Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

GULU, Uganda
Maandalizi ya kutangazwa Padri Joseph Ambrozoli kuwa Mwenyeheri yanaendelea vizuri, tukio litakalofanyika wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu itakayofanyika Jimbo Kuu Katoliki la Gulu, Uganda Novemba 20, mwaka huu.
Mchungaji John Baptist Odama wa Jimbo Kuu Katoliki la Gulu alisema kuwa Kamati Kuu ya Maandalizi (COC) yenye kamati ndogo 16 imeundwa, na wote wanafanya kazi ya kuona jinsi ya kuwapokea watu watakaokuja kuhudhuria ibada hiyo.

DAR ES SALAAM

Na Nicolaus Kilowoko

Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars Mecky Mexime amefunguka kuwa kwa sasa Watanzania wanapaswa kuganga yajayo, hasa katika kuwekeza nguvu na mapenzi juu ya timu yao ya Taifa.
Mexime ameyasema hayo mara baada ya Watanzania wengi kusikitishwa na matokeo ya Taifa kushindwa kufurukuta katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki, na kusababisha wengi kuumia.
Mexime alisema kuwa kwenye mpira hakuna kukata tamaa, na matokeo siku zote ni ya pande tatu, hivyo kwa sasa si vyema kulaumu sana, ila ni kuongeza nguvu kwa pamoja kama Watanzania.
Alisema kuwa timu ya Taifa ni ya Watanzania wote, na si ya mtu mmoja. Hivyo, kila jambo linawezekana ikiwa mataifa mengine yanafanikiwa kushiriki mashindano makubwa, hata Tanzania inaweza kushiriki katika mashindano hayo.
“Siku zote kuteleza siyo kuanguka, na hata kama ukianguka, unapaswa kusimama tena. Watanzania wazidi kupenda vya kwao na kuongeza nguvu kwa pamoja katika kuijenga timu yetu, na siyo kulaumu mtu”, alisema Mexime.
Alisema kuwa mchezo wa mpira kwa sasa ni vyema wote kwa pamoja tukatengeneza mkakati wa pamoja ili tuweze kufanya vyema katika michuano inayofuata na inayoshiriki timu hiyo.
Stars ilishindwa kufurukuta katika uwanja wa Benjamin Mkapa wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya wachezaji wanocheza ligi za ndani, CHAN, mbele ya timu ya Taifa ya Uganda kwa kufungwa bao 1-0.
Huu ni mwendelezo wa matokeo mabovu ambayo Stars wameendelea kuyapata baada ya misimu iliyopita kushindwa kufuzu kucheza Kombe la Dunia, Afcon, Chan pamoja na michezo mbalimbali ya kirafiki.
Meck Maxime anachukua nafasi ya kocha msaidizi mara baada ya kuvunjwa kwa benchi la ufundi la Stars kutokana na matokeo mabovu. Hivyo anaungana kwa sasa na kocha Mkuu, Hanour Janza, akisaidiwa na kocha wa magolikipa, Juma Kaseja.
TFF ilitangaza kukubaliana na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Kim Poulsen kumbadirishia majukumu, na sasa atabaki katika timu za vijana za Taifa.
Ikumbukwe kuwa Kim alitangazwa na TFF kuwa Kocha Mkuu wa Stars, Februari 15 mwaka 202, kabla yake aliwahi kuwa kocha wa Stars mwaka 2012 na 2013.
Kim mpaka anawekwa pembeni, amepoteza mechi 7, akipata ushindi kwenye mechi 6, na sare kwenye mechi 4. Alipewa mkataba wa miaka mitatu kuinoa timu ya Stars.

