TAFAKURI YA SOMO LA INJILI DOMINIKA YA 12 MWAKA B
Na Pd. Gaston George Mkude
Amani na Salama!
Baadhi ya miujiza inayosimuliwa katika Maandiko Matakatifu, inatuacha na mshangao mkubwa: Mti uliolaaniwa kwa kukosa kutoa matunda wakati si majira yake (Marko, 11:13), maji yanageuzwa kuwa divai (Yohane, 2:1-11), Yesu akitembea juu ya maji, na Petro akimwomba naye atembee juu ya maji (Matayo, 14:22-33), Petro analipa zaka ya hekalu kwa kupata pesa kutoka kinywa cha samaki (Matayo 17:24-27). Hivyo, ili kupata ujumbe kutoka miujiza ya namna hii, hatuna budi kuingia ndani kabisa bila kuishia katika miujiza pekee.
Muujiza wa leo pia ambapo Yesu anatuliza dhoruba ya upepo mkubwa baharini, ni moja ya miujiza inayotutaka kutafakari zaidi ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa. Baada ya kulisoma somo la Injili ya leo, mara moja tunaweza kuwa na maswali kadhaa.
Mwinjili anatuambia kuwa ilikuwa jioni, na kama ni jioni iliwapasa kurejea nyumbani Kapernaumu, na siyo kuvuka na kwenda upande mwingine, maana bado swali kwa nini muda ule walivuka kwenda upande mwingine? Na zaidi sana, kwa nini walienda upande wa Wagerasi, watu waliokuwa wapagani na wasiochangamana na Wayahudi? Na hata tukisoma zaidi Injili ya Marko, tunaona kuwa Yesu hakupokelewa wala kufahamika vyema katika nchi ile ya Wagerasi. (Marko, 5:17)
Na hata wafuasi wake wanaomwamsha ili awaokoe katika hatari ile ya dhoruba kubwa, na wanafanya hilo, kwani waliamini katika uwezo wa Yesu, lakini Yesu anawakemea kwa kuwa hawana imani. Pia, hata baada ya Yesu kuituliza dhoruba ile kubwa, tunashangaa kuona wanafunzi wake, badala ya kufurahi, wamejawa na uoga na hofu kuu.
Ni kwa msaada wa maswali haya ndipo tunaweza sasa kuona somo la Injili la leo linatualika kwenda ndani zaidi ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa. Si nia wala lengo la Mwinjili Marko kutupa simulizi tu la muujiza alioufanya Yesu wa kuituliza dhoruba, bali tangu mwanzo tunaona ni nia ya Mwinjili Marko kutusaidia hatua kwa hatua katika kumtambua Yesu ni nani, utambulisho wa Kimasiha unaojifunua hatua kwa hatua.
Hivyo, masimulizi na nia kuu ya Mwinjili Marko ni kumtambulisha Yesu kwetu, kwa kila mmoja anayetaka kukutana na kumjua Masiha, basi Injili ya Marko ni msaada mkubwa kwetu. Ni Injili ambayo tangu mwanzoni inajaribu kujibu swali lile la; Yesu ni nani.
Leo tunakutana na chombo kikiwa baharini pamoja na vyombo vingine, zaidi sana pia chombo hiki kikielekea katika nchi ya wapagani, yaani Wagerasi, mawimbi makali na makubwa, giza la usiku, maana ilikuwa jioni, Yesu amelala katika shetri na juu ya mto, upepo mkali, hofu na uoga uliowajaa wafuasi wa Yesu, ni moja kati ya lugha ya picha tunazokutana nazo mara nyingi katika Maandiko Matakatifu.
Injili yetu ya leo inaanza na kutuambia muda wa muujiza ndio jioni, na uelekeo wa chombo kile alimokuwemo Yesu na wanafunzi wake.
Ni jioni. Ndiyo kusema ni baada ya Yesu kumaliza utume na misheni yake ya kuusimika na kuutangaza Ufalme wa Mungu, wanafunzi wake wanaingia chomboni pamoja na Yesu na kuelekea upande mwingine, lakini wanakwenda wapi haswa?
Ni baada ya kusoma zaidi Injili ya Marko, kwamba walikuwa wanaelekea katika nchi ile ya Wagerasi, waliokuwa wapagani. (Marko 5:1) Na ndipo tunaona mara moja kuwa katika nchi ile kulikuwepo na nguruwe malishoni mlimani, ambapo Yesu baada ya kumponya mtu aliyekuwa na pepo wachafu, pepo wale wakamwomba Yesu, kutoka na kuwaingia nguruwe, na hata nguruwe wale wakaishia wote baharini. Uwepo wa nguruwe kati yao ni ishara tosha kuwa watu wale hawakuwa Wayahudi, bali wapagani, kwani Wayahudi ni marufuku kufuga au kula nyama ya nguruwe.
Chombo ndiyo ishara ya jumuiya ya Wakristo yaani Kanisa lake Yesu Kristo, ambao baada ya Yesu kukamilisha utume na misheni yake, wanaalikwa kutoka na kwenda kuitangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote. Lakini tunaona chomboni lazima pia awepo na Yesu, kwani uwepo wake ni wa lazima na wa muhimu kwa usalama wa jumuiya ya Kanisa. Tunaona leo chombo kikiwa katikati ya safari, kinakuwa katika hatari kubwa kwa upepo mkubwa na dhoruba.
Mwinjili Marko anatuambia pia kwamba kulikuwa na vyombo vingine, ndiyo kusema Mwinjili anajaribu kutuonesha kuwa hata baada ya utume wa Yesu Kristo kukamilika hapa duniani, kulikuwa na jumuiya kadhaa za Kikristo katika Kanisa lile la mwanzo.
Ilikuwa jioni, ndiyo kusema ilikuwa giza. Giza katika Maandiko ni ishara hasi, ni kukosekana utaratibu kama ilivyokuwa mwanzo kabla ya uuumbaji. (Tohuwabohu - Mwanzo, 1 :2). Fujo ni kukosekana uwepo, na hasa uweza wake Mwenyezi Mungu.
Ni hapo katika uwepo wa giza tunaona yule mwovu anatawala, na hivyo tunahitaji uwepo wake Mungu ili kututoa na kutuacha salama katika mitego ya yule mwovu. Chombo kinasafiri saa ile ya giza, saa ile ya fujo, saa isiyokuwa ya mwanga wala utulivu. Ni saa ile ambayo chombo kinakuwa katika hatari kubwa na kupigwa na kuyumbishwa na upepo mkali wa dhoruba.
Yesu anakuwepo chomboni, lakini amelala katika shetri, sehemu ambayo kwa desturi anakaa nahodha, muongoza meli au vyombo vya majini. Ni Yesu anayepaswa kuwa nahodha na rubani wa chombo kile, yaani Kanisa lake, Ni yeye ambaye tunapaswa kumkimbilia na kumlilia. “Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?” (Marko, 4 :38).
Kwa kumalizia Tafakuri hii nunua TumainiLetu