Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Services Agency: TFS) umesema kwamba utaendelea kuhamasisha Watanzania kujikita katika ufugaji nyuki kwa kuzingatia maelekezo yote muhimu, na kuwa na vifungashio vyenye ubora unaokubalika.
Hayo yalisemwa na Ofisa Ufugaji Nyuki, Masoko na Leseni wa TFS, Theresia Kamote, wakati wa Maadhimisho ya Barcode Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam

Na Mathayo Kijazi

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu amewapongeza wazazi waliowalea vyema watoto wao tangu walipobatizwa hadi kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, akiwataka wengine kuiga mfano huo.
Pongezi hizo alizitoa wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mtakatifu Nicholaus wa Tolentino, Msingwa, jimboni humo.
“Kwa hiyo, tunawashukuru sana wazazi ambao walikuwa pamoja na hawa watoto, wakawalea kiroho, kwa sababu wale ambao waliachwa katikati humo, baada ya kupata Ubatizo, wazazi hawakuhangaika nao;
“Kwa hiyo watoto hao inawezekana waliishilia huko, wakaendelea kukua bila kupata Ekaristi, bila kupata Kipaimara. Kwa hiyo, wako watu wa namna hiyo ambao wazazi hawahangaiki na watoto katika makuzi yao ya kiroho…. Walioko hapa mbele yetu inaonekana wazazi waliwajali, waliyajali maisha yao ya kiroho, wakawaongoza, hadi kupokea Sakramenti hii,” alisema Askofu Mchamungu.
Aidha, licha ya kuwapongeza wazazi hao kutokana na jitihada katika malezi, Askofu Mchamungu alisema kuwa bado wanalo jukumu la kuendelea kuwalea, kwani bado ni watoto na wanaendelea kukua.
Alisisitiza kuwa watoto hao bado ni wadogo huku wakiwa hawana uwezo wa kufanya maamuzi binafsi, hivyo ni vema wazazi wakaendelea kuwasimamia ili wakue katika misingi na imani thabiti.
“Bado ni watoto ambao hawawezi kufanya maamuzi binafsi, kwa sababu bado wako pungufu ya miaka 18. Aliye na miaka 18 au zaidi, tunasema ni mtu mzima, anajifanyia maamuzi yake, lakini hawa ambao leo hii wataimarishwa, bado ni watoto, na bado wanahitaji uangalizi wa wazazi,” alisema Askofu Mchamungu.
Wakati huo huo pia aliwasisitiza Waimarishwa kuzidi kuisimamia imani yao, huku akiwasihi kwamba wasije wakafika mahali wakaiacha imani yao, na kushikilia imani dhaifu katika maisha yao.
Aliongeza pia kwamba zipo jitihada kubwa zilizofanywa na Makatekista kwa watoto hao tangu walipopokea Kumunyo ya Kwanza, na kisha kuwaandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, hivyo utume wao ni wa kipekee na wenye thamani kubwa.
Askofu Mchamungu aliwakumbusha kuwa kazi ya Roho Mtakatifu ni kumwimarisha Mwamini, hivyo akawataka Waimarishwa kumpokea Roho huyo, ili awafanye kuwa Askari hodari wa Kristo katika maisha yao.
Pia, aliwasisitiza Waimarishwa hao kuwa wakakamavu kama walivyo askari wengine, akisema, “Kwa kawaida mtu anayeitwa askari, ni mkakamavu, hakuna askari ambaye yuko ‘slow slow’ tu, amelegealegea kama konokono, hapana, askari yuko mkakamavu.”
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Efrem Msigala alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kuadhimisha Misa hiyo.
Parokia ya Mtakatifu Nicholaus wa Tolentino ilianza kama Kigango cha Parokia ya Mtakatifu Augustino, Temboni, na ilitangazwa rasmi kuwa Parokia Julai 7 mwaka 2022 na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi.