ARUSHA

Na Mwandishi wetu

Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Padri Dennis Ombeni amewataka Raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki popote walipo, kuwa mstari wa mbele kulinda uhai wa mtoto angali bado tumboni.
Mambo yanayojumuisha katika kumlinda na kumtetea mtoto, yakiwemo ya ukuaji, kumlinda katika nyanja zote kiuchumi, kiafya na kiakili, na ustawi wa Mtoto.
Padri Ombeni aliyasema hayo katika warsha kwa Vijana na wazazi iliyofanyika jijini Arusha iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu athari zilizopo kwenye muswada wa ujinsi na afya ya kizazi wa Jumuiya ya Afika Mashariki wa mwaka 2021.
Kupitia mkutano huo, Padri Ombeni alieleza kusikitishwa juu ya mauaji katika jamii kati ya wanandoa yanayotokea kwa kisingizio cha wivu wa mapenzi jambo alilosema ni ouvu na linapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwani linaingilia Uhai ambao asili yake ni Mungu.
“Maandiko Matakatifu kupitia Bibilia yanaeleza kwa namna kuu mbili, juu ya thamani ya uhai katika Bibilia, Maandiko Matakatifu yanatetea uhai, hasa pale kwenye Agano la Kale, ambapo baada ya Mungu kumuumba Adamu na kumpatia msaidizi wake Eva, aliwabariki na kusema, enendeni mkazae na kuijaza dunia,”alisema Padri Ombeni.                          
Alisema pia kuwa uhai wa mwanadamu ni kitu kitakatifu, hivyo unapaswa kulindwa na kutunzwa tangu kutungwa mimba hadi kifo chake cha kawaida. Hivyo muswada huo wa Ujinsi na Afya ya kizazi haupaswi katika Mataifa ya Jumuiya Afrika Mashariki kwani unakwenda kinyume na Utu, Dini na tamaduni za watu hao.
Kwa mujibu wa Padri Ombeni Mswaada huo unatishia uwepo wa Dini na Imani za Watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia unadhalilisha Mila na Desturi za watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani hautoi nafasi kwa wahudumu wa afya kutumia dhamiri zao katika kutoe elimu ya afya ya uzazi kwa wanaowahudumia.
Kutokana na hayo na mengine maovu yaliyoko katika Mswaada huo ambao umeakisiwa na kupigiwa debe na baadhi ya vikundi vyenye nia ovu na watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Padri Ombeni amewataka watanzania wote kuungana na wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuupinga Muswaada huo.
Mmoja wa Washiriki wa Mkutano huo, aliyejitambulisha kwa jina la Anna Anatoli alisema ulimwengu umekosa hofu ya Mungu  na ndiyo maana imefika hatua wanadamu wanaweka mikakati ya kutowesha Uhai bila kuwa na hofu ya kwamba kazi hiyo ni ya kwake Mungu Muumba ambaye yeye ni asili ya Uhai wenyewe.
“Hatuna sababu ya kushabikia mambo kutoka mataifa ya mbali ambayo kwao wamefika mahali wameona Uhai si zawadi kutoka kwa Mungu kwenda kwa mwanadamu, natamani kuona tunabaki na vyakwetu huku tukiendelea kuwajengea hofu ya Kimungu watoto wetu,”alisema Anna.
Kwa upande wake Betty Sammaye aliwataka wazazi kusimama na kuwapeleka watoto wao Kanisani kwani Mtoto akikuwa kwenye uwepo wa kumcha Mungu ataweza kusimama na kujitetea na Neema ya Mungu itakuwa ndani katika kumwongoza.
Betty amewataka wazazi kuchukua muda kuzungumza na watoto wao, kwani vitu vinabadilika mno kila siku, na kamwe wasikubali watoto wao kutoka nje ya himaya yao bila kufahamu kwa kina ni wapi hasa wanakwenda na wanakwenda kufanya nini.
Muswada huo wa Afya ya Kizazi na Ujinsi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Mwaka 2021 unaelezwa kukiuka maadili, Utu na Dini za watu wa Jumuiya ambao una vipengele vinavyochochoa ngono kwa watoto na Vijana, na pia utoaji mimba.
Na ikiwa muswada huo utaachwa upite, basi itazilazimu nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutunga Sheria kulingana na matakwa ya muswada huo.

