Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

MANCHESTER, Uingereza
Meneja wa Manchester United Erik ten Hag ameweka wazi kuwa  likizo yake ya majira ya kiangazi iliingiliwa na klabu hiyo mara baada ya kumfuata kwake na kumwomba aendelee kubaki ndani ya klabu yao.
Mustakabali wa Ten Hag ulikuwa mashakani kabla ya kuiongoza United kupata ushindi katika fainali ya Kombe la FA, lakini klabu hiyo imeamua kumweka Mholanzi huyo mahali pazuri.
United walimaliza katika nafasi ya nane msimu uliopita - nafasi yao ya chini kabisa katika enzi ya Premier League.
Mmiliki mwenza mpya wa United Sir Jim Ratcliffe inadhaniwa alizungumza na kocha wa zamani wa Bayern Munich Thomas Tuchel lakini Mashetani Wekundu hatimaye wakaamua kumbakisha Ten Hag.
“Wasimamizi wa klabu walikuja kwangu nikiwa likizoni, ghafla walijitokeza kwenye mlango wangu na kuniambia wanataka kuendelea nami.”
“Manchester United wameniambia kwamba walizungumza na Tuchel, lakini hatimaye walifikia hitimisho kwamba tayari wana meneja bora,” aliongeza.
Katika msimu wake wa kwanza, Mholanzi huyo aliiongoza klabu hiyo hadi nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu, pamoja na fainali za Kombe la Carabao na Kombe la FA na Kisha akawaongoza kwa ushindi wa Kombe la EFL mnamo 2023.

BOSTON, Marekani
Boston Celtics walipata ubingwa wa 18 wa rekodi kwa kuwafunga Dallas Mavericks 106-88 na kukamilisha ushindi wa 4-1 katika Fainali za NBA.
Dallas walikuwa wameweka hai matumaini yao ya ubingwa kwa ushindi wa 122-84 siku ya Ijumaa na kuwanyima Celtics ushindi mnono katika msururu wa michuano yao bora kati ya saba.
Lakini mbele ya mashabiki wao wa nyumbani huko Boston, mbegu bora zilichochewa na ushindi wa Jayson Tatum wa alama 31.
Ushindi huo wa ubingwa ulikuwa wa kwanza kwa Celtics katika kipindi cha miaka 16, na unawafanya kuwa mbele zaidi ya Los Angeles Lakers, ambao wameshinda 17, kwenye vitabu vya rekodi.
Celtics walikuwa na nguvu tangu mwanzo na kuongoza kwa 67-46 katikati, huku Irving na Doncic wakizuiliwa kwa pointi 14 pekee kati yao katika robo ya kwanza.
Dallas walijizatiti kidogo katika hatua za mwisho za robo ya tatu, lakini bado hawakuweza kuwapita Celtics, ambao walichukua faida ya pointi 19 hadi robo ya mwisho.

