VATICAN CITY, Vatican
Baba Mtakatifu Fransisko ametaka kuwepo kwa hatua za kusitisha mapigano mara moja huko Lebanon, Gaza, Palestina, Israel na maeneo mengine kama Ukraine, Sudan na Myanmar.
Katika Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi, Papa alisema kwamba hali ya uhamaji ni fursa ya kukua kwa udugu, akitoa tangazo la ufunguzi wa mchakato wa kumtangaza Mfalme Baudouin kuwa mwenyeheri.
Baada ya Misa hiyo Takatifu iliyoongozwa na Papa Fransisko katika Uwanja wa Mfalme Baudouin huko Bruxelles, alitoa shukrani kwa Maaskofu nchini Ubelgiji kwa maneno mazuri, akisema “Ninatoa shukrani za dhati kwa Wakuu, Mfalme na Malkia, na vile vile Wakuu wa Kifalme, Mtawala Mkuu na Malkia wa Luxembourg, kwa uwepo wao na ukarimu wao katika siku hizi.
Vile vile, ninatoa shukrani zangu kwa wote ambao, kwa njia nyingi, mmefanya kazi pamoja kuandaa Ziara hii. Kwa namna ya pekee, ninawashukuru wazee na wagonjwa ambao wamesali sala zao.”
“Leo tunaadhimisha Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani yenye mada “Mungu anatembea na watu wake”. Kutoka nchi hii ya Ubelgiji, ambayo imekuwa, na bado ni kivutio cha wahamiaji wengi, ninarudia wito wangu kwa Ulaya na Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia hali ya uhamiaji kama fursa ya kukua pamoja katika udugu, na ninakaribisha kila mtu kuona katika kila jambo kaka na dada mhamiaji uso wa Yesu, ambaye alifanyika mgeni na msafiri kati yetu,” alisema Baba Mtakatifu.
Papa alibainisha kwamba anaendelea kufuatilia kwa uchungu na wasiwasi mkubwa upanuzi na kuimarika kwa mzozo nchini Lebanon, akisema kwamba Lebanon ni ujumbe, lakini kwa sasa ni ujumbe wa kuteswa na vita, hivyo ambavyo vina madhara makubwa kwa idadi ya watu, kwani wengi wanaendelea kufa, siku baada ya siku, katika Mashariki ya Kati.
Aliongeza kwamba wanawaombea wahanga pamoja na familia zao, akitoa wito kwa pande zote kukomesha moto mara moja huko Lebanon na Gaza, pamoja na maeneo mengine ya Palestina na Israeli.
“Pia, ninawashukuru wengi wenu mliokuja kutoka Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa kushiriki siku hii, asanteni.
Kwa wakati huu, pia ningependa kukupatia habari fulani. Nikirudi Roma nitaanza mchakato wa kutangazwa Mwenyeheri kwa Mfalme Baudouin, mfano wake kama mtu wa imani uwaangazie watawala. Ninaomba Maaskofu wa Ubelgiji wajitolee katika kuendeleza jambo hili,” alisema Papa.
Sambamba na hayo, aliomba kumgeukia Bikira Maria wakati wa kusali Sala ya Malaika wa Bwana pamoja, akisema kuwa hayo yalikuwa maombi maarufu sana katika vizazi vilivyopita, na hivyo napaswa kuhuishwa kwa kuwa ni muunganisho wa fumbo la Kikristo, na Kanisa linatufundisha kulijumuisha katika shughuli za kila siku.
Baada ya Adhimisho hilo la Misa Takatifu, Askofu Mkuu Luc Terlinden wa Jimbo Kuu Katoliki la Malines -Bruxelles, alishukuru kwa niaba ya Maaskofu wenzake, pamoja na Waamini wa Kanisa nchini Ubelgiji kwa ziara yake nchini.
Alimshukuru Baba Mtakatifu Fransisko kwa kwenda kukutana na wazalendo na wahusika, na kwa namna ya pekee wale walioko kwenye matatizo, pamoja na wenye majeraha ya kina yanayotokana na manyanyaso.
Aidha, alimshukuru Baba Mtakatifu kwa kuingia katika mazungumza na wanafunzi, watafiti na wanafunzi katika fursa ya miaka 600 ya Chuo Kikuu dada cha KULeuven na UCLouvain, na kwamba Papa anawafundisha wasitengenishe utafutaji wa ukweli, hekima na haki kijamii.
“Hekima inaweza kusaidia hadhi ya mtu binadamu, na kwa namna ya pekee katika Siku ya 110 ya Dunia ambayo imewekwa kwa ajili ya Wahamiaji na Wakimbizi, na inasaidia hata kulinda sayari yetu, “nyumba yetu ya pamoja,” alisisitiza, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Bruxelles.
Alisema kwamba wanaamini katika salamu za Baba Mtakatifu za wema, na kubainisha kwamba katika sala zao kwa ajili yake na kwa huduma yake, wanaikabidhi kwa Mama, Kikao cha Hekima na Mwenyeheri Anna wa Yesu.