NAIROBI, Kenya

Askofu Mkuu Hubertus Maria van Megen, Balozi wa Kitume nchini Kenya na Sudan Kusini, amewataka waamini kujitahidi kupyaisha nyuso zao na kujitoa katika huduma kwa wengine, ikiwa ni njia mojawapo ya kufanya dunia kuwa mahali bora kwa kila mtu.
Katika mahubiri yake wakati wa sherehe za kuitisha kwa ajili ya kuanza kwa Chuo Kikuu cha Tangaza mwaka wa masomo 2022/2023, Askofu Mkuu Megen, alitoa mfano wa Zaburi 104:30 na kuwataka Wakristo kubadili mienendo yao na kuishi kulingana na sheria. viwango ambavyo Mungu huweka katika Neno Lake.
“Mara nyingi tunaimba na kumsihi Roho Mtakatifu aufanye upya uso wa dunia, lakini vipi kuhusu uso wako? Kwa nini usiseme, “Bwana, itume roho yako na uufanye upya uso wangu?”
Askofu Mkuu Megen alisema kuwa ni wakati stahiki kwa waamini na wanafunzi hao kumwomba Roho wa Mungu kwa hekima na mwelekeo katika kutimiza malengo ya mwaka mpya wa masomo wa chuo hicho kinachomilikiwa na Wakatoliki.
Aidha, aliwataka Wakatoliki kumruhusu Roho Mtakatifu kuwaongoza katika utume wao, huku akiwatahadharisha kuhusu madhara yanayoweza kuepukika ya udhaifu wa kibinadamu, ambao mara kwa mara huwafanya kutafuta anasa za dunia.
“Wanadamu wana mwelekeo wa kuuumba ulimwengu wao usiolingana na kanuni za Neno; tunashawishiwa sana na ulimwengu na kuishia kuishi kulingana na mahitaji ya mwili,” alisema Askofu Mkuu Megan.
Askofu Mkuu Megen alihusisha zaidi Zaburi na amri kuu zaidi, akisisitiza kwamba ilikuwa njia pekee ya kupata ushirika wa kweli na Mungu.
Mwakilishi huyo wa Kitume alisisitiza mafundisho ya Roho Mtakatifu, kuhusu kumtumikia Mungu huku akizungumzia ongezeko la watu, wakiwemo wa kidini, kuingia katika makundi na matabaka ya kijamii.
Askofu Mkuu Megen alilielezea Kanisa kuwa ni taasisi ya kibinadamu inayoundwa na watu ambao, kama watakatifu, wanaweza kukabiliwa na kasoro za kibinadamu.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, akimpatia Sakramenti Takatifu ya Kipaimara mmoja wa vijana waliopokea Sakramenti hiyo, katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Imakulata, Upanga, Jimboni humo, (kulia kwa Kardinali) ni Paroko wa Parokia hiyo Padri Casmir Kavishe. (Picha na Mathayo Kijazi)

