NA MWANDISHI WETU
Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Dominiko - Mbezi Juu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Daniel Kilala amesema kuwa kila Mbatizwa anatumwa kupokea wajibu wa kutangaza Injili kwa maneno na matendo yake.
Padri Kilala aliyasema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Domonika ya Tano ya Mwaka ‘B’ wa Kanisa, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Paulo anatukumbusha wajibu wetu wa kuhubiri Injili. Sisi sote katika Ubatizo, tulipobatizwa, tumeshirikishwa Ukuhani, Ufalme, na Unabii wa Kristo. Kumbe kila Mbatizwa anapokea wajibu wa kutangaza Injili kwa maneno na matendo yake,” alisema Padri Kilala.
Padri huyo aliwaasa Waamini kuacha kukata tamaa, akiwasihi kuwa na matumaini kila wakati, kwani Mungu yuko pamoja nao kila wakati.
Aliwasisitiza kutokupenda tu mambo yao binafsi, bali wapende pia mambo yanayomhusu Mungu, akisema, “Watu wanapenda sherehe tu, hata ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya kutokuwaombea wanandoa, badala yake watu wanaangalia tu sherehe wakati wa harusi,” alisema Padri Kilala.
Padri Kilala aliwaonya Wakristo kuepuka kutawaliwa na mambo ya anasa na choyo katika maisha yao, akisema kuwa jambo hilo linasababisha baadhi ya mambo yao kuwa magumu.
Aliwataka kuitumia Dominika ya Tano ya Mwaka ‘B’ wa Kanisa kutafakari kuhusu mateso na mahangaiko mbalimbali wanayoyapata, huku wakizidi kumtumainia Kristo katika maisha yao.
Aliongeza kuwa hata wanapokumbana na changamoto mbalimbali za kimaisha, hakuna yeyote wa kumkimbilia, zaidi ya Kristo pekee, kwani yeye ndiye muweza wa mambo yote.
Alibainisha pia kuwa Waamini wanapaswa kutumia muda wao kuwasiliana na Mungu, huku wakitambua umuhimu wa sala, pamoja na kutenga muda maalum kwa ajili ya kusali.
Katika hatua nyingine, Padri Kilala aliwataka waamini kuitegemeza Tumaini Media kwa kuendelea kukiunga mkono chombo hicho, ili Injili iendelee kutangazwa Tanzania na duniani kote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo, Neo Pascal, aliishukuru Tumaini Media kwa namna inavyoendeleza uinjilishaji, akiwasihi Waamini kuendelea kukitegemeza chombo hicho.
Naye Katekista Joseph Francis alisema kuwa wao kama Wakristo, hawana budi kuendelea kujikita katika sala, kwani hiyo itawasaidia kupata neema ya Mungu katika maisha yao.