Dar es Salaam

Na Mathayo Kijazi

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, amewataka wazazi nchini kuendelea kutimiza wajibu wao katika kufanikisha mpango wa Mungu wa kuzaliana na kuijaza Dunia.
Askofu Mchamungu alitoa wito huo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Utoaji wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyofanyika katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Kalmeri, Bunju, jimboni humo.
“Siku hizi wapo watu wa baadhi ya Mataifa Duniani, wanaohangaika kwa nchi zao zikiwa hazina watoto…nguvu kazi imekwisha kutokana na kuzaa mtoto mmoja mmoja, ama kuzuia uzazi. Hii ni mbaya, na ni kwenda kinyume na mpango wa Mungu,” alisema Askofu Mchamungu.
Alisema kuwa Wanaparokia ya Bunju wamejitahidi kwa wazazi kutimiza wajibu wao katika kufanikisha mpango wa Mungu kwa kuzaa watoto wengi, kwani katika Misa hiyo imeshuhudiwa wazi kwamba zaidi ya watoto 200 wamepokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, na hiyo ni ushahidi tosha kwamba wanaijaza Dunia.
Askofu Mchamungu alisema kuwa ni jambo la kutia moyo kuona baadhi ya wazazi wamekuwa wakitimiza wajibu huo kikamilifu, kwani mpango wa Mungu wa kuwaweka wanadamu Duniani, ni kuutiisha Ulimwengu na kuijaza Dunia kwa njia ya kuzaliana.
Aidha, Askofu huyo alisisitiza kwamba mataifa mbalimbali Duniani ambayo yamepiga vita uzazi, matokeo yake kwa sasa wanahangaika kutokana na madhara makubwa ya kupungua kwa nguvu kazi ya Taifa kwa sababu ya kutowepo watoto.
Aliwasihi wazazi kuachana na mambo ya kuiga ya kuzaa mtoto mmoja kwa kuiga mataifa mengine, akionya kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mpango wa Mungu kuhusu uzazi.
Askofu Mchamungu aliwataka wazazi kujitahidi kuwalea watoto wao katika misingi ya kiimani, na kuwaimarisha kiroho ili kuandaa jamii bora na Taifa bora la baadaye.
Katika hatua nyingine, Askofu Mchamungu aliwapongeza waamini wa Parokia ya Bunju kwa hatua kubwa ya kujenga kanisa kubwa, alilosema kwamba endapo litakamilika, litakuwa kubwa kuliko lo lote katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, na hilo wanaweza hata kuliita Basilika.

Dar es Salaam

Na Mathayo Kijazi

Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yuda Thadei Mtume, Stakishari, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wametakiwa kuishi maisha ya utakatifu, wakitambua kamba wamebatizwa ili kuishi kitakatifu.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Laurent Lelo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyokwenda sanjari na kuapishwa kwa Viongozi wa Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Taifa, iliyofanyika parokiani hapo.
Katika homilia yake, Padri Lelo aliwasisitiza Waamini kupendana kutoka ndani ya mioyo yao, wakisaidiana pale inapohitajika, kwani hiyo ni moja ya sifa za Mkristo.
Alisema kuwa kila mmoja anatakiwa kumkimbilia Mungu zaidi, na kuwakumbusha kwamba mtu anapoutafuta utakatifu, ndipo shetani anapozidi kumnyemelea.
Wakati huo huo, Wakristo wameaswa kutambua kwamba nguvu ya Mungu ni kubwa kuliko ya mwanadamu, kwani ndiye mkombozi, na anayewatoa katika majaribu kila wanapokutana nayo.
Kwa mujibu wa Padri Lelo, waamini hao wanapaswa kuendelea kumwomba Mungu ili familia, Jumuiya, na hata Parokia zao ziwe katika muungano, huku wakiikimbilia huruma ya Mungu, kwani itawasaidia pale wanapotawanyika, hivyo Yeye aweze kuwarudisha katika misingi iliyo bora.
Aidha, wao kama wabatizwa, walikumbushwa pia kusaidia kuwarudisha kundini wale waliosambaratika, huku wakiaswa kuwa kwa kufanya hivyo, watakuwa wametimiza wajibu wao.
Padri Lelo aliwasisitiza Wakristo kulihubiri Neno la Mungu, na kuongeza kuwa hata katika shamba la Bwana, mavuno ni mengi, bali watenda kazi ni wachache.
Viongozi wa UWAKA Taifa, walioapishwa katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu, ni Mwenyekiti Cassian Njowoka, Mwenyekiti Msaidizi Salvatory Mrema, Katibu Silvester Musumi, na Katibu Msaidizi, Seraphin Mvungi.