DAR ES SALAAM

Na Alone Mpanduka

Mbio rasmi za kwanza za baiskeli zilifanyika mnamo 1868 huko Ufaransa. Mnamo mwaka 1885, baiskeli za usalama zilitengenezwa huko Coventry, Uingereza, binamu wa karibu wa baiskeli ya leo. Uendeshaji baiskeli ulianzishwa katika Olimpiki ya kwanza ya kisasa mwaka wa 1896. Mnamo 1903, Maurice Garin alishinda Tour de France ya kwanza, ambayo ilijumuisha maili 1,450 katika hatua sita. 1 Mei 2024.
Kulingana na rekodi za kihistoria, asili ya baiskeli ina mizizi yake katika bustani ya Palais Royal huko Paris, Ufaransa. Mnamo mwaka wa 1791, mtu mmoja aitwaye Comte de Sivrac alionekana akiwa amepanda kitu chenye magurudumu mawili kilichofahamika kama ‘celerifere’.Ikumbukwe kuwa usafiri mkuu wa miaka hiyo ulikuwa ni farasi.
Lakini, ikumbukwe pia kwamba mashindano ya kwanza kabisa ya baiskeli yenye mvuto duniani yalianzia nchini Ufaransa, yakifahamika kama Tour de France.
Ilikuwa ni Novemba mwaka 1902, ambapo Mkurugenzi wa gazeti la michezo la L’Auto, Henri Desgrange, alikuwa akitafuta njia ya kulishinda gazeti la Le Vélo kwa mauzo. Géo Lefèvre, mwandishi chipukizi wa gazeti la L’Auto alitoa pendekezo hili: “Kwa nini tusianzishe mashindano ya baiskeli kote nchini Ufaransa?”
Mwanzoni, wazo hilo lilionekana kuwa lisilowezekana. Hata hivyo, punde si punde likaanza kupamba moto. Alasiri ya Julai 1, 1903, saa 9:16 kamili, jijini Paris, waendeshaji 60 stadi na wengine, wakaanza mashindano yanayoitwa Tour de France ya majuma matatu yenye umbali wa kilometa 2,428.
Mara moja mashindano hayo yakawavutia watu wengi. Mashabiki wengi walikuja kutoka sehemu zote za Ufaransa ili kuwatazama na kuwashangilia washindanaji hao ambao Albert Londres, mwandishi wa habari wa Ufaransa, aliwaita “watumwa wa barabara.” Kwa kweli, katika miaka michache ya kwanza, mashindano hayo hayakuwa rahisi kwa sababu vifaa vilikuwa duni, barabara zilikuwa na mashimo, mikondo ilikuwa mirefu sana, na mara nyingi mikondo hiyo ilianza usiku.
Hatua kubwa ilipigwa kufikia mwaka wa 1919, wakati ambapo mshindi wa jumla wa kila siku alitunukiwa jezi la pekee la rangi ile ile ya kurasa za manjano za gazeti la L’Auto, yaani lile jezi la manjano ambalo hupendwa sana.
Mnamo mwaka wa 1931, Desgrange alibuni gari la matangazo ambalo liliwatangulia washindanaji kwa saa moja likiwachochea mashabiki barabarani, ili kulipia gharama za mashindano hayo.
Mauzo ya Gazeti la L’Auto, ambalo sasa linaitwa L’Équipe, yakapanda. Mwaka wa 1903, nakala 130,000 za toleo la pekee lililochapishwa dakika saba baada ya kufika kwa Maurice Garin, mshindi wa mashindano ya kwanza ya baiskeli nchini Ufaransa, zilinunuliwa mara moja kutoka kwenye vibanda vya kuuzia magazeti.
Siku hizi, kwa sababu mashindano hayo huonyeshwa kwenye televisheni katika nchi zaidi ya 150, mashindano hayo ya Ufaransa yanashikilia nafasi ya tatu kati ya mashindano ya michezo, ambayo husambazwa sana na vyombo vya habari, nafasi za kwanza mbili zikichukuliwa na Michezo ya Olimpiki, na Kombe la Dunia la Soka.
Mashindano hayo yamewavutia watu wengi sana hivi kwamba mwaka wa 1987 wabunge wa Hispania walikatiza mjadala wao ili kutazama ushindi wa mwananchi mwenzao Pedro Delgado akipiga zile kona kali 21 katika mkondo mgumu wa kupanda milima ya Alpe d’Huez.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Benchi la Ufundi la Timu ya Soka ya Simba Queens kupitia kwa kocha msaidizi Mussa Mgosi, ametamba kuwa atahakikisha klabu hiyo inabeba ubingwa mpaka pale yeye atakapoondoka.
Mgosi (pichani) ametamba kuwa kutokana na uwezo waliokuwa nao wachezaji wake, watahakikisha wengine kombe hilo wanaishia kuliona wakati likiwa linatangazwa tu mwanzoni mwa msimu, lakini kulichukua itakuw ni story za Abunuasi.
Alisema pia kuwa umakini wa wachezaji wake, hasa wanapokuwa mazoezini kabla ya mechi, ndiyo sababu kuu ya kuwafanya wafanikiwe kuchukua ubingwa kwa mara nyingine tena.
Mgosi alisema kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanapoenda kushiriki michuano ya Kimataifa waweze kufanya vizuri, na hili litawezekana tu mara baada ya kufanyika kwa usajili mkubwa ndani ya klabu yao kwa kuchukua wachezaji wenye uwezo.
“Tunataka kuuvunja utawala wa Mamelods na tutajitahidi kufanya usajili mzuri ili kubeba ubingwa wa Cecafa, na kisha tutafanya tena usajili kwa ajili ya Klabu bingwa ambayo ina timu zenye wachezaji wazuri wa kiushindani”, alisema Mgosi.
Alisema pia kuwa wachezaji wao wamekuwa chachu ya kufanikiwa klabu hiyo kwenye ligi yao kutokana na usikivu waliokuwa nao mara baada ya kumalizika kwa mechi na kuandaa maandalizi ya mechi nyingine.
Klabu hiyo kwa sasa inajiandaa na michuano ya Afrika kwa wanawake, ambapo msimu uliopita hawakufanikiwa kushiriki michuano hiyo kutokana na kuukosa ubingwa wa Ligi uliobebwa na klabu ya JKT Queens.