Na Mathayo Kijazi

Mwadhama Polycarp Kardnali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewasihi Waimarishwa wa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kutambua kwamba kwa sakramenti hiyo wanatumwa kuitangaza habari njema kwa Mataifa.
Kardinali Pengo aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 37, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Imakulata, Upanga, Jimboni humo.
“Ndugu zangu mnaoimarishwa leo katika Sakramenti hii Takatifu, tambueni kwamba mnapopakwa mafuta, mnatumwa kwenda kuifanya kazi ya Mungu ya kuitangaza habari njema kwa Mataifa, yaani mnatumwa kuwatangazia masikini habari njema,” alisema Kardinali Pengo, na kuongeza,
“Masikini hao wanaotangaziwa habari njema, siyo umasikini wa kukosa fedha, kwa sababu kama ni umasikini wa fedha, hata Yesu Kristu mwenyewe alikuwa ni masikini.”
Aidha, Kardinali Pengo aliwasihi vijana hao kufahamu kwamba hata kama ni masikini na wenye kujiona kuwa hawana thamani maishani mwao, lakini Mungu hajawaacha, hajawatupa na wala hajawalaani.
Kardinali Pengo aliongeza pia kuwa heri watu walio masikini ambao wanamtegemea Mungu, kuliko matajiri ambao wanadhani kwamba wana kila kitu, na hivyo hawahitaji uwezo wa Mungu katika maisha yao.
Alisema pia kuwa kuitangaza habari njema ni pamoja na kuyaishi Maandiko Matakatifu, kwani mtu hawezi kuitangaza habari njema kwa kutenda kinyume na mafundisho ya Mungu.
Kardinali Pengo aliwasihi wazazi na walezi kuwasindikiza watoto wao katika kumsifu na kumtukuza Mungu, ili waendelee kudumu kuwa Askari hodari wa Kristo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Casmir Kavishe alimshukuru Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa kufika Parokiani hapo na kuwapatia Sakramenti hiyo Takatifu vijana 37 katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu.
Padri Kavishe aliwashukuru Makatekista na waalimu wote walioshiriki katika kuwafundisha vijana hadi kuwa imara na kuweza kupokea Sakramenti Takatifu, huku akiwasihi vijana hao kuendelea kudumu katika yale yote waliyofundishwa.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wadau na Watetezi wa Uhai kutoka Shirika la Kutetea Uhai, Pro-Life Tanzaania, wamesema kwamba mengi yaliyoandikwa katika Barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II (Familiaris Consortio 1981) kuhusu Nafasi ya Familia katika Ulimwengu wa leo, hayaonekani katika maisha halisi, kwani dunia ya sasa ni ya kizazi kipya.
Hayo yamejiri katika Kongamano la  Shirika hilo liliofanyika Jijini Dar es Salaam, na ambalo lilijadili barua hiyo ya Kichungaji.
Katibu wa Pro-life Tanzania, Godfrey Rahabu Mkaikuta amesema kuwa maisha yamebadilika, hivyo wamefikiri ni vema kupeleka ujumbe wa barua hiyo ya Kichungaji kwa vijana, na hivyo wamelenga kuanza na Vijana katika Vyuo Vikuu.
Alisema pia kuwa mpango huo unakusudiwa kuanza kutekelezwa mapema Januari mwakani katika Vyuo vya Kati, Vidogo na Vyuo Vikuu vya Kanisa Katoliki, na tayari wameshajipanga katika makundi namna ya kufikia Vijana hao katika Vyuo.
Mkutano huo uliokuwa ukijadili Insikliko ya Baba Mtakatifu, ulishirikisha watetezi wa uhai kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda Zambia, Zimbabwe na Rwanda, uliotanguliwa na Misa Takatifu wakati wa ufunguzi iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu.
Askofu Mchamungu aliwapongeza watetezi hao wa uhai kwa juhudi na hamasa kubwa wanayofanya katika kutetea uhai bila kuchoka wala kukatishwa tamaa, na hivyo kuwataka kuendelea na moyo huo bila kuchoka.
Katika mahubiri yake, Askofu Mchamungu alieleza umuhimu wa ndoa na familia katika maisha ya binadamu, kwani familia lazima imsaidie mwanadamu kutambua wito wake mwenyewe, na kuishi kadri ya maongozi ya Mungu.
Kanisa lazima litambue muhimu wa kuweka programu zinazolinda uhai, na kustawisha ndoa na familia kwa ajili ya ustawi wake, na pia ustawi wa taifa kwa ujumla wake.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Afisa Habari wa Klabu ya soka ya Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kuwa timu yake imeanza maandalizi ya sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu ya msimu huu, licha ya kwamba bado ni mapema.
Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano maalum, Bwire alisema kwamba wanajivunia maandalizi waliyofanya kabla ya msimu kuanza na sasa wana kikosi imara.
Alisema pia kuwa wamesajili kikosi kizuri ambacho kinaweza kuhimili ushindani katika Ligi ikilinganishwa na timu zingine.
“Sisi tuna kikosi kizuri, na falsafa yetu siku zote ni kuwa na wachezaji wazawa.Hicho ndicho kitu tunachojivunia.Wanaotudharau wakija kucheza na sisi watakiona cha mtema kuni,”alisema Bwire.
Alisema kwamba hakuna timu iliyoandikiwa kupata ubingwa siku zote kwa sababu ubingwa ni haki ya kila timu inayowania, na kwamba hawapo kwenye Ligi kwa ajili ya kupoteza muda au kusindikiza tu timu zingine.
“Huwa tunasikia tu eti kuna timu zimesajili Wazungu, zingine Wabrazil, zingine Wajapan, lakini sisi hatutetereshwi na mbwembwe zao.Sisi tutawaonyesha uwanjani”       
Alisema kuwa kuna timu zinawadharau, lakini mechi inapokaribia matumbo yao yanavurugika kwa hofu ya kufungwa.