ZOMBA, Malawi

Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padri Alfred Mateyu Chaima kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Zomba, nchini Malawi.
Baraza la Maaskofu Katoliki wa Malawi (Episcopal Conference of Malawi: ECM) lilithibitisha uteuzi huo katika taarifa yake iliyotiwa saini na Rais wake, Askofu Mkuu George Desmond Tambala, ikieleza kuwa hiyo ni katika kutekeleza kazi ya Mungu.
“Naomba kila mmoja ajiunge nami, Jimbo la Zomba na Baraza zima la Maaskofu wa Malawi kumpongeza Askofu Mteule. Tumkumbuke katika maombi yetu kwa ajili ya huduma nyenyekevu na yenye mafanikio ya Uaskofu wake. Wema wa Bwana unaendelea kujitokeza mbele yetu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Jimbo Katoliki la Zomba limekuwa bila Askofu kuanzia Oktoba 2021, kufuatia Askofu wa wakati huo Mhashamu George Desmond Tambala kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Lilongwe.
Kufuatia hali hiyo, Jimbo Katoliki la Zomba limetangaza kuwa sherehe za kumweka wakfu Askofu huyo, zitafanyika Agosti 12 mwaka huu.
Akijibu habari za uteuzi wake, Padri Chaima alisema kuwa amepokea uteuzi huo na anatambua kuwa si kazi rahisi, akiwaomba watu wenye mapenzi mema, kumkumbuka daima katika sala.
“Nimefurahia maendeleo kama mtumishi katika huduma ya Mungu, ambapo unapaswa kuwa tayari kwenda popote unapoombwa kwenda. Nitategemea maombi yangu pamoja na maombi ya watu wote kanisani ili nifanikiwe,” alisema Askofu Mteule Chaima.
Askofu Mteule Chaima alihudumu kama Katibu Mkuu wa ECM katika Sekretarieti ya Kanisa Katoliki. Mbali na hayo, alihudumu katika nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kama mwalimu, Mratibu na Mkuu katika Seminari Ndogo ya Pius XII; na Katibu wa Kichungaji wa Jimbo Kuu la Blantyre.
Alikuwa Mkurugenzi wa Nantipwiri Pastoral Centre, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Kikristo cha Afya (CHAM), Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Malawi, na Mhadhiri wa Muda katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Malawi - Idara za Theolojia na Mafunzo ya Dini/ Biblia na mhadhiri wa muda katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, Chuo cha Tangaza na Taasisi ya Kichungaji ya Gaba, kwa kutaja machache tu.
Safari yake ya Upadri ilianzia katika Seminari ya Mtakatifu Pius XII ambako alipata elimu ya sekondari, na baadaye alijiunga na Seminari Kuu ya Kachebere kwa masomo ya Falsafa, na kisha aliendelea na masomo ya Theolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Petro huko Zomba.
Alipewa Daraja ya Ushemasi mwaka 1998 katika Kanisa Kuu Katoliki la Zomba, Jimbo Kuu Katoliki la Zomba, na baadaye akawa Kuhani katika Kanisa Kuu la Limbe, Jimbo Kuu Katoliki la Blantyre mwaka 1998.
Ana Shahada ya Udaktari (PhD) katika Theolojia ya Kichungaji kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki (Catholic University of Eastern Africa: CUEA).