DAR ES SALAAM

Na Nicholaus Kilowoko

Kocha Jamhuri Kihwelo amesema haoni mchezaji yeyote mzawa wa kumfananisha na mshambuliaji John Bocco, hasa kwenye nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.
Bocco ambaye alistaafu rasmi kuichezea timu ya Simba SC na kugeukia ukocha wa timu za vijana za Simba SC, hivi karibuni alipewa shukrani za dhati na kheri katika maisha yake mapya na uongozi wa wekundu hao.
Akimzungumzia mkongwe huyo, Kocha huyo mwenye jina maarufu kama Julio alisema anaufahamu vyema uwezo wake uwanjani, pamoja na nidhamu aliyonayo ambayo imemfikisha mahali pazuri kwenye soka lake, licha ya kutocheza soka nje ya nchi.
Alisema kuwa Tanzania ina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa soka lakini nidhamu yao si nzuri, na hivyo kuwafanya washindwe kufika mbali na kujikuta wanastaafu soka wakiwa na umri mdogo.
“Mimi nimefundisha wachezaji wengi waliojaaliwa vipaji vizuri na vikubwa, lakini hawana nidhamu ikilinganishwa na Bocco.Unaweza kuwaambia wachezaji waingie kambini siku fulani, lakini cha kushangaza wanachelewa kuripoti. Bocco alipojiunga na Simba akitokea Azam FC, aliibadilisha kwa kiasi kikubwa katika eneo la nidhamu,”alisema Julio.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Klabu ya Soka ya Azam FC Thabit Zacharia maarufu kama Zaka Zakazi, alisema kwamba Bocco ataendelea kubaki katika mioyo ya mashabiki na viongozi wa Azam FC kutokana na nidhamu yake.
Alisema pia kuwa Bocco hakuwa mtu wa kupigana uwanjani ama kucheza rafu zisizo na msingi ama kuwa mtu wa starehe nje ya uwanja.
“Nakumbuka Bocco wakati yupo Azam FC, ikitokea Ligi imesimama kwa wiki moja ama mbili kupisha ratiba zingine, wachezaji wenzake wote walikuwa wanaondoka kwenye hosteli, yeye anabaki peke yake na kufanya mazoezi binafsi.Anaweza kuchukua mpira akawa anaukokota goli hadi goli. Hakuwa anaijua pombe wala starehe nyingine yoyote.”
Alisema kuwa Bocco ndiye aliyefunga mabao yaliyoiwezesha timu hiyo kutinga Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2008 na kisha kuchangia katika ubingwa iliyopata msimu wa 2013/14 na kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia yake.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema kuwa Pendekoste ni mwanzo wa Kanisa, wa kuitangaza habari njema na Injli.
Aidha, amesema kuwa Injili ni mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Ekaristi Takatifu, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Maria De Mathias, Mivumoni, jimboni Dar es Salaam.
“Pentekoste ni fumbo la wokovu wetu, ambao kila mbatizwa anaitwa na anatumwa kuliishi na kulishuhudia…Kabla ya kuteswa kwake, Bwana Yesu Kristo aliwaandaa wafuasi wake, aliwafundisha, aliwatangazia kwamba ulimpasa kukataliwa na watu, kufa kifo cha aibu, lakini kwamba atafufuka.”
Alisema kuwa Yesu aliwatangazia ukweli huu wa kukataliwa kwake, kuzalilishwa kwake, kuuawa kwake na kufufuka kwake, lakini pamoja na kuambiwa jambo hilo mara tatu Mitume hawakulipokea hawakulielewa,kwa sababu vyote wanajua lakini habari ya ufufuko, si habari waliyoizoea.
Askofu Mkuu alisema: “Yesu peke yake ndiye aliyeteswa, akafa na akafufuka na kwa hayo, sisi tumekombolewa na kutambulika kama watoto wa Mungu.”
Kwa mujibu wa Askofu Ruwa’ichi, kila mmoja anapaswa kujua wajibu na jukumu lake katika utume huu, na atekeleze kwa nguvu zote.
Alibainisha kuwa Utume huo ni kumtangaza Kristo kwa ulimwengu, wamfahamu na wampokee na kupokea tunu yake Mungu.
“Kumtangza Kristo ni jukumu zito ambalo hatuwezi kufanya kwa nguvu zetu wenyewe, bali ni kwa nguvu zake Roho Mtakatifu,”alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Naye Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Maria De Mathias, Mivumoni, Padri Edwin Kigomba, alimshukuru Askofu kwa kuadhimisha Misa hiyo na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 85, akiwakumbusha waamini kutimiza wajibu wao  kuieneza Injili.
“Watoto, endeleeni na maisha ya kiroho, hata baada ya kupokea sakramenti hii.
Aidha, Padri Kigomba alitumia nafasi hiyo kuwasihi Maparoko, Waamini na wote wenye mapenzi mema, kujitoa kwa hali na mali kusaidia Tumaini Media, ili iweze kuinjlisha kote nchini.
Naye Chysanthus Chenga, Mwenyekiti Parokia hiyo, alisema kuwa wanamsukuru Mungu, na kumpongeza Askofu kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wake.
Aidha, alisema kwamba watakuwa bega kwa bega katika kuunga mkono juhudi za Askofu Mkuu Ruwa’ichi katika ujenzi wa Kanisa mbadala huko Gezaulole.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, Chenga aliwataka wenye nia ya uongozi na nia ya kuwaendeleza watu, wajitoe na kuchukua fomu wakati utakapofika, ili kuwania nafasi hizo.

