, Fumbo zima la Kristo linafunuliwa; yaani, kutoka Umwilisho na kuzaliwa, na kutoka Kupaa hadi Pentekoste
Mama Kanisa Takatifu huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu kazi ya ukombozi ya Bwanaarusi wake aliye Mungu, katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima. Kila juma, Kanisa katika siku aliyoiita “Dominika”, yaani “Siku ya Bwana”, linaadhimisha kumbukumbu ya ufufuko wa Bwana. Kwa namna ya pekee, linauadhimisha ufufuko huo pamoja na mateso yake yenye heri mara moja kwa mwaka katika Sikukuu ya Pasaka, iliyo kubwa kuliko maadhimisho yoyote (SC 102).
Katika mzunguko wa mwaka mzima, Mama Kanisa analikunjua fumbo la Kristo, tangu umwilisho na kuzaliwa, hadi kupaa mbinguni, mpaka siku ya Pentekoste na kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake Bwana. Anapokumbuka namna hii mafumbo ya ukombozi, Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake. Kwa njia hii, uwepo wa mafumbo haya unakuwapo kwa nyakati zote, ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu.
Mwaka wa Liturujia pia unawakilisha na kueneza tena  imani, maisha ya Kikristo na uwepo wa ukombozi wa Kristo na utajiri wa wokovu (SC. 102c). Mwaka wa Liturujia ni safari ya wokovu wa Kristo Mwenyewe na Kanisa lake (Lk, 24:15). Mwaka wa Liturujia sio mfuatano wa jumla wa siku na miezi, lakini unakuwa alama/ishara ya mfuatano ambao matukio ya neema yanatokea kama matukio ya wokovu kwetu hapa leo. Mwaka wa Liturujia ni wakati wa wokovu, ‘epifania’ ‘hic et nunc’ (hapa na sasa) kwetu.

2. Baadhi ya Mambo Makuu ya Mwaka wa Liturujia
2.1 Mwaka wa Liturujia ni Maadhimisho:
Matukio ya Mwaka wa Liturujia sio tu mifano ya kutafakari au kuiga uungu, lakini ni ishara zenye ufanisi za wokovu, ambao Kristo katika Utatu Mtakatifu, wamekamilisha kwa wokovu wa wanadamu. Mambo makuu ya ukombozi ni sisi kuadhimisha na kurithisha kwa kizazi kingine. Mwaka wa Liturujia una nguvu maalum ya kisakramenti na ufanisi wa kuimarisha maisha ya Kikristo.

2.2 Mwaka wa Liturujia Kuanzia Ufufuko:
Tukianzia na habari ya wanafunzi wa Emao (Lk 24:25-26); Yesu alieleza kisa chote kuanzia Ufufuko hadi Manabii. Ina maana kila kitu kinamhusu Kristo. “Bila ufufuko imani yetu haina maana” (1Kor. 15:13-17). Ufufuko ni chanzo na kitovu cha Mwaka wa Liturujia. Ufufuko ni siku ya Adamu Mpya (Rum. 11:5, Efe 2:5,8).
2.3 Siku ya Kwanza ya Juma-Dominika- Siku ya Bwana
Tangazo la ufufuko lilianza siku hii kwa amri ya Bwana (Mk.16.7, Mt. 28.7, Lk. 24.9). Ndipo wale wanawake wakatangaza ufufuko siku ile ile. Kwa hiyo, Dominika ni mwendelezo wa tangazo la Ufufuko. “Tunasherehekea Dominika kwa sababu ya Ufufuko Mtukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo, na tunafanya hivyo sio tu wakati wa Pasaka bali pia kila mzunguko wa juma, yaani kila Siku ya Kwanza ya Juma. Mtakatifu Augustino anaiita Dominika kwa usahihi kama Sakramenti ya Pasaka  (Taz . In Io. Tract . XX, 202: CCL 36,203), (SC 26, 184). Kwa Kanisa la Mashariki Dominika ni ‘Anastasimos hemera’, yaani, siku ya ufufuko.
Matendo ya kiliturujia si matendo ya kila mmoja peke yake, bali ni maadhimisho ya Kanisa, ambalo ni “sakramenti ya umoja”, yaani taifa takatifu linalokusanywa na kuratibishwa chini ya uongozi wa Maaskofu SC 26.
Kwa sababu hiyo matendo hayo ni ya mwili wote kabisa wa Kanisa, nayo huudhihirisha na kuuimarisha. Aidha, kila mmoja wa wanakanisa anahusika kwa namna tofauti, kadiri ya utofauti wa daraja, wa majukumu, na wa ushiriki kiutendaji
Matukio maalum ya kimungu siku ya Dominika pia yanaipa siku hii umaalumu wake. Maana yake:

i.    Roho Mtakatifu alitolewa kwa Wanafunzi siku ya Dominika (Pokeeni Roho Mtakatifu, wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa),
ii.    Pentekoste ilikuwa siku ya Dominika,
iii.    Dominika ni siku ya Amani, siku ya Yubilei ya Roho Mtakatifu (Lk 4:18-19, Isa 61:1-3).
iv.    Kwa namna ya pekee, Dominika ni siku ya uumbaji mpya, siku ya Jua Jipya (Mal, 4:2).