DAR ES SALAAM

Na John Kimweri

Imeelezwa kuwa kiburi cha elimu ni sababu mojawapo inayowafanya watu kuacha kumwamini Mungu, na kutegemea utashi wao na mali walizonazo, kama jawabu katika maisha.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba, wakati akitoa homilia yake kwenye Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 125, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Martin wa Porres, Mwananyamala.
Askofu Musomba (pichani) alisema kuwa kiburi ni dhambi na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani, akiwataka waamini  kuhakikisha licha ya elimu walizonazo, lakini watambue uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa sababu bila yeye, hawawezi kufanya kitu chochote.
“Kiburi cha usomi kinaweza kusababisha mtu akaona kuwa hakuna Mungu, na eti anajiweza yeye mwenyewe bila ya msaada wa Mungu, kiburi ni dhambi kubwa sana na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani,” alisema Askofu Musomba.
Askofu  Musomba, alieleza kuwa kiburi kingine ni cha maendeleo na kiroho, akiwaonya waamini wanaojiona kuwa wamekamilika kuliko wengine kuacha kufanya hivyo.
Aliwakumbusha wazazi kuhakikisha kuwa wanapowarithisha  watoto wao mali na vitu vingine vya thamani, wasisahau kuwarithisha imani, kwani hilo ni jambo lisiloharibika wala kuchakaa.     
Aidha, aliwataka waimarishwa kutambua kwamba wanapopokea Sakramenti hiyo, Roho Mtakatifu anaingia ndani mwao na kuwafanya kuwa wapya katika kila jambo, huku akiwaasa wazazi nao kuwa na desturi ya kusali pamoja, na pia kusoma Neno la Mungu na watoto wao.  
Alisema kwamba Roho Mtakatifu ni nyenzo ya utume ya kuwasaidia waamini kuinjilisha hapa duniani, na kudai kuwa utume wa kweli unatakiwa kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Kwa mujibu wa Askofu  Musomba, utii unamfanya mtu akabidhi utashi na kuwa mtii kwa Mungu mwenyewe, na kuongeza kwamba pia utii huendana na usikivu, ambapo mwisho wake huleta unyenyekevu kwa mtu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia hiyo, Jeremia Mchomvu, alisema kuwa Parokia hiyo ina jumla ya waamini 6757, kutokana na sensa iliyofanyika Januari mwaka 2020.
Alisema kuwa Parokia kwa sasa ina mpango wa kununua nyumba mbili, ili kupanua eneo la kanisa.