LUSAKA, Zambia
Baba Mtakatifu Fransisko ametangaza uteuzi wa Balozi mpya wa Kitume kwa nchi mbili katika Jumuiya ya Mabaraza ya Maaskofu Wanachama katika eneo la Mashariki mwa Afrika (Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa: AMECEA); Zambia na Malawi.
Baba Mtakatifu, katika ujumbe wake, alimtaja Askofu Mkuu Gian Luca Perici kuwa Balozi wa Kitume nchini Zambia na Malawi.
Anachukua nafasi ya Askofu Mkuu Gianfranco Gallone ambaye alitumwa tena Uruguay katika wadhfa huo mwanzoni mwa mwaka 2023.
Askofu Mkuu Perici aliyezaliwa mwaka 1964 nchini Italia, alipewa daraja la Upadri mwaka 1991, na ana Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa.
Askofu Perici alijiunga na huduma ya Kidiplomasia ya Jimbo Kuu tarehe 1 Julai mwaka 2001, na amehudumu katika Baraza la Kitume huko Mexico, Haiti, Malta, Angola, Brazil, Sweden, Hispania na Ureno.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, Padri  Francis Mukosa, alisema kuwa wamepokea uteuzi huo kwa moyo wa Kitume na kumkaribisha Askofu Mkuu Perici.
Baba Mtakatifu Paulo VI (1963-1978: wa 262), alifungua Baraza la Watawa nchini Zambia Oktoba 27 mwaka 1965, huku Askofu Mkuu Alfredo Poledrini akiwa Balozi wa kwanza wa Kitume.
Tangu mwaka 1965, Zambia ilikuwa na Mabalozi tisa wa Kitume ambao pia wanacheza kama mabalozi wa Vatican.

NAIROBI, Kenya
Wajumbe wa Jumuiya ya Kikatoliki ya Kuhudumia Watoto (CCC) imewaleta pamoja washiriki kutoka sehemu mbalimbali za Dunia, wakiwemo Maaskofu, Dini, Wakleri, Walei na washirika kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Non-Governmental Organisations: NGOs), Wawakilishi wa Serikali, kutoka Vatican, na wale wa elimu, ili kujadili ukatiti dhidi ya watoto.
Hatua hiyo ya kuitishwa kwa mkutano huo ni kutokana na muhtasari wa utafiti wake, huku wakilenga kujadili pia njia ya kusonga mbele, ikilenga matokeo ya utafiti unaotoa mfumo wa ulinzi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika eneo la Afrika Mashariki.

VATICAN CITY, Vatican
Gazeti la ‘II Messaggero’, limetimiza miaka 145 tangu kuanzishwa kwake, wakati huu linapoendelea na maandalizi yake ya Jubilei yake itakayofanyika mwaka 2025.
Baba Mtakatifu Fransisko katika ujumbe wake aliomwandikia Dk. Francesco Gaetano Caltagirone, Rais wa Gazeti hilo la ‘Il Messaggero’ pamoja na mambo mengine, alikazia kanuni maadili ili kuepuka habari za kughushi.
Gazeti la ‘Il Messaggero’ lilianzishwa mjini Roma Desemba 8, maka 1878 na Luigi Cesana kutoka Milan, wakati huo akiwa na umri wa miaka 27 na Baldassarre Avanzini kutoka La Spezia, mwanzilishi wa zamani wa Il Fanfulla huko Florence.
Matoleo manne ya majaribio yalichapishwa kati ya Desemba 16 na 19 mwaka 1878, na kwa mwaka 2023 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 145 tangu kuanzishwa kwake.
Gazeti hili limejipambanua kuwa na nguvu ya uandishi wa habari kwa ajili ya kuwahabarisha Walimwengu.
Baba Mtakatifu alitia shime watendaji wa gazeti hilo ili kujielekeza na kujikita zaidi katika kanuni maadili na utu wema, kama sehemu ya mapambano dhidi ya jamii.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amesema kwamba Wakatoliki wanapaswa kuitangaza na kuishuhudia Injili kwa Matendo ya Huruma, kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu alitoa rai hiyo katika salamu zake, akisema kuwa Bwana Yesu Kristo anayewachagua na kuwatuma Mitume wake 12 ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kuonesha uwepo wa karibu wa Mungu, waamini wanatakiwa kujifunza kuwa Mitume bora, ili kutangaza na kushuhudia upendo na matumaini kwa njia ya huduma makini, kwa sala, tafakari ya Neno la Mungu, na maisha ya Kisakramenti.
Baba Mtakatifu Fransisko alisema kuwa Injili inapaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa matendo, na si vinginevyo.
“Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima,” alisema Baba Mtakatifu.
Alibainisha kuwa Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote, kiroho na kimwili.
Papa aliongeza kusema kwamba upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii.
Alisema kuwa Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu alisema kuwa Kristo Yesu aliwachagua na kuwatuma Mitume wake kutangaza na kushuhudia kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia, yaani huruma na upendo wa Mungu umemkaribia na kumwandama mwanadamu kiasi cha kukaa kati yake.
Aliendelea kwa kusema kuwa huu ndio uhalisia wa maisha, changamoto na mwaliko kwa waamini kukuza imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu anayewapenda sana waja wake, na anataka kuwashika mkono na kuwaongoza taratibu, anataka kuwapenda, na hivyo kuhisi uwepo wake wenye nguvu, tayari kuwaongoza waja wake.
Baba Mtakatifu Fransisko alikazia kwa kusema kwamba ili kuwa Mitume wazuri, kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani, kuna haja ya kupiga magoti na kujifunza, na hatimaye kushuhudia kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Baba anayeweza kugeuza nyoyo za watoto wake, na kuwakirimia furaha na amani ambayo kwa nguvu na jitihada zao binafsi, hawawezi kuipata.

Na Pd. Gaston George Mkude

Amani na Salama!
njili ya leo inatanguliwa na Yesu anapowatuma Mitume wake kumi na wawili, na kuwapa tahadhari juu ya hatari zilizopo mbele yao, na hivyo kuenenda kwa hekima na busara, lakini zaidi sana kudumu katika ujasiri.

Tangu mwanzo, Yesu anawaonesha Wanafunzi wake na hata nasi leo kuwa utume wa kuwa mashahidi wake sio lelemama, na unatutaka kujizatiti. Ni Injili inayotualika kujiandaa kwa gharama ya ufuasi na maisha ya ushahidi.
Mwinjili Matayo anaandika sehemu ya Injili ya leo wakati Wakristo wale wa mwanzo wanapitia madhulumu ya Kaisari Domisiano, aliyetoa amri katika dola zima la Kirumi kuwekwe sanamu yenye sura yake, na kuabudiwa kama mungu.

Hivyo, wale wote waliokataa kuabudu sanamu ile, waliteswa na hata kuuawa kwa amri ya mtawala yule wa Kirumi. Wakristo wale wa mwanzo waliokuwa wenye asili ya Kiyahudi, nao pia walitengwa katika masinagogi kwa kuwa ni wafuasi wa Kristo Mfufuka.

Hivyo ni katika muktadha huo Mwinjili anaandika sehemu ya Injili ya leo kuwafariji, na zaidi kuwakumbusha maneno ya Kristo mwenyewe wakati alipokuwa nao, maana sasa tunazungumzia kizazi cha pili cha Kanisa, na wengi hawakumwona Yesu uso kwa uso, zaidi ya kupokea Habari Njema kutoka kwa Mitume wake.

Ni Kanisa teswa lililokuwa likiishi imani yake kwa hofu na kujificha, huku wakigubikwa na hofu kubwa kutoka maadui wao wakubwa wawili, ambao ni Dola la utawala wa Kirumi na Wakuu wa Masinagogi, au Wakuu wa Dini ya Kiyahudi.

Mwinjili anawakumbusha Wakristo wale wa kwanza kuwa tayari Bwana na Mwalimu wao alishawatabiria juu ya magumu, mateso na madhulumu. Hivyo sio kitu kigeni, na hawapaswi kukata tamaa wala kurudi nyuma katika safari yao ya ufuasi na kuwa mashahidi wa Habari Njema ya ukombozi. Tunaona pia Mtume Paulo anapomwandikia waraka ule wa pili Timoteo akisema;

“Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu, lazima adhulumiwe.” (2Timoteo, 3:12). Mtume Paulo anaandika naye kipindi kile kile cha madhulumu na mateso ya Kanisa lile la mwanzo.

Ni katika mazingira hayo ya mateso na madhulumu tunapoona Yesu anawaalika Wanafunzi wake kutoogopa, kutokukubali kurudi nyuma kwa sababu ya uoga na hofu. Tunasikia Yesu akiwaalika mara tatu “msiogope”. Uoga unaweza kuwa na upande chanya kututahadharisha na hatari inayokuwa mbele yetu, na hivyo kuenenda kwa tahadhari, lakini ina upande hasi, hasa pale tunapoacha kutawaliwa na uoga na hofu.

 Kila tunaporuhusu uoga ututawale hapa, tunakosa uhai na maisha, tunakosa pumzi na uwezo wa kuishi au wa kusonga mbele katika wito na utume wetu. Kuruhusu uoga utawale maisha yetu, ni kukubali kushindwa kusonga mbele, ni kukubali kujimaliza na kujiangamiza sisi wenyewe.

Uoga ni adui mkubwa katika maisha yetu ya ufuasi. Tunakuwa waoga kupoteza nafasi zetu za heshima kwa kuwa tu wafuasi wa Yesu Kristo, kupoteza marafiki zetu, kupoteza mali na utajiri wa dunia hii, kudharauliwa na wengine, na mara nyingine hata kupoteza maisha yetu. Kila anayeruhusu kutawaliwa na uoga, huyo anapoteza uhuru wa kweli. Anakuwa sawa na mmoja mwenye ugonjwa wa kiharusi kwa kukubali kutawaliwa na uoga.

Na ndiyo maana Yesu anarudia mara tatu nzima ili kututahadharidha na hatari ya uoga katika maisha ya ufuasi.
Wakati wa sherehe za Jubileo Kuu ya Mwaka 2000, Mtakatifu Papa Yohane Paulo II (1978-2005) anatuambia; Miaka elfu mbili ya Ukristo duniani inatambulishwa kwa damu ya mashahidi wa nyakati mbali mbali.
Ndiyo maana anaendelea kutuonesha kuwa Kanisa limekuwa na mashahidi wengi, au wafiadini wengi katika karne ya 20 kuliko hata wale wa Kanisa la mwanzo.

 Na hata leo katika nyakati zetu bado tunashuhudia jinsi Kanisa na Wakristo wanavyopitia madhulumu mengi mahali pengi duniani. Ni zaidi ya madhulumu ya Wafalme wale katili wa Kirumi, yaani Nero, Domisiano, na hata Deoklasiano kwa pamoja!

Anayepelekwa kutangaza Habari Njema anaweza kutawaliwa na uoga wa kushindwa katika misheni yake. Na ndiyo maana Yesu anatukumbusha kuwa hata kama tutakutana na magumu, daima Injili yake itaenea na kusambaa ulimwenguni kote.

Magumu, mateso, kukataliwa na madhulumu, ni sehemu muhimu ya maisha ya ushuhuda wa imani yetu. Ni Yesu anatangulia kutuambia hata nasi leo kuwa njia ya maisha ya ushahidi, ni hiyo ya magumu na mateso.

Yesu kwa kutuhakikishia hilo, anafanya marejeleo kwa Marabi wa nyakati zake ambao walibaki na wanafunzi wao na kuwafundisha sirini mpaka pale mmoja alipohitimu ndipo aliruhusiwa kwenda kufundisha katika viwanja na masinagogi.
 Ndiyo kusema kwamba Yesu anatusisitizia hata pale tunapoona kazi yetu haina mafanikio makubwa kwa macho, na mitazamo yetu ya kibinadamu hakika bado litazaa matunda ni kama vile mbegu iliyozikwa ardhini.