2.4 Dominika ni Kitovu na Kiini cha Mwaka wa Liturujia:
Dominika ni Kitovu na Kiini cha Mwaka wa Liturujia kwa muktadha ufuatao:
Dominika ni siku ya Bwana. Wayunani wanaiita, “Kyriake Hemera”, ambapo kivumishi ‘Kyriake’ kinarejelea Kyrios, yaani Bwana aliyefufuka pamoja na Roho (1 Kor. 16:2, Mdo, 20:7, Ufu.1.10).
Dominika ni siku ya kimungu ya kumwadhimisha Bwana, siku kwa ajili ya kumega mkate na Neno, siku kwa ajili ya karamu na kwa ajili ya kukusanya sadaka kwa ajili ya maskini (2 Kor, 9:12, Rum. 15:27).
Dominika ni siku ya mwanzo wa uumbaji, ni siku ya nane baada ya ufufuko. Ni siku ya nane kwa sababu ni nje ya muda unaopimwa katika wiki. Siku ya nane ni siku ya Ekaristi. Hivyo, Dominika hugusa fumbo zima la wokovu. Inaleta pamoja na yenyewe ulimwengu wote wa mfano wa Kikristo. Inaangazia siku ya mwisho, siku ya Parousia.
Kwa hiyo, Dominika ni siku maalum na siku pekee  ya Bwana. Inaunda mwendelezo halisi wa adhimisho wa Kanisa kutoka Pentekoste hadi kurudi kwa Bwana. Maadhimisho mengine, isipokuwa kama yana umuhimu mkubwa, hayatapewa kipaumbele kuliko Dominika ambayo ndiyo msingi wa kweli na kiini cha Mwaka mzima wa Liturujia.
Kadri ya mapokeo ya Mitume, yanayopata asili yake katika siku ya ufufuko wa Kristo, Kanisa huadhimisha fumbo la Pasaka kila siku ya nane, katika siku ile iitwayo kwa haki kabisa Siku ya Bwana au Dominika. Katika siku hii Waamini wanapaswa kujumuika pamoja ili, wanaposikiliza Neno la Mungu na kushiriki Ekaristi, wafanye ukumbusho wa mateso, ufufuko na utukufu wa Bwana Yesu. Na pia watoe shukrani kwa Mungu “aliyewazaa upya katika tumaini lenye uhai kwa njia ya ufufuko wa Yesu Kristo katika wafu” (1Pet, 1:3). Kwa hiyo, siku ya Dominika ni Sikukuu ya kwanza ambayo ni lazima ielezwe vizuri na kuingizwa, kwa kadri inavyowezekana, katika maisha ya kidini ya Wakristo, ili iweze kuwa pia siku ya furaha na ya kuacha kazi. Maadhimisho mengine yasitiliwe mkazo sana, isipokuwa yale yenye umuhimu zaidi, kwa sababu siku ya Dominika ni msingi na kiini cha mwaka mzima wa Liturujia (SC. 106).

3. Fumbo na Mafumbo ya Kristo:
Imani ya Kikristo inaadhimisha Fumbo Kuu Moja la Pasaka, nalo ni  Fumbo la Kristo, aliyeteswa, akafa, akazikwa na kufufuka. Kanisa linaendelea kuadhimisha Fumbo hili kwa njia tofauti. Fumbo hili lilianza kufunuliwa katika Agano la Kale; na linatimizwa kihistoria katika maisha ya kidunia ya Kristo, na lipo katika mafumbo ya kisakramenti.
Fumbo la Pasaka huadhimishwa katika mwaka kwa njia tofauti, lakini katika utaratibu ule ule wa Neno, mwili na kikombe cha Yesu Kristo. Awamu tofauti za maadhimisho zinalenga kutufanya tuelewe vizuri Fumbo hilo. Katika uwezo wetu mdogo wa kibinadamu na kisaikolojia, hatuwezi kulielewa na kuliadhimisha hilo Fumbo kwa wakati mmoja na kuchota utajiri wa neema ya Fumbo hilo la Kristo”, kwa hivyo, Mwaka wa Liturujia unatupa muda wa kutosha wa kuliadhimisha na kuchota neema zake.
Kwa muktadha huu, katika kila Misa kuna Majilio, Noeli, Epifania, Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu, Pentekoste, Pasaka, Kupaa, na Watakatifu wote. Kwa hiyo, Mwaka mzima wa Kanisa ni Fumbo Moja, “ Sakramenti Paschale ” ambalo huadhimishwa kila Dominika.
Kutoka hili Fumbo Kubwa la Pasaka, linajigawa katika mafumbo kadhaa yanayorejelea matukio tofauti katika maisha ya Kristo, na ni ushiriki na ukuzaji wa Fumbo moja pekee la Pasaka, ambalo huanza kutoka Usiku Mtakatifu wa Ufufuo hadi wakati wa Pasaka hadi Pentekoste, Wiki Takatifu, Kwaresima, Wakati wa Kawaida, Majilio, Noeli hadi Epifania na Sikukuu mbalimbali.
Itaendelea toleo lijalo.

Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha