NA CELINA MATUJA
Imeelezwa kuwa waamini wanashindwa kupata mafanikio katika maisha ya kiroho na kimwili kutokana na kusali kwa mazoea.
Hayo yalisemwa na Mlezi wa Karismatiki Katoliki Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, Padri Henry Rimisho katika Kongamano la Uponyaji lililofunguliwa jijini Dar es Salaam.
Alisema hayo katika mada aliyofundisha juu ya toba na Damu ya Yesu Kristo, ambayo ndiyo silaha ya kuondokana na changamoto zilizosababishwa na mazingira au binadamu.
Alieleza namna nzuri ya kufanya toba kwa kutumia Damu ya Yesu Kristo, akisema, “Kwanza, Mwamini anatakiwa kukiri kuwa amekosa; hatua ya pili ni majuto kwa kuwa toba ya kweli inafuata na majuto; kujutia ni ile hali ya kuikataa dhambi na kuumia; tatu, toba ili ikamilike, lazima mdhambi ageuke na kuanza ukurasa mpya na kufanya mema, katika kutenda haki iwe kwa wenzake, kwenye familia, ama kazini kwake.”
Aidha, Padri Rimisho alisema kuwa mtu anapogeuka na kukiri kwa Mungu, anajipatia furaha ambayo itakuwa sehemu ya maisha yake, na Mungu atammiminia neema na baraka tele.
“Hivyo, kwa kutumia Damu ya Yesu, inapata kutakatifuza, kutakasa maeneo, na hiyo ni kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu yanayosema, “Kikombe hiki ni Damu ya Agano Jipya iliyomwagika kwa ajili yenu, ambapo Mwamini anapata kufahamu mambo matatu muhimu ambayo ni; Damu ya Yesu; ya Agano Jipya; na iliyomwagika kwa ajili ya mwanadamu….
“Ikumbukwe kwamba Yesu Kristo mwenyewe alikufa na alifufuka, hivyo katika kufa kwake, alitoa Damu Yake ya gharama kubwa, ili kumkomboa mwanadamu katika maisha hapa Duniani,” alisema Padri Rimisho.
Padri huyo alisema kuwa katika Agano la Kale, damu ya wanyama ilikuwa ni ishara ya kutambuliwa na kutokudhurika, kwa mfano katika kabila, na ilileta upatanisho, ilifunika dhambi, damu hiyo ilitolewa kila wakati na kila mwaka, na hasa pale walipohitaji kushughulikia dhambi.
Aliongeza kuwa Yesu Kristo alijitoa kwa kumwaga Damu yake ili kuondoa dhambi za mwanadamu, na anaiita Damu ya Agano Jipya kwa sababu yeye alikuja baada ya Agano la Kale, ambalo Mtume Paulo analiita Agano Kuu, ni Agano Jipya kwa utendaji wake Yesu Kristo Mwenyewe.
Padri Rimisho alisema kuwa dhambi zilikuwa zinafunikwa tu, haziondolewi wakati huo wa Agano la Kale, ila kwa Agano Jipya, zinaondolewa kabisa.
“Damu hii ya Yesu ambayo tunasema kuwa ni ya Ukombozi, ni kwa sababu Mwanadamu alikuwa utumwani mwa adui shetani. Hivyo, ililipa deni na kutoa uhuru, kwa sasa Yesu anakuwa ni mjumbe wa Agano Jipya,” aliongeza kusema Padri Rimisho.
Aidha, aliwafafanulia Waamini kazi ya Damu ya Yesu, akisema kuwa kwanza inamwondolea mtu agano la uharibifu, yaani la nguvu za giza; inatumika katika hali ya hatari, ama kuota ndoto chafu kwa kusali.
Aliongeza kuwa kwa kupitia Damu ya Yesu, mwanadamu anayelindwa na nguvu za giza, itanena msamaha, inafuta laana na dhambi ambazo mwanadamu anazotenda.
Kadhalika, Padri Rimisho alibainisha kuwa Damu hiyo inafungua maeneo yaliyofungwa na mazingira, na madhara yake ni kwamba mtu anaweza kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine akiwa na mafanikio makubwa maishani mwake, lakini ghafla maisha yake yanakuwa si ya kuridhisha, hivyo anaweza kutumia Damu ya Yesu.
Alisema kuwa Damu ya Yesu Kristo ni ya Agano Jipya, kwa kuwa iwatutoa wanadamu katika utumwa wa dhambi na maonevu ya shetani, hivyo ililipa deni la mwanadamu na Yesu, ambapo sasa ni mjmbe wa Agano Jipya.
Aliongeza kuwa ni lazima kuelewa kwamba Damu ya Yesu inavunja na kuharibu kila nguvu ya giza na agano la shetani, kwani wapo baadhi wanaota ndoto mbaya, na za kutisha.
Hata hivyo, Padri Rimisho alisema kwamba hakuna atakayedhurika ikiwa ataitumia Damu hiyo, kwani ina nguvu, na imemnunua kila mmoja, hivyo ni ulinzi unaofuta laana na dhambi zinazotendwa na mwanadamu.