MVOMERO

Na Mwandishi wetu

Club ya mpira ya wahitimu Chuo Kikuu Mzumbe wameahidi kuchangia ujenzi wa vyoo na sehemu ya kubadilisha mavazi kwa Wasichana wa Shule ya Msingi Mzumbe, iliyopo wilayani Mvomero, mkoani Morogoro.
Hayo yalisemwa na Dk. Lucy Massoi, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kimataifa, Baraza la Wahitimu Chuo Kikuu Mzumbe, na kusema kwamba mkakati wa Chuo hicho ni kuendeleza mashirikiano na wahitimu wawe mabalozi wazuri  kikitangaza Chuo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB), na Jumuiya nyingine za watu wenye ulemavu, ili kuweka mazingira wezeshi yatakayowasaidia watu wenye ulemavu kufaidika na fursa mbalimbali nchini.
Rais Mwinyi aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla wakati wa kuahirisha Maadhimisho ya Kuongeza Uwelewa kwa Jamii Juu ya Watu Wenye Ulemavu katika viwanja vya mpira wa Mto wa Pwani Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema kwamba kwa kutambua kuwa watu wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana na chamgamoto mbali mbali katika jamii, kumeanzishwa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu na Mabaraza ya Wilaya ya watu wenye Ulemavu yenye dhamana ya kusimamia, kutekeleza, kutetea na kulinda haki na fursa za watu wenye Ulemavu.
Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali imetoa nafasi za Uongozi kwa watu wenye ulemavu katika Wizara mbalimbali, ambapo wamekuwa wakitekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa, jambo linalotoa hamasa kwa Serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wenye ulemavu.
Dkt. Mwinyi alisema Serikali itahakikisha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu inafanyiwa kazi na kupelekwa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kujadiliwa, na hatimaye kupitishwa kuwa Sheria kamili, ikitoa miongozo kwa Taasisi na Jumuiya za watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufanikisha malengo yao waliyojipangia.
Alibainisha kuwa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, Serikali imekuwa ikichukua hatua za kuweka mazingira bora kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kutunga Sheria ya watu wenye Ulemavu Namba (8) ya Mwaka 2022 kwa lengo la kulinda na kutetea haki na fursa za watu wenye ulemavu.
Aidha, Rais Mwinyi alisema Serikali kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, itaandaa programu maalum itakayowajengea uwelewa wananchi juu ya kutambua haki na wajibu wa watu wenye ulemavu katika Mikoa yote ya Zanzibar.
Sanjari na hilo, Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa Jumuiya za Watu Wenye Ulemavu kuongeza nguvu zaid ya uwajibikaji, na kuwahamasisha watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa mbali mbali zinazojitokeza katika Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Muhammed alisema, Serikali zote mbili zimefanya mapitio ya Sera na Sheria kuhakikisha watu wote wanapata haki sawa, ikiwa ni pamoja na makundi maalum katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii.
Dk. Khalid alifahamisha kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Uwezeshaji, imejipanga kumaliza kilio cha muda mrefu cha watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mikopo itakayowasaidia kujiendeleza kiuchumi katika miradi yao, pamoja na kujikimu kimaisha.

UZINDUZI MWEZI MOYO MTAKATIFU WA YESU

Maasi yaibua mjadala

  •  Askofu: Dunia ingekuwa basi, abiria wote wangeshuka

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Imeelezwa kuwa Dunia ingekuwa ni basi ama daladala, abiria wote wangeshuka na kuondoka zao, hasa kutokana na maasi yaliyokithiri, ikiwemo vitendo vya ushoga na usagaji vinavyozidi kushamiri nchini na dunia kwa ujumla.
Aidha waamini wamatakiwa kuchangia na kuitegemeza Tumaini Media, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwekeza mbinguni, kwani kazi kubwa ya chombo hicho ni uinjilishaji.
Hayo yalisemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Kampeni ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa mwaka 2024, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimbioni humo.
“Kwa maasi haya ya sasa, dunia ingekuwa ni basi, abiria wote wangeshuka na kuondoka zao,”alisema Askofu Mchamungu.
Aidha, Askofu Mchamungu, aliwakumbusha Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu kuiga mfano wa Yesu Kristo juu ya kuwapenda na kuwasaidia wengine, kwani Kristo alikubali kutoa uhai wake kwa ajili ya wanadamu.
“Alitupenda mpaka kufa msalabani. Na sisi tunajua waziwazi kwamba moyo unaashiria upendo, lakini pia moyo unaashiria huruma. Kristo alitupenda upendo usiokuwa na mwisho. Kwa hiyo, na sisi Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu tunapaswa kumuiga Kristo ambaye alitupenda mpaka kumwaga damu yake.
“Pengine si rahisi kufikia kile kiwango chake kwamba tuko tayari kutoa uhai wetu kwa ajili ya wengine. Mbona hata katika familia wakati mwingine mwanandoa mmoja anaweza akamuacha mwenzake, kisa ‘ame-paralyse’, kwa sababu ameshaona kwamba mwenzake hajiwezi tena, hivyo anaona atapata shida sana. Kwa hiyo pamoja na hayo, tutambue kwamba tunapaswa kupendana,” alisema Askofu Mchamungu.
Wakati huo huo, Askofu huyo aliwataka Wanamoyo kuongeza nguvu katika kusal ili maovu yapungue, kwani baadhi ya mambo yanayoendelea ulimwunguni, si ya kuridhisha.
Aliwapongeza pia kwa jinsi wanavyojitahidi katika masuala ya imani, huku akiwasihi kuongeza jitihada hizo ili zionekane katika matendo juu ya kuichukia dhambi.
Askofu alibainisha kuwa miongoni mwa mambo makubwa wanayotakiwa kuyazingatia Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu, ni pamoja na kuichukia dhambi, kwani haipendezi kumuona mwanachama huyo kushabikia dhambi katika maisha yake.
Aliwaonya pia kuepuka kufanya vitendo vya mauaji, wala kuhusika katika tukio lolote la kuangamiza uhai wa mtu mwingine, kama vile kibaka, kwani lengo la chama hicho ni kuiga upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao.
“Ikitokea, kwa mfano, kuna kibaka huko ameiba akakamatwa, watu wakaanza kumzunguka wanataka kumuadhibu kwa kumchoma moto, itakuwa ni kitu cha kushangaza sana kuona kwamba kati ya hao wanaotaka kufanya kitendo hicho, yupo mtu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kitakuwa kitu cha ajabu sana, yaani haiingii akilini…
“Katika tukio hilo, unamkuta mtu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ndiye anaenda kutafuta kibiriti au mafuta ya taa kwa ajili ya kumchoma kibaka, hiyo haiji kabisa, haviendani na vile Kristo alivyotutaka, na kwamba mtu anajiunga kwenye Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kuiga ule upendo na huruma ya Mungu,” alisema Askofu Mchamungu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padri Chesco Msaga, ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Tumaini Media, aliwaomba Waamini kuendelea kuvichangia vyombo hivyo, kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa wameshiriki katika kazi ya uinjilishaji.
Naye Mkurugenzi wa Tumaini Media, Padri Joseph Massenge alimshukuru Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi kwa kukubali mwezi Juni uwe ni maalumu kwa ajili ya kukichangia chombo hicho, ili kiendelee vyema katika kazi yake ya uinjilishaji.