Padri Germine Laizer akiwavisha rozari baadhi ya wanachama wapya wa Chama cha Wajane na Wagane

Dar es Salaam

Na Benedikto Agostino

Wajane na Wagane nchini wametakiwa kuendelea kuishi fadhila za Mtakatifu Monica bila kukata tamaa, na kumshukuru Mungu kwa maisha ya wenzi wao waliotangulia mbele ya haki, bila kusahau kuwaombea hao na watoto waliochwa na wazazi wao kila mara.
Hayo yalisemwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Kamili, Yombo Kiwalani, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaaam, Padri Germine Laizer, wakati akihubiri katika Adhimisho la MIsa Takatifu ya Somo wa Wajane na Wagane, Mtakatifu Monica, iliyofanyika kwa ngazi ya Jimbo katika Parokia hiyo.
Katika homilia yake, Padri Laizer aliwakumbusha wajane na wagane kutambua maisha ya Mtakatifu Somo wao, Monica, kama mjane aliyeishi katika mateso na maisha mabaya ya mwanae Augustino, lakini licha ya kupitia changamoto hizo, hakukata tamaa hadi mtoto wake alipoongoka, na sasa ni Mtakatifu.
Alisema kwamba pamoja na ujane na ugane wao, ni muhimu kuishi fadhila ya unyenyekevu, kwani ni ishara ya itii mbele ya Mungu na watu, na hasa kila mmoja anapojishusha na kuwa kama mtoto mdogo.
“Maisha yetu yana maana kubwa kila tunapojinyenyekeza na kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani kila mmoja wetu anadaiwa kadri anavyokuwa mkuu kunyenyekea,” alisema Padri Laizer.
Aliongeza kusema kwamba watu wengi walioishii fadhila hiyo ya unyenyekevu wamepata kibali mbele za Mungu, na kujibiwa sala na maombi yao na kumbukumbu lao linaishi hata hivi leo.
“Tabia ya kiburi na majivuno ni kinyume cha unyenyekevu, na mara baada  ya mtu kuwa na maisha hayo, hali ya mtu hubadilika na kuharibika kabisa,” alisema Padri Laizer.
Alisema kuwa tukiongozwa na unyenyekevu ni lazima tufike mbali, kwani fadhila hiyo inalipa, na hakuna aliyeishi hali hiyo ambaye hakufanikiwa kamwe.
“Ni wazi unyenyekevu unapokosekana popote, yanatawala mafarakano, uogomvi na majigambo, hali inayotawanya kundi na kupoteza amani na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu,” alisema padri huyo.
Aliwataka waamini kuiga mfano mzuri wa mtu pekee aliyeishi fadhila ya unyenyekevu, ambaye ni Bikira Maria ambapo pamoja na magumu aliyoyapitia, aliyaweka mengi moyoni mwake.
Naye Mwenyekiti wa Wajane na Wagane Jimbo, Sweetbeter Mzungu alimshukuru Paroko wa Parokia hiyo, kwa utayari wake wa kupokea ujio wa sherehe hizo, na kuwapongeza wanachama wote waliojitokeza kufanikisha shughuli hiyo muhimu ambayo hufanyika mara moja kila mwaka.
Sweetbeter alisema kwamba moja ya mafanikio makubwa kwa sasa ni hatua waliopiga kutoka kutambuliwa kama kikundi na kuwa chama cha kitume ingawa bado changamoto kubwa ni mwitikio, hasa wa kupokelewa katika Parokia zote.
Alibainsha kuwa mara nyingi watu wengi hawapendi kujitambulisha kama wajane au wagane, na hali hiyo hutokana na kutokujikubali au kuipokea baada ya kuondokewa na wapendwa wao, na hasa wagane.

MOSHI

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Jeshi la Polisi (Inspector General of Police: IGP) nchini, Camillus Wambura amesema kwamba takwimu za makosa makubwa ya jinai nchini yameongezeka katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2022.
IGP Wambura aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha maofisa wa waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, na makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi, akisema kuwa makosa hayo yameongezeka kutoka 24,848 kipindi kama hicho mwaka 2021 hadi makosa 27,848, sawa na ongezeko la asilimia 11.2.