Mfano wa wazi ni watesi wa Yesu mwenyewe mara baada ya kumuua na kumzika na kuweka jiwe kubwa katika mlango wa kaburi, walijiridhisha na kujihakikishia kuwa sasa wameshinda na kufaulu kumnyamazisha mtu yule kutoka Galilaya. Siku ya tatu akafufuka na kuwa mzima tena! Amefufuka kama mbegu iliyokuwa imezikwa ardhini, na sasa imechipua na kuleta matumaini na mwanga mpya.

Sababu ya pili inayoweza kutuletea uoga na hofu, ni madhulumu na mateso, na hata kifo. Na ndipo Yesu pia anatuhakikishia kuwa hakuna ushindi wowote unaoweza kupatikana kwa wale wanaotesa mwili, kwani kila anayekuwa tayari na jasiri kumfuasa Yesu na kuwa shahidi wa Injili, huyo anajaliwa uzima wa milele, maisha ya kweli sasa, na hata milele.

Kila mfuasi wa kweli huyo anapokea siyo tu maisha ya kibailojia, bali maisha ya muunganiko na Mungu mwenyewe. Hivyo ni maisha ya hapa duniani na milele yote. Mtume Paulo anapowaandikia Warumi anawakumbusha pia ukweli huo; “Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? (Warumi, 8:35-39).

Lakini anaendelea Yesu na kututahadharisha kumwogopa mmoja anayeangamiza, si mwili tu, bali pamoja na roho.
Kwa kweli tafsiri sahihi siyo kitu kinachokuwa nje yetu, bali kila mmoja wetu anacho ndani mwake tangu kuzaliwa kwetu, yaani ndiyo nguvu ile ya mwovu inayotuambia kila mara kuenenda kinyume na njia na mipango yake Yesu Kristo.

Kila wazo linalopinga mpango mzima wa Yesu, huwa linapelekea katika angamio langu na lako kwani tunaangamia, si tu mwili, bali pamoja na roho. Kila mmoja wetu anajua ni nini katika maisha yake kinamkinza katika kuiishi na kuwa shahidi wa Injili, na tukichunguza tunaona jambo au kitu hicho asili yake ni ndani mwetu sisi wenyewe. Ule uasi na uovu tunaokuwa nao ndani mwetu unaotushawishi kuenenda kinyume na mapenzi na maagizo ya Mungu, na Neno lake.

Sababu ya tatu inayotuepelekea kuogopa sasa inagusa si tu sisi, bali hata na wale wanaokuwa karibu nasi. Na ni hapo Yesu anapotuhahakishia ulinzi wa Mungu Baba, kwani sote tu wa thamani kubwa mbele yake.

Anatumia mifano ya shomoro na nywele. Shomoro kwa nyakati za Yesu walihesabiwa kuwa ni viumbe wasio na thamani, kwani walikuwa ni ndege waharibifu kwa mazao, na hasa ngano ikiwa bado shambani. Hivyo Wayahudi walipowabariki viumbe vyote vya Mungu, hawakuwabariki shomboro, kwani ni waharibifu, ila leo Yesu anatuonesha kuwa mbele ya Mungu, kila kiumbe kina thamani kubwa.

Hivyo kutuhakikishia kuwa hatuna sababu ya kuwa na uoga wala hofu, hata kama mbele yetu kuna mateso na madhulumu makubwa. Mungu anajua hata hesabu ya unywele mmoja, vile sisi hatuwezi kuhesabu nywele, lakini mbele ya Mungu, sisi sote kama viumbe vyake, tuna thamani kubwa.

Yesu anamalizia kwa ahadi kuwa kila anayemkiri mbele ya watu, huyo atamkiri mbele za Baba yake wa Mbinguni. Ni hakika kuwa tunatambuliwa na Mungu, hata sisi tukiwa kweli wafuasi wa kweli wa Kristo bila kujali hatari zinazoweza kutukabili na hata kutuzuia kuwa mashahidi.
Daima mfuasi hana budi kumtegemea Mungu katika kila hali za maisha ya ufuasi, kwani neema yake ni ya kutosha.
Tafakari njema na Dominika Takatifu!