Padri Massenge aliwashukuru Maaskofu Wasaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Henry Mchamungu na Mhashamu Stephano Musomba kwa kuendelea kuhamasisha pamoja na kuvilea vyombo hivyo vya Tumaini Media, vinavyohusisha televishen, radio, pamoja na gazeti.
Sambamba na hayo, Mkurugenzi huyo alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kuadhimisha Misa hiyo Takatifu, huku akiwashukuru pia Mapadri wenzake wote walioungana naye kwa ajili ya Adhimisho hilo.
Padri Cornelius Mashare, Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme - Tabata, alikipongeza chombo hicho kwa kazi yake kubwa ya uijilishaji, huku akiwaomba Waamini kuendelea kukiwezesha, kukitangaza, pamoja na kukisaidia chombo hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko wa Tumaini Media, Arnord Kimanganu Mtui aliwashukuru Waamini kwa majitoleo yao, huku akisema kuwa kutokana na mwitikio mkubwa ambao ulionekana mwaka jana 2023, mwaka huu wameanza vyema kwa kujiwekea malengo ya kukusanya kiasi cha Shilingi milioni 550, wakiwa na imani kwamba kama zitafanyika juhudi kama za mwaka jana, watafikia malengo hayo.
Kimanganu  aliongeza kuwa mpaka sasa tayari gharama za upanuzi wa masafa kwenda Mahenge Shilingi milioni 30 zimeshafanyika, hivyo kinachosubiriwa kwa sasa ni kwenda tu kuwasha mitambo hiyo, na kuongeza kuwa sababu iliyochelewesha ni kutokana na ubovu wa miundombini ya barabara ya kwenda Mahenge.
Naye Mhandisi John Ndazi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam alisema kuwa Tumaini Media ni chombo cha wote, hivyo ni wajibu wao kujitolea kukichangia chombo hicho.
Akizungumza katika Adhimisho hilo, Mwenyekiti wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Godon Rwenyagira, alimwahidi Mkurugenzi pamoja na wafanyakazi wa Tumaini Media kuwa wao kama Wanamoyo, wamejipanga kuhakikisha kwamba bahasha zote zilizotolewa kwa ajili ya michango hiyo, zitarudishwa kama ilivyokusudiwa, kwani wamelibeba jukumu hilo kwa upendo mkubwa.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Vijana wameonywa kuacha kuiga tamaduni zisizofaa, ikiwemo wanaume kuvaa hereni na kusuka nywele zao.
Aidha, wametakiwa kudumu katika imani, wakitambua kwamba tamaduni hizo zinaweza kuwaingiza  kwenye dhambi.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 98 katika Parokia ya Mtakatifu Fransisko Ksaveri – Chang’ombe, jimboni humo.
“Mnapopokea Sakramenti hii ya Kipaimara na mnatakiwa muendelee kudumu katika imani yenu, hivyo mnatakiwa kuepuka kuiga tamaduni zisizofaa, mfano, unamkuta mwanaume anavaa suruali anaweka mlegezo, anavaa hereni, anasuka nywele kichwani kama mwanamke. Epukeni kuiga tamaduni za namna hiyo,” alisema Askofu Mchamungu.
Pia, aliwasisitiza kujiepusha na tabia za udokozi pamoja na kutumia mali zisizokuwa za kwao, bali wahakikishe kwamba pale wanapookota vitu, wavirudishe kwa wenyewe.
Aliwasisitiza pia kuwajibika katika usafi pamoja na kutunza mazingira, akisema kuwa suala la usafi wa mazingira wao kama vijana, linatakiwa kuwa kipaumbele kwao.
Wakati huo huo Askofu Mchamungu aliwakumbusha Wasimamizi wa Waimarishwa hao kwamba miongoni mwa majukumu yao, ni pamoja na kusaidiana na Wazazi katika malezi, ili kujenga maadili ya vijana hao.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Novatus Mbaula alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kufika parokiani hapo pamoja na kuwaimarisha vijana 98 wa Parokia hiyo.
Aidha, Padri Mbaula aliwasihi vijana hao kuendelea kuyazingatia yale yote waliyoambiwa na Askofu wakati wa homilia yake, kwani mafundisho hayo yatawasaidia kukua katika misingi iliyo bora.
Naye Katibu wa Parokia hiyo, Simon Sangawe alivishukuru vyombo vya habari vya Kanisa vilivyoshiriki katika Adhimisho hilo, ikiwemo Tumaini Media, akisema kuwa vyombo hivyo vinafanya kazi kubwa katika suala la uinjilishaji.